Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza imewaburuza kortini watumishi 19 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa katika halmashauri za mkoa huo.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa, Agosti 16, 2024 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi ya taasisi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.
Bila kutaja majina yao, Ruge amesema watumishi hao wanafanya kazi katika Idara za Uhasibu na Mapato, Uvuvi, Kilimo na Mifugo katika halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na Ilemela na mashauri hayo yako katika hatua mbalimbali za usikilizwaji wake.
“Katika kipindi cha miezi mitatu mashauri mapya ya rushwa 26 yalifunguliwa mahakamani kati ya hayo, 19 yanawahusu watumishi wa umma kutoka katika idara za uhasibu na mapato, uvuvi, kilimo na mifugo katika halmashauri za Sengerema na Ilemela. Mashauri saba yaliwahusu wengine wakiwemo watendaji wa kata,” amesema Ruge.
Kwa mujibu wa Ruge watumishi hao wamefikishwa mahakamani baada ya kubainika kukusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali bila kuyawasilisha katika akaunti za akaunti za Serikali badala yake wanaingiza katika akaunti binafsi (hakutaja kiasi).
Katika hatua nyingine, Ruge amesema katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu, Takukuru imefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi 17 ya maendeleo yenye thamani ya Sh6.5 bilioni na kubaini miradi saba yenye thamani ya zaidi ya Sh2.09 bilioni ikiwa na mapungufu.
Amesema baada ya kubaini mapungufu hayo, waliitisha nyaraka zote za miradi hiyo ikiwemo nyaraka za manunuzi ya vifaa na kuainisha mapungufu hayo kisha kuwashauri wahusika kuyafanyia kazi kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Lengo la kufuatilia miradi ya maendeleo ni kuhakikisha fedha zinayotolewa na Serikali zinaakisi thamani, ubora na lengo la Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi. Lengo siyo kuwakamata watu na kuwapeleka mahakamani bali kuhakikisha fedha zimetumika ipasavyo na huduma zimetolewa,” amesema.
Wakati huo, Ruge amesema kupitia uchambuzi wa mifumo ya ukataji na uwasilishaji wa kodi ya zuio ‘withholding tax’, Takukuru imefanikiwa kurejesha Sh290 milioni zilizokuwa hatarini kutowasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo.
Amesema katika kuhakikisha vitendo vya rushwa vinatokomezwa katika ofisi za umma, miradi ya maendeleo na jamii, Takukuru imeanza mkakati wa utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na kukutana na wadau wakiwemo viongozi wa dini.
“Tumeshaanza kutekeleza mkakati wa kuzuia vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi na tayari tumeshaanza kutoa elimu kwa waandishi wa habari, tutaendelea kuwaelimisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025 haugubikwi na rushwa,” amesema.
Akizungumzia jambo hilo Waziri Kivuli wa Nishati, ACT Wazalendo na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Philbert Macheyeki amezitaka mamlaka zilizokasimiwa mamlaka ya ufuatiliaji wa miradi kutolala badala yake ziendelee kufuatilia kwa kina utekelezaji wake kwa kuwa zitabaini madudu lukuki.
“Nimewahi kusema kwamba siyo mara moja wala mara mbili, CAG amekuwa akionyesha kwenye ripoti yake jinsi fedha za umma zinavyotafunwa huko na watendaji wa umma na kushauri wachukuliwe hatua lakini hatua hazichukuliwi. Pengine sasa Takukuru inaweza kudhibiti wizi huo,” amesema Macheyeki.
Mwanasiasa huyo ameshauri wasimamizi na Mamlaka za uteuzi kutowafumbia macho watendaji wanaobainika kuleta uzembe, kusababisha upotevu wa fedha na kuigharimu Serikali badala yake wachukuliwe hatua kali za kisheria kukomesha vitendo hivyo.
Mkazi wa Mkolani jijini humo, Rehema Mwangi ameishauri Takukuru kuendelea kutoa taarifa za watuhumiwa wa ubadhirifu wa Ofisi za Umma na hatua walizochukuliwa ili kuwa fundisho kwa watumishi wengine wenye njia ya kutapanya mali za umma.