Dar es Salaam. Balozi wa India nchini Tanzania amesema ziara aliyofanya na Rais Samia Suluhu Hassan nchini India Oktoba mwaka jana, imeongeza zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili hususani kibiashara.
Balozi Bishwadip Dey amesema hayo katika hotuba yake wakati wa hafla ya kusherehekea miaka 78 ya uhuru wa India iliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam na kuhudhuria na wanadiplomasia wa nchi tofauti waliopo nchini, viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi.
Katika hotuba hiyo, Bishwadip Dey amesema ushirikiano wa India na Tanzania umepiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni ukihuishwa kutoka uhusiano wa kawaida na kuwa wa kimkakati hatua ambayo imekuja na manufaa mengi.
“Ushirikiano wetu uliboreshwa na kuhuishwa kuwa wa kimkakati wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India Oktoba 2023. Tangu wakati huo kumekuwa na ugeni mkubwa wa Watanzania nchini India,” amesema Dey ambaye ana takribani wiki mbili tangu ashike nafasi ya kuiwakilisha nchi yake nchini.
Amesema uhusiano wa kibiashara kati ya India na Tanzania upo katika mwenendo chanya, urari wa biashara kati ya hizo mbili umefikia Dola za Marekani takribani 8 bilioni (Sh21.5 trilioni) na sasa Tanzania ni mbia namba mbili wa kibiashara wa India barani Afrika.
Balozi huyo ameeleza miradi ya maendeleo ambayo India inaisaidia Tanzania na kuongeza kuwa kutokana na vivutio vingi vya utalii na ukarimu sasa Tanzania ni chaguo la watu wengi wa India kwa ajili ya mapumziko na kujivinjari.
Aidha balozi huyo amesema miaka 78 iliyopita India ilikuwa miongoni mwa mataifa masikini na ambayo hayajaendelea, lakini sasa ni taifa la tano kwa uchumi mkubwa duniani na miongoni mwa nchi zenye ukuaji wa kasi kiuchumi.
“Tumedhamiria kuwezesha nchi na wananchi kuwa huru na kujitegemea katika nyanja zote. Tuna wigo mkubwa wa kampuni changa na bunifu duniani, tumefanya makubwa kwenye sekta ya afya na vifaa tiba lakini pia mifumo mizuri ya malipo kidijitali ambayo inatumiwa na mataifa tofauti,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema kwa niaba ya Rais na Watanzania anaipongeza India kwa kuadhimisha miaka 78 ya uhuru wa Jamhuri ya India, huku akisema nchi hiyo imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania tangu mwaka 1961.
Dk Ndumbaro naye alizungumzia namna ziara ya Rais Samia katika taifa hilo ilivyoongeza ari ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kufanya biashara kati ya mataifa hayo mawili.
“Sasa India ilitangaza kuwa Tanzania ni mshirika namba mbili wa kibiashara barani Afrika ikitoka nafasi ya tatu … India imeendelea kuwa soko kubwa la bidhaa za Tanzania na Taifa hili limekuwa miongoni mwa vyanzo vitatu vya uwekezaji wa kutoka nje,” amesema.