NYUMA YA PAZIA: Shika peni na karatasi Ligi ya mfalme Charles

NA imerudi tena. Wakati inaondoka unaweza kudhani haitarudi tena hivi karibuni lakini ghafla imerudi tena. Ligi Kuu ya England. Zamani ilikuwa Ligi Kuu ya Malkia Elizabeth lakini baada ya yeye kutoweka duniani amemuachia mwanae Mfalme Charles. Dunia imeanza kusimama upya.

Inanikumbusha katika kikao fulani cha wakubwa wa Ulaya pale Ujerumani kila kiongozi mkubwa alikuwa anajisifu ni bidhaa gani kubwa ambayo taifa lake inasafirisha nje. Kwa majivuno makubwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, Gordon Brown alijibu: “Ligi Kuu ya England”. Hakuna aliyeweza kumbishia.

Na sasa imerudi tena ikiwa na maswali magumu kuliko msimu uliopita. Tuanze na swali gani? Tuanze kwa mwenye Ligi yake kwa sasa. Pep Guardiola. Msimu uliopita kwa tofauti ya pointi moja tu alichukua ubingwa mbele ya Arsenal. Ulikuwa ubingwa wa nne mfululizo. Hakuna timu ambayo imewahi kufanya hivyo katika Ligi Kuu ya England. Hata Sir Alex Ferguson hakuweza.

Pep anaweza kuchukua mara tano mfululizo? Ni swali. Akiweza itakuwa rekodi juu ya rekodi. Wachezaji bado wana miguu ambayo haijachoka? Hapo hapo tunajikumbusha kwamba roho ya timu, Kevin De Bruyne ametimiza miaka 33 kwa sasa. Bado atabakia kuwa yuleyule? Ni kwamba Erling Haaland atabakia kuwa yuleyule?

Wiki iliyopita Bernardo Silva ametimiza miaka 30. Atabakia kuwa yuleyule? Kama yeye na De Bruyne kwa pamoja wana miaka 66. Wataendelea kuwa wale wale? Timu itakuwa na nguvu ile ile? Na katika hali ya kawaida ya kibinadamu, katika ligi yenye ushindani kama Ligi Kuu ya England, City wataendelea kudumu vile vile kwa msimu wa tano mfululizo bila ya kupitiwa na bahati mbaya?

Halafu tuna Mikel Arteta mezani. Hili ni swali la pili. Kwa misimu miwili mfululizo Arsenal wameshindwa kutwaa ubingwa wa England katika dakika za jioni. Hasa zaidi katika msimu uliopita. Arteta ataendelea pale pale alipoishia au atachukua ubingwa au timu yake utashuka kidogo?

Msimu uliopita kuna jambo alidhihirisha. Kwamba msimu mmoja kabla alikuwa hajabahatisha wakati alipoiweka City kikaangoni mpaka alipochemsha dakika za mwisho. Msimu ulioisha alithibitisha kwamba Arsenal itaendelea kuwa pale pale kuipa changamoto City. Kwamba msimu mmoja kabla alikuwa hajabahatisha.

Hata hivyo, hatoshi. Mara nyingi vitu kama hivi tunasema ‘mara tatu’. Hata wakati tunajaribu kukimbia huwa tunahesabu mara tatu kisha wanariadha wanaanza mbio. Yaani ‘moja, mbili, tatu’. Arteta yupo katika tatu yake kwa sasa. Wazungu wanasema ‘it’s now or never’. Ni sasa au sahau kabisa. Tumemsamehe Arteta mara mbili na kulikuwa na sababu nyingi za kumsamehe. Mara ya tatu hatasamehewa.

Mara ya tatu ikitokea yale yale Arteta hatafukuzwa bali itaanza kuaminika kwamba yupo Arsenal kwa ajili ya kutoa changamoto kwa Pep lakini sio kuchukua mataji. Huwa inatokea. Hata katika ngumi kuna bondia ambaye anatoa changamoto zaidi kuliko kutwaa mataji. Kama kuna kocha atatazamwa kwa jicho kali zaidi msimu huu basi ni Mikel.

Halafu kuna joto kali pale Old Trafford. Rafiki yetu, Erik Ten Hag alikuwa amekwishauona mlango wa motoni. Dakika za majeruhi kabisa akasalimika kutoka kwa malaika wa peponi. Ilibakia mechi moja tu muhimu afukuzwe. Dhidi ya Manchester City katika pambano la fainali za FA. Wakati huo alikuwa amekwishaitoa Manchester United katika Top Four. Alikuwa anasubiri afungwe na Manchester City katika pambano la mwisho la msimu wa soka England ili afukuzwe.

Haikuonekana kama angeweza kuifunga City kisha akaendelea kuwepo katika msimu mwingine. Hata hivyo, kwa maajabuajabu akaifunga City na kutwaa taji la FA. United walibadili gia angani baada ya kuondoka Wembley wakiwa na taji la FA. Hii ilikuwa salama ambayo hata baadhi ya mashabiki wa United hawakuipenda. Hata hivyo, ndio ilikuwa imetokea.

