Azam FC, JKU kanyaga twende kimataifa

AZAM FC kutoka Bara na JKU ya Zanzibar zitakuwa na jukumu zito leo kuiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali kwenye viwanja mbalimbali.

Azam iliyomaliza ya pili katika Ligi Kuu Bara itakuwa katika Uwanja wa Azam Complex kucheza na APR ya Rwanda kuanzia saa 12:00 jioni, huku JKU ikiikaribisha Pyramids ya Misri dimba la 30 June Stadium, saa 2:00 usiku.

Mechi ya JKU itaenda sambamba na Uhamiaji ya Zanzibar ambao watakuwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Tripoli, Libya kuvaana na Al Ahli Tripoli katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika – maafande hao wakiwa wenyeji wa mchezo.

AZAM FC VS APR
Azam imerejea kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo kurejea kwao ni mara ya pili kufuatia kufanya hivyo mwaka 2015.

Mwaka huo timu hiyo ilishiriki baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2013-2014 bila kupoteza mchezo ambapo katika michezo 26 ilishinda 18 na sare nane chini ya Kocha Mcameroon, Joseph Omog.

APR ambao ni mabingwa mara 22 wa Ligi Kuu Rwanda inakutana na Azam FC ambayo malengo yake makubwa ni kutinga hatua ya makundi msimu huu, huku ikihitaji kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kabla ya mechi ya marudiano Agosti 24.

Timu hiyo imekuwa na michezo mingi ya kujipima ubavu ambapo ilishiriki Kombe la Kagame mwaka huu jijini Dar es Salaam na kupoteza fainali kwa penalti 10-9 dhidi ya Red Arrows ya Zambia baada ya sare ya kufungana bao 1-1.

Mbali na kutumia mashindano hayo, APR pia ilicheza na Simba katika tamasha la ‘Simba Day, lililofanyika Agosti 3 jijini Dar es Salaam na kuchapwa mabao 2-0, jambo ambalo linaonyesha mchezo na Azam utakuwa ni mgumu.

JKU VS PYRAMIDS
Mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), JKU itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na, Pyramids kwenye Uwanja wa 30 June, ambapo wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano hiyo wameomba michezo yao yote miwili kuchezea ugenini huko Misri.

Wakati timu nyingi zikitumia faida ya kucheza nyumbani, ila kwa JKU imekuwa tofauti baada ya hapo awali kocha wa timu hiyo, Haji Salum kunukuliwa akisema sababu kubwa ya kuchezea michezo yote miwili ugenini ni kutokana na kulipiwa gharama zote.

Haji alisema, timu hiyo imepata udhamini wa kulipiwa gharama za safari ya Misri, kambi, utalii, uwanja wa mazoezi, mafunzo kwa makocha na kuiingiza shule ya soka ya jeshi hilo kwenye programu za Klabu ya Pyramids.

Licha ya faida kubwa ambayo timu hiyo itaipata kutokana na kitendo cha kulipiwa gharama zote hizo, ila ni wazi itakuwa na kazi kubwa ya kufanya kupata matokeo chanya, yatakayoifanya kusonga mbele kutokana na kukosa faida ya kucheza nyumbani.

Mshindi wa jumla wa JKU na Pyramids atacheza na mshindi kati ya Azam FC na APR kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi jambo ambalo linaonyesha wazi michezo hii itakuwa migumu, kwani kila timu imedhamiria kufanya vizuri kutokana na usajili uliofanyika.

UHAMIAJI NA WALIBYA
Mechi hii ya Kombe la Shirikisho itapigwa kuanzia saa 2:00 usiku tofauti na awali ilivyoonekana ingepigwa saa 9:30 alasiri, ikizikutanisha wawakilishi wa Zanzibar, Uhamiaji itakayopepetana na Al Ahli Tripoli ya Libya kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Tripoli, jijini Tripoli wakiwa wenyeji.

Uhamiaji imepata nafasi hiyo ya kucheza michuano huyo baada ya Chipukizi ya Pemba iliyokuwa imekata tiketi kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (ZFF) kuomba kutoshiriki kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, na Walibya kuwaomba maafande hao wakicheze mechi zao zote Tripoli kama ilivyo kwa JKU.

Hii ni mara ya kwanza kwa Uhamiaji kuiwakilisha Zanzibar katika michuano ya kimataifa, lakini ikiwa na mtihani mbele ya wababe hao wa Libya ambao watarudiana nao kwenye uwanja huo wiki ijayo kusaka mshindi wa kucheza na Simba katika raundi ya pili.

KAULI ZA MAKOCHA
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo alisema anatarajia mchezo mgumu kutokana na jinsi alivyowaona wapinzani wao huku akiweka wazi, shauku kubwa kwake ni kuhakikisha anapata matokeo mazuri nyumbani ili kurahisha mechi ya marudiano Rwanda.

“Utakuwa ni mchezo mzuri kwa sababu APR ni timu yenye wachezaji wazuri na wamekuwa na michezo mingi ya kujipima ubavu, tutapambana kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri nyumbani kwani ugenini tutakuwa na kazi ya ziada,” alisema.

Kocha Mkuu wa APR, Mserbia Darko Novic alisema katika michuano hiyo hakuna timu dhaifu hivyo njia nzuri ni jinsi gani utajipanga kimbinu, huku akimwaga sifa kwa nyota wa Azam kutokana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja waliokuwa nao.

Related Posts