Sababu mjamzito kuhisi baridi kali wakati, baada ya kujifungua

Dodoma. Suala la kupata mtoto ni jambo linalomfurahisha kila mwanamke, lakini ikumbukwe kwamba furaha hiyo hutokana na mapito kadhaa wakati wa ujauzito wake.

Lakini cha kufurahisha, mama akishajifungua, basi husahau magumu yote aliyopitia tangu kubeba ujauzito mpaka kufikia hatua ngumu zaidi ya kujifungua mtoto wake.

Mwananchi imezungumza na baadhi ya wanawake kutaka kufahamu ni hali gani wanazozipitia kipindi cha ujauzito ambazo wanakumbuka.

Miongoni mwao wanasema ni pamoja na ile ya kujisikia baridi mwili mzima, hali hii huwakumba wajawazito wengi.

Hata hivyo, baadhi yao wamekiri kupitia hali hiyo hasa wanapokaribia kujifungua na baada ya kujifungua iwe ni kwa njia ya kawaida au ya upasuaji na hawajui sababu ya kupata hali hiyo.

Baadhi ya wanawake waliozungumza na Mwananchi wanasema baridi hiyo huwa si ya kawaida na inasababisha mwili wote kutetemeka na meno kugongana.

Mariam Mhoga, ambaye alijifungua kwa upasuaji, anasema alianza kuhisi baridi kali wakati anaandaliwa kuingia kwenye chumba cha upasuaji mara tu alipotundikiwa dripu ya maji.

Anasema hali ya hewa ilikuwa kawaida, haikuwa na baridi kali kiasi kwamba hata kama asingevaa nguo asingeweza kuihisi, lakini wakati maandalizi yakiendelea, hususan baada ya kuwekewa maji ya dripu kwa ajili ya upasuaji, hali ilizidi na alitamani afunikwe blanketi ili apate joto.

Anasema hali hiyo iliendelea hata baada ya kujifungua kwa zaidi ya dakika 30, mwili wote ulikuwa wa baridi.

“Hii hali iliniogopesha, nilikuwa siwezi kufanya kitu chochote, baada ya kujifungua niliomba wanifunike mablanketi mengi ili nipate joto, nashukuru Mungu baada ya nusu saa hali yangu ilirudi kawaida,” anasema Mariamu.

Naye Bertha Msihi anasema alishikwa na baridi baada ya kuambiwa anywe maji mengi kwa ajili ya kuharakisha uchungu baada ya chai aliyokuwa anakunywa kumchubua mdomo.

“Nilikunywa chai takribani chupa nne kubwa mpaka mdomo ukababuka na kutoa vidonda, nilishindwa kuendelea kuinywa, ndipo daktari akanitaka ninywe maji mengi, matokeo yake nilijisikia baridi kali wakaamua kunitundikia dripu mbili za maji,” anasimulia Bertha.

Anasema alipotundikiwa dripu hizo alishikwa na baridi kali na kuanza kutetemeka akiwa kwenye kitanda cha kujifungulia, hali iliyosababisha wakunga kumfunika mashuka na mablanketi ili kumpa joto, lakini haikusaidia.

Anasema ile baridi iliendelea mpaka alipojifungua na kukaa saa nzima, ndipo aliporudi kwenye hali yake ya kawaida.

“Nilikuwa nasikia baridi kali, hadi nilishindwa kumnyonyesha mtoto, lakini baada ya saa moja kupita nilirudi kwenye hali yangu ya kawaida na ile baridi sikuisikia tena,” anasema Bertha.

Wakizungumzia hali hiyo, wataalamu wa afya wanasema mara nyingi huwakuta baadhi ya wanawake wanapojifungua na haina madhara yoyote kiafya.

Muuguzi kutoka Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania, Rehema Msanjila anasema hali hiyo huwa inasababishwa na misukosuko na uchungu wa kuleta kiumbe kipya duniani.

Muuguzi huyo anasema baridi hiyo husababishwa na uchungu mkali wanaoupata wanawake wakati wa kujifungua kwa sababu hutumia nguvu kubwa kusukuma mtoto kusudi atoke tumboni.

Msanjila anasema baada ya mama kujifungua, mwili wake hupoa na kuanza kusikia baridi kwa sababu ile misukosuko inakuwa imeisha.

“Pia kuna damu nyingi ambayo hutoka wakati wa kujifungua ambayo pia husababisha mwili kupoa kabla ya kurudi kwenye hali yake ya kawaida, kwa sababu hii hali hudumu kati ya dakika tano hadi dakika 60,” anasema Msanjila.

Anasema hakuna madhara yoyote yanayosababishwa na baridi hiyo kwa kuwa huisha yenyewe au kwa kunywa vinywaji vya moto kama vile chai, uji, maji ya moto na kuvaa mavazi ya kuleta joto.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na afya ya uzazi kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dk Israel Soko anasema kinachosababisha baridi kwa wanawake wanaojifungua ni sindano za kuzuia damu isitoke baada ya kujifungua na dripu za maji wanayotundikiwa wakati wa kujifungua.

Anasema dripu za maji wanazotundikiwa zina maji ya baridi ambayo husababisha mwili kupoa na kuleta baridi kali.

Anasema kwa sasa wana mpango wa kuanza kutumia dripu zenye maji ya uvuguvugu sawa na joto la mwili, ili kuwaepusha na baridi ambayo huwakuta kwa kutundikiwa dripu zenye maji ya baridi.

Anasema pia sindano wanayochomwa kwa ajili ya kuzuia damu kutoka baada ya kujifungua, husababisha mwili kupata baridi kwa sababu ya ile damu inayorudi mwilini.

“Baada ya kujifungua wanawake huwa wanatokwa na damu nyingi, kwa hiyo ile sindano wanayochomwa kwa ajili ya kuzuia damu isitoke kusababisha damu iliyopo kwenye placenta kurudi mwilini na kile kitendo huwa kinasababisha mwili kupoa na hivyo mama kuhisi baridi kali,” anasema Dk Soko.

Anasema si kila mwanamke anayejifungua huhisi baridi hiyo, kuna wengine huwa hawasikii kabisa na kwa wanaoipata, huwa inadumu kutegemeana na mwili unavyoipokea na hudumu kati ya dakika tano hadi 30 na haina madhara yoyote kiafya.

Related Posts