Mwanza. Pamba Jiji na Tanzania Prisons zimeshindwa kufungana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo Ijumaa Agosti 16, 2024 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa Pamba Jiji ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa takribani miaka 23.
Mashabiki wa soka jijini Mwanza wamepata nafasi ya kuishuhudia timu yao ikicheza mechi ya ligi kuu, lakini waliondoka wakiwa hawajashuhudia nyavu zikitikiswa.
Katika mchezo huo uliokuwa na mashambulizi ya kushtukiza kwa pande zote mbili, kipa wa Pamba Jiji ambaye msimu uliopita aliitumikia Tanzania Prisons, Yona Amos, alifanya kazi kubwa ya kuokoa michombo iliyoelekezwa langoni kwake.
Kiwango kizuri alichoonyesha kipa huyo, kilimfanya kukabidhiwa Tuzo ya Mchezaji Bora wa mchezo huo ambapo alikabidhiwa tuzo hiyo na wadhamini wakuu wa Ligi Kuu Bara.
Makocha wa timu zote mbili, Goran Kopunovic wa Pamba Jiji na Mbwana Makata wa Tanzania Prisons, kila mmoja kwa nafasi yake alionekana muda mwingi kutoa maelekezo ambayo mwisho wa siku hayakuleta pointi tatu, wakajikuta wakigawana alama mojamoja.
Baada ya leo, Agosti 24, 2024 Pamba Jiji itaendelea kuwa nyumbani kuikaribisha Dodoma Jiji kwenye Dimba la CCM Kirumba ikiwa ni mechi ya pili, huku Tanzania Prisons ikisafiri tena kwenda Kigoma kucheza dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Agosti 23, 2024.