Unguja. Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) umefunga bucha nne majini hapa kwa kukiuka taratibu za biashara.
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Bidhaa za Mifugo, Dk Thamra Khamis Talib, amesema leo, Agosti 17, 2024, kuwa bucha hizo zimefungwa baada ya ukaguzi katika Mkoa wa Mjini Magharibi kubaini baadhi zinafanya biashara bila kusajiliwa.
Amesema taasisi hiyo inafanya operesheni za mara kwa mara na kuchukua hatua dhidi ya bucha zinazokiuka taratibu ili kuhakikisha bidhaa zinabaki salama kwa matumizi ya binadamu.
Ukaguzi unahusisha kusajili wa bucha, usafi, matumizi sahihi ya vifaa kama misumeno ya umeme na kuangalia afya za wahudumu wa bucha hizo, kwa lengo la kumlinda mtumiaji wa nyama.
Dk Talib amewataka wafanyabiashara kufuata miongozo ya ZFDA, ikiwa ni pamoja na kupima afya, kusajili bucha na kudumisha usafi ili kumlinda mtumiaji wa mwisho wa bidhaa.
Ameongeza kuwa, licha ya juhudi zinazofanywa, bado baadhi ya wafanyabiashara wanakiuka taratibu zilizowekwa, jambo linalohatarisha afya za wananchi.
“Kati ya bucha 15 hadi 20 tulizopitia, ni tatu hadi nne tu ndizo zinazokidhi vigezo na masharti ya ZFDA. Hali hii inatokana na uelewa mdogo wa wafanyabiashara, wengi wao wakiwa wanaangalia kipato na si afya za watumiaji,” amesema.
Ameongeza kuwa ZFDA itaendelea kuchukua hatua kwa wafanyabiashara wote wanaokiuka taratibu za taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kufunga bucha hadi pale watakapofuata taratibu hizo.
Pia, amewataka wafanyabiashara kufika ZFDA kupata elimu na miongozo ya kuendesha biashara hiyo ili kuepuka makosa.
Mmoja wa wafanyabiashara, Juma Ali Vuai wa eneo la Kibandamaiti, amekiri kubainika na makosa na kuahidi kurekebisha ili kufuata miongozo ya Serikali.
Naye Suleiman Hamad wa Jang’ombe pia amekiri kosa la kuendesha shughuli bila usajili na ameahidi kujirekebisha.
Mafunda Said Ali, mmoja wa watumiaji wa bidhaa za bucha amewashauri wafanyabiashara kuwa wazalendo na kujali afya za watumiaji badala ya masilahi binafsi, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha usafi ili kuvutia wateja.
Tuanze kuzijali afya zetu sisi wenyewe tuhakikishe tunanunua bidhaa katika maduka ambayo ni masafi na wauzaji wake ni wasafi ili kulinda afya zetu. Na hatua hii inaweza kusaidia baadhi ya wafanyabiashara kubadilika na kudumisha usafi,” amesema.
Pia, amesema jukumu la kulinda afya linaanza na mtumiaji mwenyewe, hivyo wateja nao wazingatie usafi wa muuzaji na mazingira ya bidhaa kabla ya kununua.
Ukaguzi wa ZFDA ulifanyika katika bucha za Mombasa, Jang’ombe, Amani, Magomeni na Kibandamaiti.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.