Dar es Salaam. Mahakama Kuu imelikataa ombi la timu ya Tout Puissant Mazembe Englebert Sarl (TP Mazembe) ya Democratic Republic of Congo (DRC) ya kutaka itoe amri ya kuzuia zaidi ya Sh1.5 bilioni za mchezaji wa kimataifa wa Tanzania.
Uamuzi huo ulitolewa Agosti 16,2024 na Jaji Arnold Kirekiano, alisema kutolewa kwa amri ya kuzuia fedha hizo, itakuwa sawa na kuzuia michakato ya mahakama, ambayo mwombaji tayari amecheza kwa busara kuheshimu sheria.
Julai 11,2019 mchezaji huyo wa kimataifa wa Tanzania, Suzana Singano Yahaya maarufu, aliingia mkataba wa kuichezea TP Mazembe, lakini hata hivyo ukasitishwa na kutokana na hilo akimbilia Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kudai haki yake.
Chemba ya usuluhishi wa migogoro ya Fifa ilimpa ushindi mchezaji huyo wa kitanzania na kuamuru alipwe Dola 585,000 za Marekani ambazo ni sawa na zaidi ya Sh1.57 bilioni za Tanzania, kulingana na kiwango cha Dola 1 kwa Sh2,700.
Fedha hizo zilikuwa ni fidia kwa ajili ya kukiukwa kwa mkataba huo, mishahara, malimbikizo ya mshahara na riba na mchezaji huyo yuko mbioni kutekeleza uamuzi huo wa Fifa na tarehe ya malipo hayo ilipangwa kuwa Agosti 15,2024.
Ili kuzingatia tuzo hiyo ya Fifa, TP Mazembe katika maombi hayo namba 19685 ya 2024, iliiagiza benki yake kuhamisha fedha hizo kwenda kwenye akaunti ya mchezaji huyo iliyopo benki ya NMB PLC iliyopo Bank House Jijini Dar es Salaam.
Kesi ya mabilioni juu ya kesi
Kwa upande mwingine, TP Mazembe inadai uwepo wa kugushi na kesi ya jinai ilifunguliwa dhidi ya mchezaji huyo katika Mahakama Kuu ya Lubumbashi iliyopo jimbo la Haut-Katanga huko DRC ambayo timu hiyo inadai kushinda shauri hilo.
Katika kiapo chake, timu hiyo inasema mahakama Kuu ya Lubumbashi iliipa tuzo ya Dola 650,000 za Marekani, sawa na Sh1.75 Bilioni za Tanzania kama fidia kwa timu hiyo kutokana na uhaibifu uliofanywa na mchezaji huyo na gharama za kesi.
Jaji alisema ni muhimu kufahamu muombaji katika maombi hayo (TP Mazembe) yuko mbioni kusukuma utekelezaji wa tuzo hiyo kupitia maombi namba RC35507 ya 2024 aliyoyafungua katika mahakama kuu ya Lubumbashi nchini DRC.
Hivyo katika maombi yake namba 19685 ya 2024 aliyoyawasilisha Mahakama Kuu ya Tanzania, TP Mazembe aliiomba itoe zuio la muda la kumzuia mchezaji huyo wa Tanzania, kutohamisha Dola 585,000 zilizopo katika akaunti yake benki ya NMB.
TP Mazembe iliomba fedha katika akaunti hiyo inayosomeka ‘Ramadhan Yahaya Singano’ zisihamishwe wakati wakisubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi yao namba 19536 ya 2024 ya kuomba kusajili tuzo ya Mahakama Kuu Lubumbashi.
Wakati maombi hayo yalipoitwa kusikilizwa kwa upande mmoja (ex parte) mbele ya Jaji Kirekiano Agosti 15,2024, mawakili Ferdinand Makore na Kulwa Shilemba waliegemea kiapo cha Kalomba Eid Solomon wa timu hiyo ya TP Mazembe.
Mawakili hao waliiambia mahakama kuwa muombaji katika shauri hilo ambaye ni TP Mazembe amekwishaiagiza benki yake huko Lubumbashi, kuhamisha Dola 585,000 za Marekani kwenda kwenye benki ya NMB PLC ya mchezaji huyo.
Kulingana na hoja zao, endapo fedha hizo hazitazuiwa, mchezaji huyo ataachiliwa wakati wao (TP Mazembe) wana tuzo ya mahakama Kuu Lubumbashi kupitia kesi namba RC35507 ya 2024 ambapo mahakama imeamuru walipwe Dola 650,000.
Katika uamuzi wake alioutoa leo Agosti 16,2024, Jaji Kirekiano alisema amepitia ombi la TP Mazembe pamoja na kiapo chao na kwamba kinachoonekana, pande mbili hizo zina migogoro miwili ambayo inashikiliwa katika maeneo mawili.
Jaji Kirekiano alisema waombaji, TP Mazembe wanataka tuzo ya Dola 650,000 za Marekani waliyoipata baada ya kushinda kesi katika mahakama kuu Lubumbashi kupitia shauri namba RC35507, isajiliwe katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
“Hivyo, maombi yanayoombwa ni kuhusiana na fedha zilizotumika kutekeleza uamuzi wa Fifa, ambao mwombaji alitekeleza kwa kumlipa mlalamikiwa Dola 585,000 za Marekani,” alisema Jaji katika uamuzi wake huo na kuongeza kuwa:-
“Hii ni kusema kuwa, kwa upande mmoja, muombaji (TP Mazembe) ameheshimu na kutekeleza amri ya Fifa, lakini kwa upande mwingine anataka kuzizuia (Dola 585,000) alizozituma”
Jaji alisema inaweza kuelezwa kuwa kuna hoja za mabishano dhidi ya mjibu maombi (Suzana). Tukienda na maombi ya muombaji, yanaonekana yako dhidi ya benki inayotunza fedha za Suzana na sio Suzana mwenyewe,”alisema Jaji.
Akinukuu ombi hilo, Jaji alisema “amri (ombi) ya muda kuizuia benki ya mjibu maombi (Suzana) isiruhusu kutolewa kwa Dola 585,000 za Marekani zilizopo benki ya NMB PLC Dar er Salaam, Tanzania kwa jina la Ramadhan Yahaya Singano”
Jaji alisema hakuna mahali benki ya mjibu maombi imeombwa katika maombi hayo wala katika ombi la kusajili hukumu ya nje ya nchi, kwa hiyo amri hiyo ikitolewa itakuwa mbaya kwa vile benki ya mjibu maombi itakuwa haijasikilizwa.
“Hili liko wazi kwa sababu hakuna maombi dhidi ya benki (NMB) alisema Jaji Kirekiano na kuongeza kuwa kutolewa kwa amri ya kuzuia fedha hizo, itakuwa ni sawa na kuzuia michakato ya mahakama, ambayo muombaji tayari anaitumia.