Tanzania yajipanga kunufaika na soko la umeme Afrika Mashariki

Kampala, Uganda. Tanzania imejipanga kuhakikisha inatumia fursa ya uwepo wa soko la pamoja la mauziano ya umeme kwa nchi wanachama mashariki mwa Afrika (EAPP) kwa kuhakikisha inaunganisha miundombinu yake ya kusafirisha umeme kwa nchi wanachama.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, wakati wa mkutano wa 19 wa nchi wanachama wa umoja huo uliowakutanisha mawaziri wa nishati na makatibu wakuu, jijini Kampala, Uganda.

Mkutano huo umezungumzia masuala mbalimbali ikiwemo kupitisha mabadiliko ya muundo wa kiuongozi wa EAPP, kuridhia kanuni na taratibu za kiuendeshaji, sambamba na kuridhia uwepo wa kitengo huru cha masoko kinachojitegemea kusimamia soko la pamoja la mauziano ya umeme kwa nchi wanachama.

“Nafurahi kuona kuwa tumefikia muafaka kwenye masuala ya msingi kwenye kikao cha mawaziri wa nishati, hususani uwepo wa kitengo huru cha masoko kinachojitegemea kwa ajili ya kusimamia mauziano ya umeme.

“Kwa kuwa Tanzania tutakuwa na umeme kutoka mradi wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), tutatumia vema fursa hiyo kuwauzia umeme nchi wanachama pale tutakapokuwa na ziada na sisi kununua tutakapokuwa na upungufu,” amesema Dk Biteko.

Katika kufanikisha hilo, Dk Biteko amesema tayari miundombinu wezeshi inaendelea kuwekwa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili kujiandaa kuingia kwenye soko la pamoja, ambapo laini kubwa ya kuunganisha Tanzania na Kenya kupitia Namanga imeshajengwa na imekamilika na ile ya kuunganisha Tanzania na Zambia (Taza) imeshaanza kujengwa na itakamilika ifikapo 2026.

Mwenyekiti wa sasa wa soko hilo, Dk Ruth Ssentamu, amesema EAPP imeridhia ushiriki wa makatibu wakuu wa nishati kutoka nchi wanachama kushirikishwa katika muundo wa kiutawala wa EAPP kwa ajili ya kusaidia kuchakata na kupitia taarifa kutoka kwa watendaji wa kisekta kabla ya kupelekwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri la nchi wanachama kwa maamuzi.

Aidha, Ssentamu ambaye ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini nchini Uganda, amesema maazimio hayo yamefikiwa kufuatia makubaliano ya mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri uliofanyika Kenya kuhusu umuhimu wa kupitia mapendekezo ya uendeshaji wa shughuli za EAPP.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema pindi uuzaji wa umeme kwenye soko la pamoja utakapoanza, utatoa nafasi za ajira kwa nchi wanachama wa EAPP pamoja na kubadilishana wataalamu hususan kwenye miradi ya kusafirisha umeme na hivyo kuiongezea Tanesco mapato na hatimaye kutoa nafasi ya ukuaji wa pato la Taifa.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa Baraza la Mawaziri wa Nishati uliongozwa na Dk Doto Biteko ukihusisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mipango, Utafiti na Uwekezaji Tanesco, Renata Ndege, pamoja na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts