Licha ya vikwazo iliyowekewa Moscow na Umoja wa Ulaya, hali hii bado halijabadilika na gesi ya Urusi bado inaendelea kuwasili katika mataifa ya Ulaya, hata baada ya vikosi vya Ukraine kuonekana kuchukua udhibiti wa kituo cha kupimia gesi karibu na mji wa Urusi wa Sudzha katika harakati za Kyiv za kusonga mbele katika eneo la Kursk nchini Urusi.
Gesi asilia hutiririka kutoka maeneo ya Siberia Magharibi kupitia mabomba ambayo hupita katika mji wa Sudzha na kuvuka mpaka hadi kuwasili katika mfumo wa Ukraine. Baadaye gesi hiyo husafirishwa katika mataifa ya Umoja wa Ulaya kwa kupitia Slovakia, na kisha kutuma gesi kwa nchi za Austria, Slovakia na Hungary.
Gesi asilia hutumika kuzalisha umeme, kuendesha shughuli za viwanda na katika baadhi ya hatua husaidia kupasha joto majumbani.
Je, hali ikoje katika kituo cha kupimia cha Sudzha?
Gesi inaendelea kutiririka kama hapo awali. Na hilo halishangazi, kwani Ukraine igeliweza kusitisha mtiririko huo kwa wakati wowote. Lakini ni vigumu kupata tathmini halisi katika kituo hicho kutokana na usiri wa kijeshi na kuzuia ufikiaji wa eneo hilo kwa waangalizi au waandishi wa habari.
Soma pia: Kwanini Umoja wa Ulaya bado unaagiza gesi kutoka Urusi?
Kwa mujibu wa idara ya usambazaji wa gesi ya Ukraine, siku ya Jumanne, mita za ujazo milioni 42.4 za gesi zilitakiwa kusafirishwa kupitia kituo cha Sudzha, hii ikiwa ni idadi sawa ukilinganisha na siku 30 zilizopita.
Kwa nini gesi bado inatoka Urusi kwenda Ulaya?
Kabla ya vita, Ukraine na Urusi walisaini mkataba wa miaka mitano ambao uliitaka Urusi kutuma viwango kadhaa vya gesi kupitia kwenye mifumo ya mabomba ya Ukraine kuelekea Ulaya, iliyojengwa wakati nchi hizo mbili zilikuwa sehemu ya muungano wa Soviet. Kampuni ya Urusi ya Gazprom hujipatia fedha kutokana na mauzo ya gesi hiyo huku Ukraine ikikusanya kodi za kuwezesha usafirishaji.
Mkataba huo utaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2024. Waziri wa nishati wa Ukraine German Galushchenko, amesema Ukraine haina nia ya
kuurefusha au kuufanyia marekebisho mkataba huo. Kabla ya vita, Urusi ilikuwa ikisafirisha takriban asilimia 40 ya gesi asilia kuelekea Ulaya kupitia mifumo minne ya mabomba ya gesi, ikiwa ni pamoja na chini ya Bahari ya Baltic, kupitia Belarus na Poland, nyingine kupitia Ukraine na pia kwenye “Turk Stream” chini ya Bahari Nyeusi kupitia Uturuki hadi Bulgaria.
Urusi yasitisha usafirishaji kupitia baadhi ya mabomba
Mara tu baada ya vita kuanza, Urusi ilisitisha usambazaji wa gesi kupitia mabomba yaliyopo chini ya Bahari ya Baltic na yale ya Belarus na Poland, ikisema ni kutokana migogoro ya malipo ambapo mataifa ya Magharibi yalitaka kulipa gesi hiyo kwa kutumia sarafu ya Urusi ya rubles kutokana na vikwazo vya kuizuia Moscow kupata sarafu za kigeni kama Dola za Marekani na Euro. Bomba kwenye bahari ya Baltic liliripuliwa kufuatia kitendo cha hujuma, lakini hadi leo hii tukio hilo bado ni kitendawili.
Soma pia: Ukraine yakanusha kuhusika kulipua bomba la Nord Stream 2
Hatua hiyo ya Urusi ya kusitisha usambazi wa gesi, ilisababisha mzozo wa nishati barani Ulaya. Ujerumani ililazimika kutoa mabilioni ya euro ili kuanzisha vituo vinavyoelea baharini ili kupokea gesi iliyosindikwa na iliyoagizwa kutoka nje na iliyokuwa ikiwasili kwa meli na si kutumia mabomba. Watumiaji wa gesi barani Ulaya walikabiliwa na viwango vya juu vya bei ya nishati hiyo huku wakipunguza pia matumizi yao.
Marekani na Norway yalijaribu kuziba pengo la Urusi na kuwa wauzaji wakuu wawili wa gesi barani Ulaya. Mataifa ya Ulaya yalichukulia hatua hiyo ya Urusi kama usaliti na vitisho kwa kutumia nishati hiyo na yameelezea mipango na mikakati ya kuachana kabisa na uagizaji wa gesi ya Urusi ifikapo mwaka 2027.
(Chanzo: AP)