Dar es Salaam. Kim Ung-Yong ‘Genius’, anatajwa kama mmoja wa watu mashuhuri waliowahi kuvunja rekodi ya dunia kwa kuwa na akili nyingi duniani akiwa katika umri mdogo.
Haikutokea tu kama bahati. Kama wasemavyo wahenga kuwa nyota nyema huanza asubuhi, ndivyo ilivyokuwa kwa Kim Ung- Yong.
Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia alizaliwa kwenye familia ya wasomi katika mji wa Seoul nchini South Korea Machi 8, 1962 baba yake akiwa Profesa wa fizikia na mama yake akiwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Seoul.
Historia yake ya kustaajabisha ilianza alipokuwa na umri wa miezi sita tangu kuzaliwa, wakati baadhi ya watoto katika umri huo huwa katika hatua ya kutambaa kwa Ung-Young ilikuwa tofauti.
Kwa mujibu wa tovuti ya Genius Club katika umri huo Ung- Young alikuwa tayari anaweza kuzungumza lugha mama vizuri jambo ambalo liliwashangaza wengi.
Alipofika umri wa miaka minne alikuwa tayari na uwezo wa kuzungumza na kuandika lugha zaidi ya tano ikiwemo Kiingereza, Kijapani, Kijerumani, Kikorea pamoja na Kifaransa na aliendelea kujifunza lugha nyingine.
Akiwa na miaka minne alikuwa na uwezo wa kuandika vitabu vya simulizi zenye ukubwa mpaka kufikia kurasa zaidi ya 200.
Pamoja na kujua lugha mbalimbali na kuandika simulizi pamoja na mashairi akiwa katika umri mdogo Yong alikuwa ‘mkali’ wa kukokotoa maswali ya hisabati.
Umaarufu wake katika kufanya maswali magumu ya hisabati ukaongezeka sana miaka hiyo na ikamfanya kualikwa mara kwa mara kwenye vipindi vya televisheni ili kuonyesha kipawa chake cha ajabu.
Kwa mujibu wa tovuti ya ‘history of yesterday’ akiwa na umri wa miaka mitano alialikwa katika kituo cha televisheni cha Fuji huko nchini Japan kwa ajili ya kuonyesha uwezo wake katika somo la hisabati.
Alistaajabisha watu waliokuwa wakifuatilia kipindi hicho cha televisheni baada ya kuweza kufanya maswali magumu ya ngazi ya chuo kikuu na kutoa majibu sahihi huku akiwa mubashara.
Pia aliweza kuandika mashairi katika lugha mbalimbali ikiwemo Kijapani, Kikorea, Kijerumani.
Akiwa katika umri huo, alianza kusoma katika Chuo Kikuu cha Hanyang huko Korea Kusini, ambako alisomea fizikia, huku akitajwa kama mwanafunzi mdogo zaidi kusoma chuo kikuu akiwa katika umri huo na baadaye alikwenda kusoma katika chuo cha Colorado state cha nchini Marekani ambapo alipata PhD akiwa na umri wa miaka 15.
Mwaka 2007, aliajiriwa kama mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Chungbuk, na 2014 alitimiza ndoto yake ya kuwa Profesa katika Chuo Kikuu cha Shinhan akiwa na umri wa miaka 51.
Awali aliwahi kuajiriwa katika taasisi ya Marekani ihusikayo na masuala ya anga za juu (Nasa) kama mtafiti.