Mtaalamu wa IT, wenzake mbaroni utengenezaji noti bandia

Musoma. Polisi mkoani Mara wanawashikilia watu watatu akiwepo mtumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora kwa tuhuma za kupatikana na noti bandia na mtambo wa kuzitengeneza.

Wanatuhumiwa kupatikana wakiwa na noti bandia za Sh7.7 milioni ambazo walikuwa wakijiandaa kuziingiza mtaani.

Taarifa kuhusu watuhumiwa hao imetolewa Agosti 16, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase alipotoa taarifa ya utendaji kazi wa jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Kamanda Morcase amesema awali jeshi hilo liliwakamata watu wawili wakiwa katika nyumba moja ya kulala wageni mjini Musoma na baada ya kuwapekua waliwakuta wakiwa na noti 857 za bandia.

“Walikuwa na noti 753 zote za Sh10,000 zikiwa na namba LH6792622 na noti 104 zote za Sh2,000 zikiwa na namba JX0271439. Baada ya kufanya nao mahojiano ndipo wakamtaja mwenzao ambaye ni mtumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, tulimkamata akiwa na mtambo wa kutengeneza noti bandia,” amesema.

Amewataja watuhumiwa kuwa ni Frank Mambo ambaye ni mtaalamu wa IT katika hospitali, aliyekamatwa mkoani Tabora baada ya kutajwa na wenzake.

Wengine waliokamatwa mjini Musoma ni Emmanuel Atanas (27), mkazi wa Kihonda Maghorofani mkoani Morogoro na Jovin Samson (17), mkazi wa Nyamakokoto wilayani Bunda.

Amesema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.

Katika hatua nyingine, Kamanda Morcase amesema katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita jeshi hilo limekamata zana haramu za uvuvi 49 zilizokuwa zikitumiwa na wavuvi ndani ya Ziwa Victoria.

Amesema ili kutokomeza uhalifu ndani ya mkoa huo, jeshi hilo limeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushirikisha jamii ili kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya uhalifu, lengo kuu likiwa kuzuia uhalifu usitokee.

“Tunataka vitendo vya uhalifu visitokee, yaani tuwe na uwezo wa kuvizuia kabla ya kutokea kwani madhara yake ni makubwa, hivyo pamoja na kupambana navyo tumeona tuelekeza nguvu kubwa katika kuzuia,” amesema.

Amesema moja ya mikakati waliyojiwekea ni kushirikisha makundi ya kijamii likiwamo la bodaboda.

Kamanda amesema katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita jeshi hilo limetembelea vijiwe 186 vya bodaboda ndani ya mkoa huo.

“Hivi ni vijiwe rasmi vinatambuliwa na Jeshi la Polisi, tumeweka utaratibu kila vijiwe vitano vinakuwa na askari mmoja anayevilea, hapo tunazungumza na hawa vijana juu ya wao wenyewe kujitambua, usalama barabarani na jukumu lao katika mapambano dhidi ya uhalifu. Tayari tunaona kuna mafanikio makubwa katika hili,” amesema.

Amesema katika kipindi hicho cha mwezi mmoja uliopita wamekamata watuhumiwa 357 wa makosa mbalimbali ya uhalifu, yakiwamo ya ukatili wa kijinsia, watumiaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya, wezi wa mifugo, na uhalifu mwingine.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamepongeza jeshi hilo kwa uamuzi wa kushirikisha makundi mbalimbali katika jamii, hatua ambayo wanaamini itasaidia kutokomeza uhalifu.

“Nimemshuhudia kamanda mwenyewe akitoa elimu kwenye mikutano ya hadhara ambayo siku hizi inaandaliwa na polisi, lakini mbali na mikutano, kamanda pia amekuwa akitembelea mitaa mbalimbali ya manispaa kila siku kuzungumza na viongozi wa mtaa na wananchi.

“Nadhani hili ni jambo la kupongeza, wananchi watakuwa tayari kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na kuliwezesha jeshi hilo kuchukua hatua,” amesema Bosco Odhiambo.

Masenti Josiah, amesema wahalifu wanatoka katika jamii, hivyo jeshi hilo likiendelea na utaratibu wa kuwa na mahusiano mazuri na jamii upo uwezekano mkubwa wa jamii kutoa taarifa za wahalifu ili wachukuliwe hatua, hali itakayowezesha kukoma vitendo vya kihalifu.

Related Posts