Kibaha. Baada ya kupotea kwa siku nne akidaiwa ametekwa na vijana watatu, Ally Pweku (22), Mkazi wa Mbwate, mkoani Pwani, amekutwa amefariki dunia vichakani.
Inadaiwa kijana huyo alitekwa usiku wa Agosti 14, 2024 kwenye moja ya baa zilizopo mtaani hapo, alikokuwa akinywa pombe.
Kwa mujibu wa wakazi wa mtaa huo, wamegundua mwili wa Ally baada ya kuhisi harufu kali iliyotokea eneo ulikokuwepo mwili huo, ambalo si mbali sana na makazi ya watu.
Mmoja wa majirani hao aliyeomba hifadhi ya jina lake, leo, Jumapili Agosti 18, 2024 amesema wakati anarudi nyumbani kutoka kwenye shughuli zake, alihisi harufu kali na ndipo alipoamua kuifuatilia.
“Nikafuatilia na nilipokaribia nikaona mwili wa mtu amefariki nikashituka,” amesema.
Baada ya kubaini hilo, amesema alimfuata mwenyekiti wa serikali ya mtaa kumpa taarifa na walipokwenda pamoja walikuta mwili umeharibika.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti huyo, Abdalah Mtandi amesema tayari wameshafanya mawasiliano na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuuchukua mwili huo kwa kuwa ulishaharibika.
Waliposikia taarifa za kutekwa kwa Ally, amesema walimtafuta katika maeneo mbalimbali bila mafanikio na hadi unapatikana mwili wake, walikuwa katika harakati za kumtafuta.
“Alipopotea tulimtafuta kwa juhudi kubwa lakini hatukumpata na hatimaye leo amepatikana akiwa amefariki na tumeshawapa taarifa Polisi wamesema wanakuja” amesema.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa siku ya tukio linalodaiwa la kutekwa kwake, wanasema alifika katika baa hiyo kwa ajili ya kunywa pombe ilipofika saa nne usiku walitokea vijana watatu walimbeba kwa nguvu na kutokomea naye kusikojulikana.
Mama mzazi wa kijana huyo, Tatu Putu amesema siku ya tukio mwanawe alirudi mapema kutoka kazini na alimuaga anakwenda baa na angerejea baadaye.
Amesema hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kuzungumza na kuonana na mwanawe huyo kwani hakurejea kama alivyoahidi, jambo lililompa wasiwasi kupitiliza.
Kutokana na mazingira hayo, amesema alikwenda kwa mwenyekiti wa mtaa kutoa taarifa za kutoweka kwa kijana wake na juhudi za kumtafuta ziliendelea bila mafanikio.
Balozi wa mtaa huo, Linda Salimu amesema baada ya taarifa ya kutekwa kwake aliambatana na viongozi wengine kwenda hadi eneo la tukio, lakini hawakumkuta Ally wala waliodaiwa kumteka.
Juhudi za kumtafuta ziliendelea bila mafanikio na hatimaye wamepokea taarifa kuwa, amefariki.
Muhudumu wa zamu katika baa alikokwenda kunywa pombe kijana huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Neema amesema Ally alifika hapo saa mbili usiku akaagiza kinywaji na baadaye waliingia watu wengine.
Ameeleza baada ya kuingia watu hao watatu walikuwa katika mazungumzo na Ally na baadaye ikaonekana wanamchukua kwa nguvu na kutokomea naye.
“Hakukuwa na watu wengi lakini alipofika aliagiza pombe nikamhudumia nikaenda jikoni wakati niko huko nilisikia hali ya mvutano kama wanagombana na niliporudi niliwasikia kwa mbali wanasema ndio huyu ndio huyu na wakatokomea naye,” amesema.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema wamepata taarifa juu ya tukio hilo na watalitolea ufafanuzi kesho Jumatatu.