Rais Samia ashika usukani asasi ya ulinzi, usalama SADC

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Anachukua nafasi kutoka kwa Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema aliyemaliza muda wake.

Asasi hiyo ni chombo ndani ya SADC kinacholenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama katika nyanja za siasa, ulinzi na usalama.

Miongoni mwa majukumu yake ni kukuza amani na usalama ikiwamo kuzuia migogoro katika nchi wanachama, kuhimiza demokrasia na utawala bora, na kudhibiti vitisho vya kiusalama.

Rais Samia amechaguliwa kushika nafasi Agosti 17, 2024 nchini Zimbabwe kwenye Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC.

Mkutano huo uliofanyika jijini Harare, Zimbabwe umeongozwa na kaulimbiu ‘Kukuza ubunifu ili kufungua fursa ya ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu kuelekea Sadc yenye viwanda.’

Kupitia mkutano huo, Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnagagwa amekabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo, akichukua nafasi ya Rais wa Angola, Joao Lourenco aliyemaliza muda wake.

Mnagagwa baada ya kukabidhiwa uenyekiti huo, amesema nchi za SADC zitapata maendeleo na viwanda kuimarishwa kupitia nguvu ya pamoja ya watu wake.

“Jukumu la kujenga nchi yetu na kanda yetu kwa maendeleo endelevu yamo kwetu, Zimbabwe falsafa yetu ya maendeleo ni kwamba nchi inajengwa, inatawaliwa na inaombewa na watu wake. Vivyo hivyo, kanda yetu itaendelea kupiga hatua kupitia viwanda kutoka kwa watu wake na juhudi zetu za pamoja, wale wanaotaka kutusaidia wanakaribishwa lakini lazima wafanye hivyo kwa masharti yetu, na kuheshimu vipaumbele na jamii zetu,” amesema.

Mbali na hayo, Rais Mnangagwa amesema mataifa ya Afrika yanakabiliwa na athari ya mabadiliko ya tabianchi yanayochochea athari kwa binadamu, ikiwemo usalama mdogo wa chakula hivyo ni muhimu kufanya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na kuleta mbinu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa nchi za SADC, Rais Mnangagwa amesema viongozi wa mataifa hayo wanapaswa kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ubunifu kupitia kwa watu wake, kuboresha utendaji wa viwanda na maisha ya wananchi.

“Matumizi ya teknolojia ni muhumu katika kuinua ubunifu, kuzalisha bidhaa mpya na kuziongezea thamani pamoja na madini yetu na rasilimali tulizonazo,” amesema.

Akizungumzia suala la mabadiliko ya tabianchi, Rais wa Angola, Lorenzo amesema ili kupunguza athari zinazotokana na majanga ya asili, miundombinu bora kwa nchi za ukanda wa SADC inahitajika.

“Nafahamu yapo mambo mengi tunahitaji kufanya ili kujilinda dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, mwaka jana, Kituo cha Operesheni za Kibinadamu cha SADC kilikuwa na jukumu la kuratibu maandalizi ya kukabiliana na athari zitakazotokea kutokana na majanga.

“Suala la amani na usalama bado ni kipaumbele cha SADC, tumechukua hatua zinazohitajika kuhakikisha nchi ya DRC inarejea kwenye amani, mgogoro huu bado ni changamoto na tunahitajika kuendelea kuushughulikia,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Namibia, Nangolo Mbumba amesema mkakati wa muda mrefu wa maendeleo ulioandaliwa na SADC wa 2020-2050 hauwezi kufanikiwa kama hakuna amani, usalama na utawala bora.

“Kanda yetu bado inakabiliwa na changamoto za usalama hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutokana na mzozo wa wanamgambo wa kundi la M23, haya yanaibua wasiwasi wa amani yetu ndani ya SADC kuhatarishwa, hivyo tunahitaji jitihada za pamoja na utashi wa kisiasa kurejesha amani DRC,” amesema.

Katibu Mkuu wa SADC, Elias Mahozi amesema ni muhimu kwa mataifa ya SADC kuhimiza ubunifu kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa viwanda kupitia vijana.

Amesema biashara baina ya mataifa ya Afrika ipo chini ya asilimia 23 akisema maana yake ni kuwa nchi za SADC zinafanya biashara nje zaidi kuliko ndani ya jumuiya.

“Tunapaswa kuleta nguvu zetu pamoja kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya mataifa yetu hasa kero za kikodi, tutumie soko letu kukuza uchumi wa mataifa yetu na wananchi hii itasaidia biashara ndani ya nchi zetu kukua,” amesema.

Mahozi amesema nchi za SADC kama yalivyo mataifa mengine idadi ya watu inaongezeka kwa kasi, hivyo suala la kukuza uchumi ni muhimu vijana wajengewe uwezo kwa ajili ya kusaidia kukoleza mageuzi kupitia viwanda.

Related Posts