WAKATI Ceasiaa Queens ikitema na kuingiza nyota wapya 10 wakiwamo watano wa kimataifa, kocha mkuu wa timu hiyo, Noah Kanyanga amethibitisha kugomea ofa aliyoletewa na Yanga Princess akidai haikumshawishi.
Walioongezwa ni straika Tantine Mushiya (DR Congo), mabeki Lukiya Namubiru, Tukamuhebwa Recho na Dorcus Nabuufu na winga Halima Nanteze wote kutoka Uganda.
Wengine walioongezwa ni wazawa Zuhura Wazuri (Fountain Gate Princess), Zainab Pazzi, Mwantumu Ramadhan na Rahma Hassan (Baobab Queens) na Fatuma Zaid kutoka Mashujaa Queens.
Kanyanga alikuwa katika kiwango bora akiiongoza timu hiyo ya mkoani Iringa kumaliza katika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Wanawake, huku akiingia katika orodha ya makocha bora wa msimu uliopita.
Kocha huyo ambaye amehudumu kikosini humo kwa zaidi ya misimu mitatu sasa, Yanga Princess walimpandia kuhitaji huduma yake, ambapo dili hilo limekwama rasmi.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema baada ya mazungumzo na vigogo hao wa Jangwani, hawakufikia muafaka baada ya dau waliloweka mezani kutomshawishi kutimkia huko.
Alisema kwa sasa tayari ameanza maandalizi ya msimu ujao na kikosi chake, ambapo katika usajili wa dirisha kubwa lililofungwa juzi, Agosti 15, amefyeka wachezaji 10 na kuingiza wapya idadi hiyo.
“Nitaendelea kuwa kocha mkuu Ceasiaa Queens, mpango wangu wa kuondoka umekwama kwa kuwa dau halikushawishi, tayari nimeanza maandalizi na timu kwa ajili ya msimu ujao,” alisema.
Alisema kwenye usajili wao, wameongeza nyota watano wa kimataifa na sita wazawa, ambapo msimu ujao wanahitaji kuwania ubingwa kutokana na uwezo wa wachezaji.