Wanafunzi 20 wa chuo kikuu watekwa

 

ZAIDI ya wanafunzi 20 wa Chuo Kikuu cha Nigeria wametekwa na watu wenye silaha waliovizia magari yao kaskazini mwa nchi hiyo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Msemaji wa jeshi la polisi katika eneo la Benue, Catherine Anene amesema jana Ijumaa wanafunzi hao walikuwa wakielekea kusini mwa nchi kushiriki mkutano wa wanafunzi wanaosomea udaktari ndipo walipovamiwa katika jimbo la Benue nchini humo.

Amesema shambulizi hilo lilitokea kando ya barabara ya Benue’s Otukpo, mahali palipojulikana sana kwa utekaji nyara.

Wanafunzi waliotekwa ni wa vyuo vikuu vya Maiduguri na Jos, vyote vya kaskazini mwa Nigeria na tayari wanafunzi wenzao wamelaani tukio hilo na kuzitaka mamlaka kuwalinda wanafunzi na kuhakikisha wenzao wanaachiliwa.

Haikubainika mara moja ni kundi gani lililofanya shambulizi hilo au mahali ambapo mateka walipelekwa na polisi bado ilikuwa haijasema chochote kuhusiana na juhudi za kuwaokoa.

Kiongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Maiduguri, Ijaban Bajam amesema kwenye taarifa yake kwamba wamesikitishwa na kitendo hicho na kutoa wito wa wanafunzi hao kurudi salama.

About The Author

Related Posts