Arteta mataji yalimpita, pesa zikamfuata

LONDON, ENGLAND: WANASEMA hata bahati mbaya ni bahati. Kwa Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kwa kukosa taji la Ligi Kuu England misimu miwili mfululizo hasa kutokana na kuwa na kikosi bora, ni bahati mbaya, lakini kwa upande mwingine ni bahati kwake.

Arsenal ilishindwa kwa pointi mbili dhidi ya Manchester City na kuambulia nafasi ya pili huku City ikibeba taji la Ligi Kuu England msimu uliopita.

Hata hivyo, pamoja na kukosa bahati hiyo ya mataji lakini Arteta amezidi kujiongezea kipato kutokana na madili makubwa aliyoisaini na kampuni mbalimbali kubwa.

Pia kocha huyo Mhispania anatarajia kusaini mkataba mpya Arsenal jambo ambalo litamfanya aendelee kuingiza pesa. Mkataba wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.

Hadi kufikia sasa anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 25 milioni na mshahara wake kwa wiki ni Pauni 150,000 ambao hufikia Pauni 8.3 milioni kwa mwaka.

Taarifa zinaeleza ofa ya mkataba mpya aliyowekewa mezani inafikia Pauni 16 milioni kwa mwaka, zaidi ya Pauni 300,000 kwa wiki.

Mshahara huo mpya utamfanya kuingia katika orodha ya makocha wanaolipwa zaidi England akiungana na Pep Guardiola anayepata Pauni 15 milioni kwa mwaka.

Arteta pia anapata pesa kutokana na madili yake ya nje ya uwanja na kwa sasa amesaini mkataba mnono na Adidas na anaripotiwa kupata Dola 3 milioni kwa mwaka. Arteta pia anapata pesa kutokana na biashara zake za nje uwanja.

Kocha huyu pia ana kampuni zinazomiliki majengo mbalimbali Uingereza na Hispania, moja ya kampuni hizo ni Littlewoods Investment LLP aliyoinunua mwaka 2013.

Littlewoods Investments LLP inamiliki majengo ambayo ni makazi ya watu na ofisi.

Mara kadhaa ameonekana akiendesha magari ya kifahari kama cadillac escalade lenye thamani ya Dola 101,595,  Bentley Continental G inayofikia Dola 250,000 pia anamiliki Bentley SUV na zote zinakadiriwa kufikia Dola 400,000.

Anamiliki mjengo huko Kaskazini mwa Jiji la London. Ndani ya nyumba yake kuna kiwanja kidogo cha mpira ambacho huwa anakitumia kufanyia mazoezi anapokuwa mapumziko wakati ligi imesimama. Mjengo huo unakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 2 milioni.

Yeye na mkewe, Lorena Bernal wamekuwa sehemu ya taasisi ya Global Gift Foundation ambayo husaidia wanawake na watoto wenye matatizo mbalimbali.

Mwaka 2017 alikuwa mmoja ya wadau waliotoa misaada kusaidia waathirika wa kimbunga cha Maria na binafsi aliliripotiwa kutoa zaidi ya Pauni 50,000.

Arteta yupo kwenye ndoa na muigizaji maarufu Hispania, Lorena Bernal tangu mwaka 2010 na wamepata watoto Gabriel Arteta Bernal, Oliver Arteta Bernal na Daniel Arteta Bernal.

Katika maisha ya bata, sio mtu wa kujitanua sana, ingawa anakunywa pombe, lakini ni mara chache sana kuonekana akifanya hivyo, muda mwingi hupenda kukaa na familia yake ligi inapokuwa imesimama.

Related Posts