Muheza. Wazee mkoani Tanga wameiomba Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya hasa utoaji tiba kwa wenye matatizo ya macho, kwa kuwa ni miongoni mwa changamoto kubwa kwao.
Wazee hao wamesema kliniki za macho zinazofanyika kwenye jamii mara kwa mara zinaweza kusaidia wananchi kupata huduma haraka na kwa muda mfupi.
Wakizungumza kwenye ufunguzi wa Mama Samia Eye Clinic inayohusu utoaji huduma za macho wilayani Muheza kwa ufadhili wa taasisi Mo Dewji Foundation leo Agosti 17,2024, wazee hao wameeleza kuwa kliniki za macho zinazofanywa na madaktari maalum zimekuwa na manufaa kwao.
“Waweke huduma vizuri jamani, watu wengi wamefurahi kuja kukuta hali hii ya kuambiwa kuwa mnatibiwa bure, kwa kweli mimi nimefurahi sana. Unamuona daktari muda mchache na huduma zote muhimu wala hakuna kulala hili ni jambo jema,” amesema mkazi mmoja.
Naye Mariam Wandi (90) mkazi wa wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga alielezea jinsi alivyopata huduma ya macho kwa kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, ambapo awali alikuwa akihofia kwenda hospitali akiogopa gharama.
Anaeleza kuwa changamoto yake ilikuwa ni kuwa na huyo mtoto wa jicho, kutokuona vizuri na kuwasha, ila alikuwa anaogopa kwenda hospitali, kwa kuhofia gharama, kwani uwezo wake wa kifedha ni mdogo.
“Nilikuwa na mabinti zangu wawili mmoja alikuwa askari magereza na mwingine nesi ambao ndio walikuwa wananisaidia ila wamefariki dunia wote kwa nyakati tofauti, hali hiyo ikanifanya kuogopa kwenda hospitali kwani sina bima, nilipopata taarifa kuwa kuna huduma bure nikaona nijitokeze na nashukuru nimehudumiwa”,amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya ambapo mkoa huo umepokea zaidi ya Sh97.9 bilioni, kwa ajili ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati.
“Mkoa wa Tanga tumepata Sh97.9 bilioni katika sekta ya afya peke yake tumeweza kujenga zahanati 72,vituo vya afya zaidi ya 23,tumejenga hospitali mpya sita, kukarabati hospitali za wilaya tatu na maboresho mengine,” amesema.
Mratibu wa mipango ya huduma za macho kutoka taasisi hiyo ya Mo Dewji Foundation Amina Ramadhan anasema ndani ya siku tatu matarajio ni kuhudumia watu takribani 2,000.
Amesema kambi hiyo ya Muheza ni ya saba kwa mwaka huu na jumla ya wananchi 26,000 wamepatiwa huduma kwenye kambi zilizofanyika maeneo mbalimbali kila mwezi.