Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema kuenea kwa aina mpya ya virusi vya monkeypox (homa ya nyani) vinavyoweza kuambukizwa kwa njia ya ngono, kunahitaji hatua za dharura za kimataifa kudhibiti ugonjwa huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Dharura chini ya Kanuni za Afya za Kimataifa (IHR), Profesa Dimie Ogoina amesema hayo katika taarifa kwa shirika hilo aliyoitoa Agosti 14, 2024.
Kamati hiyo ya wataalamu huru iliitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedross Ghebreyesus kumshauri iwapo mlipuko wa sasa wa Mpox ni suala la dharura la afya ya umma, linalohitaji kushughulikiwa kimataifa.
Profesa Ogoina alisema, “ongezeko la sasa la Mpox katika sehemu za Afrika, pamoja na kuenea kwa aina mpya inayoweza kuambukizwa kwa njia ya ngono ya virusi vya monkeypox, ni dharura, siyo kwa Afrika pekee, bali kwa dunia nzima. Mpox ambayo ilianzia Afrika, ilipuuzwa na baadaye ilisababisha mlipuko wa kimataifa mwaka 2022. Ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia historia kujirudia.”
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa kwenye tovuti ya WHO, imesema Dk Ghebreyesus amefikia uamuzi kuwa ongezeko la maambukizi ya Mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na ongezeko la nchi zinazoathirika barani Afrika, ni dharura ya afya ya umma ya kimataifa (PHEIC) chini ya Kanuni za Kimataifa za Afya za mwaka 2005.
Kujitokeza kwa aina mpya ya virusi hivyo nchini DRC mwaka jana, vya clade 1b, ambayo inaonekana kuenea zaidi kupitia ngono, na kugundulika kwake katika nchi jirani na DRC, kumeelezwa ni jambo linalotia wasiwasi na ni moja ya sababu za kutangazwa kwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa.
Who imesema Julai kulikuwa na taarifa zaidi ya 100 zilizothibitishwa kimaabara kuwa ni za maambukizi ya virusi vya clade 1b katika mataifa ya jirani na DRC, ambayo hayajawahi kuripoti Mpox awali – Burundi, Kenya, Rwanda, na Uganda.
Wataalamu wanaamini idadi halisi ni kubwa kwa kuwa baadhi ya watu wenye viashiria vya dalili za Mpox hawajafanyiwa vipimo.
Akifafanua kuhusu hali hiyo, Dk Allan Tarimo, mtaalamu wa Epidemiolojia nchini, amesema Mpox husababishwa na kirusi na ugonjwa huo husababisha muwasho wenye maumivu, uvimbe sehemu za mwili na homa.
Epidemiolojia ni elimu ya sayansi ya tiba inayohusika na mlipuko wa magonjwa, usambaaji na njia ya kudhibiti.
Mtaalaamu huyo amesema Mpox husambaa kwa kugusana, kufanya ngono na kupigana busu na mtu mwenye maambukizi.
Njia zingine ni kugusana na mnyama mwenye ugonjwa huo, kula mnyama mwenye maambukizi au kuipika, kugusa mashuka, nguo au vitu vyenye ncha kali vyenye maambukizi ya homa ya nyani.
“Pia mjamzito anaweza kumwambukiza mtoto ambaye hajazaliwa, ukiwa na ugonjwa huu mweleze mtu aliye karibu na wewe, kaa nyumbani hadi vidonda vyote vipone, funika majeraha yako na vaa barakoa wakati unazungumza na watu,” amesema.
Akizungumzia njia ya kudhibiti ugonjwa huo, Dk Tarimo amesema ni kupata chanjo ambayo hupaswa kutolewa ndani ya siku nne baada ya kugusana na mtu mwenye ugonjwa huo.
Amesema watu wenye hatari ya kupata ugonjwa huo ni muhimu kupata chanjo ili kuzuia maambukizi na hasa wakati wa mlipuko.
Watu walio kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo, amesema ni wanaofanya ngono ya jinsia moja, wanaofanyabishara ya ngono na wenye wapenzi wengi.
Licha ya kwamba ni salama, Serikali ya Tanzania imetoa tahadhari kwa wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa wa homa ya nyani.
Wizara ya Afya katika taarifa kwa umma iliyotolewa hivi karibuni, ilisema hadi sasa Tanzania ni salama na hakuna mgonjwa yeyote aliyepatikana na ugonjwa huo ambao dalili zake ni upele, malengelenge au vidonda kwenye mwili, hasa mikononi na miguuni, kifuani, usoni na wakati mwingine sehemu za siri.
