ACT–Wazalendo yahitimisha ziara ikitaja kero tano zinazotesa wananchi

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimehitimisha awamu ya kwanza ya ziara ya viongozi wakuu kwenye mikoa 22 na majimbo 125, ikiainisha mambo matano ambayo ni changamoto zinazowakabili wananchi.

Changamoto hizo zimetajwa kuwa ni hali ngumu ya maisha, huduma mbovu ya afya, migogoro ya ardhi, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na vitisho na ubabe kwa baadhi ya viongozi.

Ziara hiyo ya takribani mwezi mzima ililenga mambo makuu mawili ikiwemo kuzindua kampeni ya kusajili wanachama, lengo likiwa kufikia milioni 10 ndani ya miezi 10 na kusikiliza kero za wananchi.

Akihitimisha ziara hiyo leo Jumamosi Agosti 17,2024  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mabanda ya Papa, mjini Tanga, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita amesema kwenye migogoro ya ardhi, wamepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kuporwa ardhi na baadhi ya taasisi za Serikali au kuwapa wawekezaji.

“Tumekuta kuna shida kubwa nchi nzima ya uporaji wa ardhi, mpaka hivi sasa tunapozungumza kuna vijiji 975 vina migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na wananachi,” amesema.

Amesema pia kuna migogoro kati ya wakulima na wafugaji inayosababisha mauaji, akidai Serikali imeshindwa kuwa na sera madhubuti na mipango bora ya matumizi ya ardhi.

“Sisi sio wafugaji wakubwa, Ethiopia ndio nchi inaongoza kwa kuwa na mifugo mingi Afrika, lakini wenzetu hawana matatizo ya migogoro ya ardhi kwa kuwa wana sera nzuri,” amesema.

Kuhusu vitisho na ubabe wa viongozi kwa wananchi, amesema walikopita wamekuta vilio vya watu kutishwa na wengine akidai kutekwa na watu wasiojulikana.

Amesema kero kuhusu huduma za afya ni changamoto nyingine iliyoibuliwa na wananchi, huku  baadhi wakitoa ushuhuda wa kufiwa na ndugu zao kwa kukosa fedha.

Kuhusu hali ngumu ya maisha, amesema kumekuwepo na kupanda kwa bei za bidhaa kama vile mbolea, mafuta ya kula, petroli, dizeli, nauli za mabasi, kuongezeka kwa kodi, ushuru na tozo.

Mbali na hayo amesema wananchi wanalalamikia ukosefu wa ajira na mazingira magumu ya kujipatia kipato.

Malalamiko mengine amedai ni kuwepo utaratibu mbovu wa utoaji fedha kwa wanufaika wa Tasaf.

Amemuomba Mkurugenzi wa Tasaf kufuatilia namna fedha hizo zinavyotolewa.

Awali Katibu wa Ngome ya Wazee Taifa wa chama hicho, Janeth Fusi, amesema maisha ya wanawake yamezidi kuwa magumu na hilo linajidhihirisha katika minada ambako kumejaa vitanda na magodoro kutokana na wanawake kuchukuliwa vitu vyao vya ndani kwa kushindwa kulipa mikopo maarufu  kwa jina la ‘kausha damu.’

Related Posts