Mahakama yaridhia wananchi kumpinga Waziri wa Madini

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Musoma imeridhia maombi ya baadhi ya wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara, kufungua shauri kupinga Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii za mwaka 2023.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Marline Komba kutokana na shauri la maombi lililofunguliwa na wananchi hao, Godfrey Kegoye, Gotora Chichake, Paul  Bageni, Daudi Nyamhanga, na Bogomba Chichake dhidi ya Waziri wa Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri la maombi mchanganyiko namba 0000429, wananchi hao waliomba ridhaa ya Mahakama wafungue shauri la maombi ya mapitio ya kimahakama kuomba amri za kutengua uamuzi wa waziri huyo kutunga kanuni hizo, na kumuamuru kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Jaji Komba amefikia uamuzi huo baada ya kuridhika kuwa waombaji wamekidhi masharti ya kisheria kustahili kupewa ridhaa, yaani kuwapo hoja ya kujadiliwa, maombi kuwasilishwa ndani ya wakati uliobainishwa kisheria (miezi sita) na kuonyesha masilahi waliyo nayo katika suala husika.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo mawakili wao, Kasim Gila akisaidiana na Kelvin Mtatina,  walieleza na kuonyesha mahakama kuwa wateja wao wamekidhi vigezo hivyo.

“…ninaona kuwa kuna hoja ya kujadili katika maombi, hususani malalamiko kuhusu kuvuka mipaka ya kisheria, ninayaridhia,” amesema Jaji Komba baada ya kurejea hoja za pande zote na kuzifanyia uchambuzi.

Jaji Komba amewapa waombaji hao muda wa siku 30 kuanzia tarehe ya uamuzi huo Agosti 12, 2024, kufungua shauri la maombi ya mapitio.

Waombaji walichukua hatua hiyo baada ya Waziri wa Madini kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii za Mwaka 2023, GN (Tangazo la Serikali) namba 409 la mwaka 2023, Juni 23, 2023.

Kanuni hizo zimeweka mgawanyo wa fedha za CSR kutoka kwa kampuni za uchimbaji madini baina ya vijiji vinavyozunguka migodi ya madini na halmashauri za miji, wilaya, manispaa au jiji  katika maeneo ambako shughuli za madini zinafanyika.

Zinaelekeza vijiji vinavyozunguka migodi hiyo kupokea asilimia 40 ya fedha hizo na asilimia 60 kwenda kwa halmashauri za miji, wilaya au manispaa au jiji husika ambako shughuli za madini zinafanyika.

Wananchi hao wanapinga kanuni hizo wakidai zimepunguza haki yao kupokea na kutumia asilimia 100 ya fedha za CSR.

Katika kiapo chao cha pamoja kilichounga mkono maombi hayo ya ridhaa, walidai kanuni zinawaondolea umiliki kamili na kufaidika kwa asilimia 100 na fedha na raslimali zinazotolewa na mgodi wa dhahabu wa North Mara, kama sehemu ya wajibu wa kampuni hiyo kwa jamii.

Pia walidai halmashauri za wilaya, miji na manispaa ambazo zimetengewa asilimia kubwa ya fedha au rasilimali, si sehemu ya jamii wenyeji wa eneo ambamo shughuli za uchimbaji madini zinafanyika.

Vilevile walidai asilimia 40 ya fedha au rasilimali zinazotolewa kwa jamii wenyeji kupanga na kutekeleza shughuli za kimazingira, kiuchumi, kijamii na za kiutamaduni,  ni kinyume cha kusudio la Sheria ya Madini, Sura ya 123, iliyorejewa mwaka 2019.

Hivyo waliomba ridhaa ili wafungue shauri la mapitio kuomba amri ya kutenguliwa na zuio la GN namba 409 la mwa 2023, kwa madai kuwa wao kama miongoni mwa wa jamii husika hawakushirikishwa katika mchakato wake na kwamba, limevuka mipaka ya kisheria.

Awali wajibu maombi waliweka pingamizi la awali wakidai shauri hilo lilikuwa limefunguliwa nje ya muda, lakini mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote ilitupilia mbali pingamizi hilo Julai 9, 2024, ikieleza lilifunguliwa ndani ya muda uliobainishwa kwenye sheria.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo la maombi ya ridhaa, wakili wao, Gilla alibainisha masharti ambayo wanapaswa kuyatimiza wateja wake ili kupewa ridhaa hiyo, akieleza masharti hayo kuwa ni muda wa kufungua maombi, masilahi ya waombaji na kuwepo hoja ya kujadili.

Kuhusu sharti la muda, ambalo hata hivyo lilikuwa limeshaamriwa wakati wa usikilizwaji wa pingamizi la awali la wajibu maombi, wakili Gilla alidai kuwa kanuni hizo zilichapishwa Juni 23, 2023 na kwamba, waombaji walifungua ndani ya muda wa miezi sita kwa mujibu wa sheria.

Katika sharti la masilahi, alieleza waombaji ni wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara na ni wanufaika wa fedha zinazotolewa na kampuni hiyo, kama wajibu wa kampuni kwa jamii, kiuchumi, kijamii na nyinginezo.

Kuhusu hoja inayohitaji kujadiliwa, wakili Gilla alidai wameonyesha kitendo cha Waziri kutunga kanuni kuwa ni kinyume cha kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini (5), Sura ya 123.

Alidai kifungu hicho kinaeleza wanaopaswa kunufaika ni wakazi wa eneo ambalo shughuli za madini zinafanyika na kwamba kanuni hizo hasa kanuni ya 4 inakiuka kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini.

Wakili Gilla alifafanua kuwa sehemu 4(a) na (b) ya kanuni hizo zinazolalamikiwa imepanua wigo wa wanufaika wa fedha za CSR mpaka kwa manispaa, majiji na halmashauri jambo ambalo ni kinyume cha sheria mama, ambayo iliwalenga jamii wenyeji.

Alihitimisha kuwa, hapakuwa na nafuu nyingine kwani waombaji walishamwandikia barua Waziri wa Madini na wamekuwa na vikao kujadili suala hilo na mgawanyo huo wa asilimia 40 kwa 60, lakini barua hiyo haikujibiwa na vikao havikuleta matunda, hivyo wakaamua kutumia mahakama.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Kitia, alipinga maombi hayo.

Akirejea uamuzi wa kesi kadhaa zilizoamriwa na mahakama hiyo, alidai mahakama iliongeza sharti la nne kwamba ili kupewa ridhaa kufungua shauri linalokusudiwa ni lazima waombaji wawe hawana njia mbadala ya kupata nafuu wanazozilalamikia.

Wakili Turoke alidai kanuni hizo hazikiuki kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini bali hukamilisha kifungu cha 129 cha sheria hiyo kinachomtaka waziri kutunga kanuni.

Alidai kifungu cha 105 kinaelekeza kuwa fedha za  CSR sharti zielekezwe kwa maeneo ambako shughuli za madini zinafanyika na kwamba maeneo hayo husimamiwa na serikali za mitaa zikiwamo manispaa, majiji na halmashauri.

Hivyo alidai kanuni ya 4(a), (b) huakisi kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini na kusisitiza kuwa kifungu hicho cha sheria hakijakiukwa kwa kuzingatia kuwa wanufaika wanaotajwa katika kanuni hizo ni halmashauri ambamo waombaji wanaishi.

Wakili Turoke alihitimisha kwa kuiomba mahakama ione kuwa hakuna hoja ya kujadiliwa na kwamba, hawawezi kusema kuwa hawana namna mbadala kwa kuwa kilichofanywa na waziri kimeelekezwa kwenye sheria.

Related Posts