Waliohukumiwa kifo kwa mauaji ya mlinzi KKKT wakwaa kisiki kortini

Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa waliyohukumiwa wakazi wawili wa Mkoa wa Ruvuma.

Walituhumiwa kumuua aliyekuwa mlinzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Songea Mjini, Rashid Machupa.

Waliohukumiwa ni Twaibu Ngindo na Sadala Mchopa ambao kwa pamoja walishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea uliotolewa Septemba 28, 2022 katika kesi ya mauaji namba 23/2022, ambao uliegemea zaidi maelezo ya onyo ya watuhumiwa hao na maelezo ya ziada waliyotoa mbele ya hakimu (mlinzi wa amani), ambako walikiri kutenda kosa hilo.

Mahakama ya Rufani iliyoketi Songea, ilitupilia mbali rufaa hiyo ya jinai namba 478 ya mwaka 2022, baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote.

Majaji baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia kumbukumbu za rufaa, walieleza shtaka hilo lilithibitishwa kikamilifu na kukiri kwa warufani wenyewe ambao maelezo hayo hawakuyapinga waliposomewa mahakamani wakati wa usikilizwaji.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufani umetolewa Agosti 16, 2024 na majaji Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Omar Othman Makungu, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa Septemba 12, 2020 katika kanisa hilo walimuua mlinzi aliyekuwa ametoka kwenye Kampuni ya Ulinzi ya Ilonjezi.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa na shahidi wa kwanza ambaye alikuwa mfanyakazi mwenzake marehemu, Godfrey Mangamale aliyedai alikuwa zamu siku hiyo.

Alisema  akiwa kwenye lango kuu, saa sita usiku alienda kumuangalia mwenzake huyo katika eneo la Chekechea alikokuwa akilinda lakini hakumkuta.

Alidai baada ya kumfuatilia na kufika kwenye ukumbi wa mikutano, aliona nguo za Machupa zikiwa zimetawanyika chini, akiwa bado anashangaa, aliona watu watatu wakikimbia na baadaye, mmoja alianza kumfukuza lakini alifanikiwa kutoroka, huku akipiga kelele kuomba msaada.

Shahidi alidai aliokolewa na walinzi wengine waliokuwa wakilinda nje ya ukuta wa KKKT, mita chache kutoka kwenye ukumbi wa mikutano  walimkuta Machupa akiwa amelala chini, huku akiwa na jeraha kubwa kichwani.

Alidai kando yake kulikuwa na jiwe la umbo la pembetatu na upande mmoja ulikuwa umetapakaa damu, huku bunduki aliyokuwa nayo Machupa ikiwa upande mwingine.

Shahidi alidai alikwenda nyumba ya karibu ya mwinjilisti wa kanisa hilo, Laban Kaminyonge kumjulisha kuhusu tukio hilo.

Washtakiwa Twaibu na Sadala walikamatwa kwa kosa la uvunjaji wa nyumba sehemu nyingine mkoani Njombe na baadaye kuhusishwa na tukio hilo la mauaji. Katika maelezo yao ya onyo walikiri kumuua mlinzi huyo.

Oktoba 21, 2020 Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo alirekodi maelezo ya watuhumiwa hao nje ya mahakama na walikiri kumuua marehemu.

Katika utetezi wao, warufani walikana kutenda kosa la mauaji, pia walikana kukiri katika maelezo ya onyo na kwa mlinzi wa amani.

Twaibu alidai aliteswa na kulazimishwa kusaini karatasi bila kujua kilichoandikwa.

Sadala alidai kukamatwa kwa kosa la kugombana chini ya kifungu cha 89 (i) (b) cha Kanuni ya Adhabu lakini cha kushangaza alishtakiwa kwa mauaji.

Katika rufaa hiyo, Twaibu na Sadala waliwakilishwa na mawakili Hillary John na Elias Ndunguru, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Baraka Mgaya.

Sababu za rufaa zilikuwa ni mahakama ilikosea kisheria kuwatia hatiani na kuwahukumu warufani kwa kuzingatia maelezo yao ya onyo na kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi dhidi yao pasipo kuacha shaka.

Mawakili wa warufani waliomba mahakama kukubali rufaa hiyo kwa madai kuwa Twaibu alilazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyafahamu na Sadala maelezo yake yaliandikwa kinyume cha sheria, pia kosa hilo halikuthibitishwa kwani hukumu iliegemea maelezo ya onyo na maelezo ya ziada ambayo yana mkanganyiko.

Wakili wa mjibu rufaa alieleza maelezo ya onyo ya warufani hao yalirekodiwa ilivyostahili na kuwa katika Mahakama Kuu, Twaibu na Sadala hawakuyapinga hata pale  yalipopokelewa kama vielelezo mahakamani na kusomwa.

Kuhusu hoja ya kosa kutothibitishwa pasipo shaka, alidai maelezo ya maungamo ya warufani yalidhihirisha bila shaka kuwa walitenda kosa la mauaji kwani maelezo yao ya onyo yalikuwa ya hiari.

Majaji katika hukumu wamesema wanakubaliana na uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu kwamba katika kesi hiyo hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaowahusisha warufani na mauaji ya marehemu.

Hata hivyo, wamesema warufani walikiri kumuua mlinzi huyo katika maelezo yao ya ziada ya kimahakama,  na kuwa kama ilivyoelezwa kwa usahihi na wakili Baraka kuwa maungamo (maelezo ya onyo) ya warufani hayana shaka kwamba wao ndio waliomuua.

“Shitaka hilo lilithibitishwa kikamilifu na kukiri kwa warufani wenyewe na tunakubaliana na uwasilishaji wa wakili Baraka kwamba, malalamiko ya warufani kwamba maelezo yao ya onyo yalichukuliwa kimakosa kwa sababu walitia saini baada ya kuteswa hayana msingi,” imeeleza hukumu ya mahakama.

Wameeleza kumbukumbu za mahakama zinaonyesha hata mahakamani wakati wa usikilizwaji, warufani walisomewa yaliyokuwa yameandikwa kwenye maelezo hayo lakini hawakuyapinga na walipewa fursa ya kumhoji shahidi wa tisa aliyerekodi ila hawakuuliza.

“Kwa hiyo tunaona hata masuala yaliyotolewa na wakili wa warufani kupinga taarifa za ungamo katika hatua hii ya rufaa, hayana msingi wowote na tumeridhika kwamba mashtaka yalithibitishwa bila shaka yoyote hivyo tunatupilia mbali rufaa,” imeeleza sehemu ya hukumu ya mahakama. 

Related Posts