Ilisema dalili nyingine ni homa, maumivu ya kichwa, misuli, mgongo, uchovu na kuvimba mitoki.
“Ugonjwa huu haujaingia nchini, hivyo, ni vema tukashirikiana kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa salama,” ilieleza taarifa hiyo ya wizara.
Kutokana na hilo, Serikali imewataka Watanzania kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kubusiana na mtu mwenye dalili za Mpox.
Serikali imewataka wananchi kuepuka kugusana na mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox, na kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Pia imewataka kuepuka kula au kugusa mizoga au wanyama mfano nyani au swala wa msituni, kusafisha na kutakasa vyombo vilivyotumika na mhisiwa au mgonjwa pamoja na maeneo yote yanayoguswa mara kwa mara.
Watoa huduma za afya wametakiwa kuzingatia miongozo ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi (IPC) wakati wote wanapowahudumia wagonjwa.
Akizungumza na Mwananchi Agosti 16, 2024 Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Englibert Kayombo alisema:
“Tunafanya ufuatiliaji wa karibu na tayari tumetoa tahadhari kwa watu juu ya ugonjwa huu ambao umeingia nchi za Afrika Mashariki. Tumechukua hatua ya kutoa elimu kwa wananchi kujikinga na ugonjwa huu kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Kwa maeneo ya mipakani, Kayombo alisema wameongeza ufuatiliaji wa abiria wanaoingia na kutoka ambao huchunguzwa lengo likiwa kujikinga na ugonjwa huo.
Alisema endapo mtu yeyote akibainika kuwa na ugonjwa huo mipakani, wamejipanga kutoa huduma za matibabu ili usienee nchini.
Kamati ya IHR chini ya Profesa Ogoina iliwasilisha ripoti kwa Dk Ghebreyesus ikieleza ilichambua data zilizowasilishwa na wataalamu kutoka WHO na nchi zilizoathirika, ikieleza kuna uwezekano wa Mpox kusambaa zaidi katika nchi za Afrika na hata nje ya bara hilo.
Baada ya kupokea ripoti hiyo, Dk Ghebreyesus alisema, “kujitokeza kwa aina mpya ya virusi vya Mpox, kuenea kwake haraka mashariki mwa DRC na kuripotiwa maambukizi katika nchi kadhaa jirani ni jambo la kutia wasiwasi.”
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti amesema jitihada zinaendelea kwa kushirikiana kwa karibu na jamii, serikali na timu za kitaifa zinafanya kazi kusaidia kuimarisha hatua za kudhibiti Mpox.
“Tunapanga kuongeza zaidi jitihada kupitia hatua za kimataifa zilizoratibiwa ili kusaidia nchi kumaliza milipuko hii,” amesema.
Uamuzi wa PHEIC ni wa pili katika kipindi cha miaka miwili kuhusu Mpox.
Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu mwaka 1970 nchini DRC ukiathiri zaidi nchi za Afrika ya kati na magharibi.
Julai 2022, mlipuko wa Mpox katika nchi nyingi ulitangazwa kuwa dharura ya kimataifa kutokana na kuenea kwake haraka kupitia uhusiano wa kingono katika nchi ambazo virusi hivyo havikuwa kubainika awali.
Tangazo hilo la dharura ya kimataifa lilifikia ukomo Mei 2023 baada ya kushuka kwa kasi ya maambukizi kimataifa.
Nchini DRC kwa zaidi ya muongo mmoja kumekuwa na ripoti kuhusu maambukizi ya Mpox na kila mwaka idadi ya maambukizi huongezeka.
Kwa mujibu wa WHO, idadi ya ripoti za ugonjwa mwaka jana iliongezeka kwa kiasi kikubwa, na tayari idadi ya walioripotiwa mwaka huu imezidi jumla ya mwaka jana ikiwa ni 15,600 na vifo 537.
WHO imesema kuna aina mbili za chanjo za Mpox zinazopendekezwa na ambazo zimeidhinishwa na mamlaka za udhibiti za kitaifa zilizoorodheshwa na shirika hilo pamoja na nchi binafsi kama vile Nigeria na DRC.
Wiki iliyopita, WHO ilianzisha mchakato wa orodha ya matumizi ya dharura kwa chanjo za Mpox, ambayo itaharakisha upatikanaji wa chanjo kwa nchi zenye kipato cha chini, ambazo bado hazijaziidhinisha.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.