Dk Mwinyi: Tamasha la Kizimkazi litumike kubainisha fursa za uwekezaji 

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amewataka vingozi wa mikoa na wilaya kulitumia tamasha la Kizimkazi, kuandaa mipango madhubuti ya kubainisha fursa za uwekezaji kisiwani humo ili kuongeza vivutio vya utalii.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo Agosti 18, 2024 wakati akifungua tamasha hilo la mwaka 2024 eneo la Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.

“Niwatake wakuu wa mikoa na wilaya kutumia tamasha hili kuzibainisha na kuzitangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika kisiwa hiki hususani katika sekta ya utalii jambo ambalo litaongeza watalii kuja nchini,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema uwapo wa tamasha hilo na matamasha mengine likiwemo la mwakakogwa ni fursa muhimu katika mkoa huo.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wadau wengi hususani sekta binafsi kufungua fursa za uwekezaji, akieleza jinsi sekta binafsi ilivyo na umuhimu katika uchumi wa taifa.

Ametumia fursa hiyo kuzipongeza sekta za kibenki ambazo zimekuwa na mkazo katika kudhamini tamasha hilo hivyo kuendelea kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia mikusanyiko hiyo.

Akijibu baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na Katibu wa tamasha hilo wakati akisoma risala, Hindi Juma Ramadhan, Dk Mwinyi amesema mipango ya Serikali ni kuhakikisha inaondoa changamoto zinazowakabili wananchi hao.

 Kuhusu umeme mdogo katika  mkoa huo, Dk Mwinyi amesema tatizo hilo litakwisha muda mfupi ujao, kwani kinajengwa kituo kikubwa cha kupooza umeme katika mkoa huo

Kwa upande wa changamoto ya maji, amesema kuna miradi ikubwa inatekelezwa na kwamba baada ya kukamilika kituo cha umeme pia maji yataanza kupatikana kwa wingi huku akisema tayari ameagiza migogoro ya ardhi ishughulikiwe. 

“Kuhusu uhaba wa wataalamu wa afya nalo tunalitambua lakini Serikali inalifanyia kazi, niseme kwamba changamoto zote zilizotajwa hapa zinashghulikiwa kwa ukamilifu wake,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ambayo ndio wadhamini wakuu, Arafat Haji amesema benki hiyo imefikia rasilimali za Sh2.2 trilioni huku ikizidi kukua kwa kasi na kujitanua kwa kuchangia katika huduma za kijamii.

Awali Mwenyekiti wa tamasha hilo Mahfoudh Said Omar amesema tamasha hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwani kuna shughuli mbalimbali za kiutamaduni, ufunguzi miradi ya maendeleo zimefanyika.

Mbali na miradi, pia zaidi ya vijana 500 watapata mafunzo katika sekta za kilimo, ufugaji utalii na ufundi.

Tamasha hilo lilianza mwaka 2015 na ilikuwa ni sherehe ya kumuaga Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais John Magufuli.

Baada ya kuteuliwa Samia alikutana na wananchi wa Kizimkazi na kufanya sherehe ya kumuaga mwaka 2016 iliyojulikana kwa jina la  Samia Day na ilipofika nwaka 2017 jina likabadilishwa na kuwa Kizimkazi day.

Related Posts