Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu, kondakta Abubakari Msawa(41) maarufu kama Ustadh kwenda jela miaka 15, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha vipande vitatu vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Sh35 milioni.
Ustadh anadaiwa kusafirisha nyara hizo alizokuwa amezificha ndani ya bengi la nguo, bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.
Hata hivyo, kutokana na kukaa kwake gerezani kwa muda miaka saba tangu alipofikishwa mahakamani hadi kutolewa hukumu, Mahakama hiyo imempunguzia adhabu na kwamba atatumikia kifungo cha miaka minane gerezani.
Uamuzi huo umetolewa leo, Agosti 16, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi aliyekuwa anasikiliza shauri hilo.
Amesema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka pasina na shaka baada ya kupekea mashahidi saba na vielelezo tisa.
Akisoma hukumu hiyo yenye kurasa 16, Hakimu Msumi amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.
Amesema Msawa anakabiliwa na kosa moja la kupatikana na nyara za Serikali, kinyume cha sheria.
“Ili Mahakama iweze kuthibitisha kuwa mshtakiwa ana hatia lazima upande wa mashtaka uweze kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa kweli alitenda kosa hilo,” ameeleza Hakimu Msumi.
Amesema kuwa kwa ushahidi uliotolewa na shahidi wa namba, tano na namba sita haujaacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alikutwa maeneo ya Kiwalani akiwa na vipande vitatu vya meno ya tembo.
Hakimu Msumi amesema upelelezi wa shauri hilo ulipokamilika, upande wa mashtaka waliwasilisha mashahidi tisa na vielelezo saba kuthibitisha shtaka na mshtakiwa alikutwa na kesi ya kujibu.
Amesema alipopewa nafasi ya kujitetea mshtakiwa alidai hausiki na meno hayo lakini mahakama baada ya kupita ushahidi huo, ilimtia hatiani kama alivyoshtakiwa.
Baada ya kumtia hatiani, Wakili wa Serikali Aaron Titus aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na hasara aliyosababisha kwa taifa.
“Pia kutokana na umuhimu na thamani aliyonayo mnyama huyu aliyeuliwa ambaye anaingiza fedha za kigeni kupitia utalii, tunaomba mshtakiwa apewe adhabu kali,” alieleza wakili Titus.
Hata hivyo, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa tayari amekaa miaka saba gerezani tangu alipokamatwa mwaka 2018.
“Pia nina tegemewa na familia yangu na mama yangu pia ni mzee ana umri wa miaka 85, hivyo naomba mahakama inipunguzie adhabu,” alisema Ustadh.
“Baada ya kusikiliza ombi la mshtakiwa, mahakama hii inaamuru mshtakiwa kupewa kifungo cha miaka 15 jela na katika miaka hiyo itatolewa miaka saba ambayo amekaa gerezani, hivyo mshtakiwa utatumikia miaka minane gerezani na haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo hujaridhika na uamuzi huu,” amesema Hakimu Msumi.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.