Na sasa jicho litakwenda kuwa kali kwa Ten Hag. Anaweza kuirudisha United Top Four? Na kama atairudisha, itakuwa inatoa matumaini kwamba yeye ndiye mtu pekee anayeweza kuipeleka United katika nchi ya ahadi kwa sasa? Huu utakuwa msimu mwingine mgumu kwa Ten Hag ambaye bado mashabiki wengi wa United pamoja na mabosi wao wana wasiwasi naye.

Ameendelea kujaza wachezaji wengi ambao alifanya nao kazi Ajax. Wanatosha katika soka la Uingereza? Msimu mwingine ambao kwa namna moja au nyingine utaendelea kuamua hatua ya Ten Hag. United wanapitia kipindi kigumu. Siku hizi hata kina Brighton hawaoni kama Old Trafford ni uwanja mgumu. Wanahisi ni uwanja wa kuchukua pointi tatu au moja. Ni kipindi cha mateso.

Halafu kuna swali kwa rafiki zetu wa Anfield. Hapa kuna mtihani mgumu na kuna swali gumu kwa mtu anayeitwa Arne Slot. Wakati raia mwenzake wa Uholanzi, Erik Ten Hag anapitia wakati mgumu kupata ufalme wa kurithi kiti cha Sir Alex Ferguson kama kwa wenzake wengi waliomtangulia, Slot ana moja kati ya kazi ngumu duniani.

Kazi ya kurithi kiti cha Jurgen Klopp. Anapoondoka kocha kama Sir Alex Ferguson, au Arsene Wenger, au Pep Guardiola au Jurgen Klopp basi kocha anayefuata anakuwa na kibarua kigumu kukalia kiti. Mbuyu unang’ooka halafu unaambiwa upande mbuyu wako katika mwendo ule ule au kasi ile ile. Sio kazi rahisi.

Slot kama ilivyo kwa Ten Hag ametokea Uholanzi moja kwa moja na kutua katika moja kati ya ligi ngumu duniani. England. Zaidi ya kila kitu amekwenda katika timu ambayo ina presha kubwa. Liverpool. Ataiweza kazi hii? Kung’ara Uholanzi ni jambo moja lakini kung’ara England ni jambo jingine. Uwe mchezaji au uwe kocha hii ni mitihani miwili tofauti. Amuulize Ten Hag.

Zaidi ya kila kitu, Liverpool kuna misingi inakaribia kuanguka pale. Kuna timu mpya ambayo inapaswa kujengwa. Virgil Van Dijik hawezi kuendelea kuwa yule tena wakati huu akikabiliwa na miaka 33. Msimu uliopita tulimuona namna ambavyo alikuwa anakaba kwa macho zaidi. Julai mwakani atakuwa akitimiza miaka 34.

Mo Salah, 32, sio yule tena. Msimu uliopita alionekana kushuka tofauti na misimu mingi aliyotamba England. Slot ni mpya na anatazamiwa kuitengeneza Liverpool mpya. Tayari Klopp aliianza kazi hii lakini hatujui kwanini aliamua ghafla kukaa zake pembeni huku akidai kwamba anaona hana nguvu za kukaa katika benchi tena. Pep alichangia kumchosha. Muulize pia Arteta namna kazi ya kupambana na Pep ilivyo ngumu.

Kama Slot atafanikiwa kuonyesha makali yake basi tutashukuru. Vinginevyo unaweza kuwa mwanzo mpya wa Liverpool kuanza kuhangaika kusaka makocha kila uchao. Ni kama kile kinachotokea Old Trafford baada ya Mkubwa Ferguson kuondoka zake. Umekuwa msiba mzito kwa muda mrefu sasa. Kama Slot akianza vibaya basi huenda ukawa mwanzo mpya wa ‘fukuza ingia’ katika kiti cha Anfield ambacho Klopp alikituliza kwa muda mrefu.

Chelsea? Na wao tuwajadili? Wanachosha. Hatujui wanachotaka. Tajiri yao ni kama amechanganyikiwa hivi. Ananunua wachezaji kila uchao. Kitu kizuri ni kwamba amefuata nyayo za Arsenal kwa kwenda kumchukua mmoja kati ya watu waliowahi kufanya kazi na Pep Guardiola, Enzo Maresca. Itawasaidia? Hatujui. Arsenal imewasaidia kidogo kufuata falsafa za Pep kupitia kwa Arteta.

Labda tumpe muda kidogo Maresca ambaye aliipandisha Leicester City Ligi Kuu kwa mbwembwe. Lakini hata mfuata falsafa mwingine wa Pep, Vincent Kompany aliipandisha Burnley kwa mbwembwe lakini akaishusha daraja msimu uliofuata. Sio kazi rahisi kufuata nyayo za Pep kama makocha wengine wanavyojaribu. Mechi za kirafiki za Maresca kabla ya msimu mpya pia zimetia shaka.

Related Posts