MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru Azam Media Group kumlipa kiasi cha Sh. 100 milioni mpishi maarufu nchini Master Chef Fred Uisso maarufu kama ‘Mzee wa Maspatasapta’ baada ya kushinda kesi dhidi yake na wenzake watatu baada ya Azam kumtangaza mpishi huyo kupitia channel yake ya Sinema Zetu katika kipindi kinachorushwa na Azam TV bila makubaliano naye. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Matangazo hayo yaliyorushwa kwa zaidi ya wiki mbili katika kipindi cha mwezi Agosti, 2023 yalionesha kuwa Mpishi maarufu huyo atahudhuria katika Tamasha la Wapi Muziki na Misosi Festival, 2023 lililoandaliwa na EX-Nihio Ltd kampuni inayomilikiwa na Paul Mashauri.
Mpishi huyo maarufu anayemiliki mgahawa wake wa vyakula vya asili uliopo Kijitonyama, alimfikisha Azam Media Group, Ex-Nihio pamoja na Paul Mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai kwamba wadaiwa hao wameupotosha umma kwa kuwahadaa kuwa atashiriki katika tamasha hilo suala ambalo si la kweli.
Katika Mahakama ya Kisutu, Master Chef Fred Uisso aliiomba Mahakama kuwataka wadaiwa kumlipa fidia ya madhara ya jumla kwa kuwa matangazo yake yaliuhadaa umma suala lililopelekea kukosa biashara katika mgahawa wake.
Mahakama baada ya kusikiliza shauri hilo kwa takribani mwaka mmoja, jana tarehe 16 Agosti 2024 imefikia maamuzi hayo chini ya Hakimu Mwandamizi Fahamu Kibona kwa kuwataka wadaiwa kumlipa fidia ya madhara ya jumla kiasi cha Sh 100 milioni pamoja na gharama za uendeshaji wa shauri hilo.
Awali tarehe 25 Agosti 2023 Mahakama ilizuia kutofanyika kwa tamasha hilo baada ya Master Chef Fred Uisso kufungua shauri la kuzuia kufanyika kwa tamasha hilo la Wapi Muziki na Misosi, 2023 Festival lililopagwa kufanyika katika viwanja vya Posta Kijitonyama.
Akizungumza Wakili Ferdinand Makore aliyemuwakilisha mdai, mara baada ya kutoka Mahakamani, alisema “Haya maamuzi ya leo yanatoa fundisho kwa watu wote wanaopenda kutumia majina ya watu kwa ajili ya umaarufu wa majina hayo, kwa kuwaamiisha umma kuwa fulani atakuwepo, suala ambalo mara nyingi huwa ni uongo na hufanya hivyo kwa lengo la kupata watu wengi.
“Mahakama imetamka wazi kuwa neno fulani atakuwepo bila kupata ridhaa yake kabla ya tangazo husika ni kosa kisheria,” aliongeza Wakili Makore.