Mabaharia Zanzibar kuingia soko la kimataifa

Unguja. Kilio cha mabaharia wa Zanzibar kukosa sifa za kutambulika kimataifa huenda kikapata ufumbuzi baada ya kuanza kupatiwa mafunzo maalumu yatakayokidhi viwango vya kimataifa.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutia saini makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Heroes kutoka Uholanzi, ambao utashirikisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) katika uendeshaji wa mafunzo ya ubaharia.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka saba.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo Agosti 16, 2024, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Hamad Bakari Hamad, amesema mabaharia wa Zanzibar sasa watapata utaalamu na vyeti ambavyo vitawawezesha kufanya kazi katika meli za kimataifa.

“Mabaharia wenye ngazi ya maofisa ni wachache, lakini wenye ngazi ya chini ya maofisa ni wengi duniani, na kwa Zanzibar ndivyo ilivyo. Hii imekuwa changamoto katika soko la kimataifa kwani mabaharia wetu hawawezi kuingia katika soko hilo,” amesema Hamad akisisitiza kuwa wizara tatu zinashirikishwa katika kufikia hatua hiyo.

Suza, ikiwa chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo, itahusika na kufundisha taaluma, huku utoaji wa vyeti vya umahiri ukisimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Baharini (ZMA).

Wizara ya Uchumi wa Buluu itaratibu mafunzo hayo, kwa kuwa masuala ya bahari ni miongoni mwa sekta tano za uchumi wa buluu, zingine zikiwa ni utalii, mafuta na gesi, uvuvi na ulinzi wa bahari.

Hamad amebainisha kuwa darasa la kwanza la mafunzo ya viwango vya umahiri (STCW) linatarajiwa kuanza mwaka huu na litakuwa na wanafunzi 20. Walimu wa mafunzo hayo wanatarajiwa kutoka Afrika Kusini au India.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mabaharia Zanzibar, Hussein Nasor Uki, amesema hii ni fursa nzuri kwa mabaharia wa Zanzibar kupata sifa za kimataifa.

Amefafanua kuwa kampuni nyingi za meli duniani hazijaweza kuwaamini mabaharia wa Zanzibar kama mabaharia kamili kwa sababu ya kukosa vyeti vinavyotambulika kimataifa.

“Kutia saini ni jambo moja na kutekeleza ni lingine, kwa hiyo tunataka tuone matokeo yake katika kuwasaidia mabaharia wetu,” amesema Uki.

Kwa mujibu wa Uki, chama hicho kina mabaharia 500, kati ya hao wanawake ni 15 pekee.

Katibu wa Jumuiya ya Wanawake Mabaharia Zanzibar (Zawosa), Raya Juma Khalfan, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanawake wengi waliokuwa wanatamani kusoma fani hiyo lakini walishindwa kutokana na kukosa chuo visiwani humo.

 Ameeleza kuwa kuna wanawake wenye fani za unahodha na uhandisi wa meli, lakini wapo katika viwango vya chini zaidi kutokana na changamoto ya ukosefu wa chuo cha kufundishia.

Raya amesisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi wanawake wenye msingi mzuri lakini hawana mwendelezo, akiongeza kuwa changamoto nyingine ni mtazamo potofu kwamba wanawake hawawezi, jambo linalowakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha, na Utawala Suza, Dk Hashimu Hamza Chande, amesema wamepata faraja kwani wapo kwenye mchakato wa kuanzisha chuo na sasa wataongezewa utaalamu wa kufundisha.

Ameeleza kuwa Zanzibar haina walimu mahiri wa kufundisha ubaharia, lakini kupitia mkataba huo, watapata wataalamu wazuri na hatimaye mabaharia wa Zanzibar wataweza kuingia katika soko la kimataifa kwa viwango bora zaidi.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts