Azam hesabu kali uwanja wa nyumbani leo

Dar es Salaam. Mchezo dhidi ya APR nyumbani leo kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 12:00 jioni ni kipimo tosha cha utayari wa Azam FC katika harakati za kupigania ndoto iliyodumu kwa miaka 11.

Tangu 2013 iliposhiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya klabu Afrika ambapo ilicheza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika hadi leo hii, Azam FC haijafanikiwa kuingia hatua ya makundi ya mashindano hayo na ndio limekuwa lengo lake kuu kila inaposhiriki.

Safari hii Azam FC imetamba kuwa imejipanga kutimiza lengo hilo inaposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika lakini ili hilo litimie, inapaswa kuutumia vizuri mchezo wa leo nyumbani ili ipate matokeo mazuri ambayo hayatowapa kazi ngumu watakaporudiana na wapinzani wao hao huko Rwanda mwishoni mwa wiki ijayo.

Na hilo litawezekana ikiwa Azam FC itatumia vyema faida ya kucheza nyumbani lakini pia iwapo benchi lake la ufundi litafanyia kazi udhaifu ambao timu hiyo imeonyesha katika siku za hivi karibuni ili iweze kuitoa APR.

Udhaifu wa safu ya ulinzi ya Azam FC ambao umeonekana katika mashindano ya ngao ya jamii unampa kibarua kigumu kocha wake Youssouf Dabo kuufanyia kazi kwa haraka ili usije kuigharimu timu hiyo dhidi ya APR leo.

Walinzi wa kati wa Azam FC, Yeison Fuentes, Yannick Bangala na Yoro Diaby wameonekana kutokuwa na mawasiliano mazuri lakini pia wana udhaifu wa kuchelewa kufika katika maeneo sahihi pindi timu yao inaposhambuliwa jambo ambalo limeifanya kuruhusu mabao sita katika mechi mbili tu za mashindano ya Ngao ya Jamii yaliyomalizika siku chache zilizopita ikiwa ni wastani wa mabao matatu kwa mchezo.

Lakini udhaifu huo wa safu ya ulinzi ya Azam FC haujaanzia tu kwenye Ngao ya Jamii bali hata mechi za maandalizi ya msimu ambapo ilikuwa imecheza mechi tano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano ikiwa ni wastani wa bao moja kwa kila mchezo.

Mechi hizo za Ngao pia zimeonyesha udhaifu wa Azam kucheza na mfumo wa kupanga mabeki watatu wa kati na hivyo inalazimika kurudi katika ile ya kutumia mabeki wawili wa kati.

“Hadi kufikia siku chache zilizopita tulikuwa tumejiandaa vyema kwa mchezo huu na nimekuwa nikiwaambia wachezaji wangu umuhimu wa hii mechi. Kwa sasa tunastahili kuwaonyesha watu kuwa hatubahatisha kuwepo hapa. Tutaingia uwanjani tukiwa tayari kupambana kusaka matokeo mazuri.

Kocha wa Azam FC, Youssouf Dabo alisema kuwa wamejipanga vyema kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi ya leo.

“Tunapaswa kujiamini sisi wenyewe. Tunawahitaji sana mashabiki wetu. Mashindano haya ni kwa ajili yao na ndio maana natamani wawepo ili tufurahie pamoja,” alisema Dabo.

Ukiondoa mechi hiyo ya Azam, kutakuwa na mechi nyingine mbili za wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya klabu Afrika ambazo ni JKU itakayocheza na Pyramids huko Misri kwenye Ligi ya Mabingwa na Uhamiaji ikiwa na kibarua dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya katika Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa huko Benghazi, Libya.

Related Posts