Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemjibu Makamu Mwenyekiti wake bara, Tundu Lissu juu ya msisitizo wake wa kutaka tuhuma zinazoibuliwa na aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa zijibiwe.
Katika majibu yake juu ya hoja ya Lissu, chama hicho kimetoa sababu tatu zinazoakisi ukimya wa Chadema dhidi ya hoja za Mchungaji Msigwa, ikiwemo mfululizo wa hati safi kilichozipata baada ya Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mara kadhaa Lissu amesisitiza tuhuma zinazoibuliwa na mwanasiasa huyo zijibiwe, akitaka mamlaka zinazohusika ikiwemo ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho kwa kuwa ndiye mtunza nyaraka imjibu.
“Kwa kuzingatia tuhuma zenyewe, zinatakiwa zijibiwe. Kama mali zisizohamishika majengo na chochote kitakuwa na nyaraka, lakini kama mali zinazohamishika kama fedha hizo vile vile zina nyaraka,” aliwahi kusema Lissu.
Hoja hiyo aliirudia usiku wa jana Jumamosi, Agosti 17, 2024 alipokuwa katika mahojiano na kituo luninga cha Star TV akisisitiza Mchungaji Msigwa anapaswa ajibiwe na mamlaka stahiki za chama hicho.
Tuhuma zilizowahi kuibuliwa na Mchungaji Msigwa dhidi ya Chadema tangu alipotimkia CCM Juni 30, 2024 ni kile alichokiita ufisadi anaodai upo ndani ya chama hicho.
Moja ya matendo aliyoyarejea kama ya kifisadi ni fedha zaidi ya Sh2 bilioni walizochangishwa na waliokuwa wabunge wa chama hicho mwaka 2015, ambazo amedai hadi sasa haijulikani zilipokwenda.
Pia alisema ni kuwekwa hadharani kiasi na matumizi ya fedha zilizochangwa wakati wa Operesheni ya Join the Chain iliyoendeshwa na chama hicho.
Kwa sababu fedha hizo zilikusanywa kwa njia ya mitandao na benki, amesema bila shaka nyaraka zipo ni sahihi watu kuhoji zilivyotumika na sahihi kuambiwa ukweli.
Leo Jumapili, majibu ya Chadema yametolewa na Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje ya chama hicho, John Mrema alipozungumza na Mwananchi Digital.
Amesema kwa miaka mitano mfululizo chama hicho kimekuwa kikipata hati safi baada ya ukaguzi wa CAG na Mchungaji Msigwa anafahamu hilo.
“Kwa kuwa alikuwa mjumbe wa vikao vya Kamati Kuu ambavyo taarifa za fedha huwasilishwa analijua,” amesema.
Kuhusu kujibiwa kwa nyaraka, Mrema amesema haiwezekani hilo lifanyike kwa tuhuma zilizotolewa bila ushahidi, anapaswa aweke hadharani uthibitisho wa tuhuma anazoziibua.
“Haiwezekani mtu akaenda kusema uongo huko hadharani, hana ushahidi kisha chama ndio kimsaidie ushahidi! Aweke ushahidi hadharani kwani tunajua anafanya porojo za kisiasa,” amesema.
Hata hivyo, amesema mali zote zinazohamishika na zisizohamishika za chama hicho zipo salama chini ya Bodi ya Wadhamini, ambayo ndio msimamizi mkuu wa mali hizo, akidokeza rejesta ya mali hukaguliwa na CAG kila mwaka.