Dar es Salaam. Jukwaa la Ubora na Usalama wa Chakula Tanzania, linawasisitiza Watanzania kula vyakula bora na Salama, kwani mlo kamili ni chanzo cha kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kama utapiamlo na kisukari.
Jukwaa hilo limewataka Watanzania kuwa makini kwenye ulaji wa vyakula na uandaaji wake ambapo maandalizi hayo yanaanzia shambani hadi jikoni kwa mpishi.
Wameyasema hayo leo Agosti 17, 2024 kupitia Tamasha la Ubora na Usalama wa Chakula kwenye viwanja vya Zakhem Mbagala jijini Dar es Salaam.
Dk Esther Nkuba, ambaye ni mtalaam wa lishe ya binadamu, amesema Watanzania wengi hawazingatii namna ya kuandaa chakula wakati wa upikaji.
“Kabla ya kuanza kupika chakula unatakiwa kuosha mikono yako kwa sabuni na maji safi ndipo uanze kupika, na siku hiyo kama mpishi anaumwa mafua au kikohozi, mpishi huyo afunike pua na mdomo kwa kitambaa”, amesema Ndashau.
Ametoa elimu ya namna ya kupika mboga za majani akisema zinapaswa kuoshwa ndio ikatwe na sio ikatwe ndio ioshwe lakini pia ni lazima kuweka mafuta kidogo na limau kwani ni muhimu kwenye kuboresha afya ya ubongo.
Mtaalamu mwingine Joyline Ndashau yeye amesema Watanzania wengi hawazingatii ubora wa chakula pale wanapoenda kununua bidhaa dukani au sokoni.
“Ni muhimu kuangalia vielelezo na namna ilivyosindikwa kabla ya kununua bidhaa zetu ili kufahamu kama hiyo bidhaa inafaa au haifai”, amesema Ndashau.
Faraja Mapunda ambaye ni mama nitilie wa Mbagala, amesema amefurahishwa na elimu aliyopata zaidi kuhusu kuandaa chakula bora na salama.
“Mimi ni mamantilie na ofisini sipo peke yangu hivyo elimu hii niliyopata nitaenda kuwapatia na wengine ili kuongeza thamani ya biashara zetu”, amesema.