Fadlu aanza kwa kishindo, Simba ikikaa kileleni

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ameanza kwa kishindo Ligi Kuu Bara baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Tabora United katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam, Complex, jijini Dar es Salaam na kukwea hadi kileleni mwa msimamo ikiing’goa Singida Black Stars.

Fadlu ni mara ya kwanza kufundisha timu nchini kama ilivyo kwa kocha wa Tabora Unitd, Francis Kamanzi ambaye alishindwa kuwatumia baadhi ya nyota wa kigeni waliosajiliwa na timu hiyo kutokana na kilichoelezwa kuwa ni ‘zengwe’ lililofanywa dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo huo.

Huo ulikuwa ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Simba dhidi ya Tabora tangu timu hiyo ya Tabora ilipopanda daraja msimu uliopita, kwani katika mechi mbili zilizopita za ligi hiyo ilipasuliwa nje ndani na Mnyama, ikianza kwa kulala 4-0 kisha kufungwa tena 2-0 kabla ya leo tena kupewa dozi nyingine na kuifanya iende mkiani mwa msimamo ikiipokea KenGold iliyofungwa mabao 3-1 mchana wa leo na Singida Black Stars.

Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 14 lililofungwa kwa kichwa na beki wa kati Che Malone, akipokea mpira wa kona uliyochongwa na Jean Charles Ahoua, huku ikionekana safu yake ya ushambuliaji kukosa utulivu.

Kuna wakati mawinga na viungo wa kati walionekana kutengeneza mashambulizi ambayo hayakuwa yanazaa matunda.

Dakika ya  37 Edwin Balua akiwa amebakia na kipa wa Tabora United, Haroun Mandanda akampiga chenga wakati anaachia shuti likagonga ukuta, jambo lililoibua kelele za lawama kutoka kwa mashabiki, ambao walikuwa jukwaani, wakimtaka acheze mpira aachane na mbwembwe.

Wakati Balua akipokea  pasi kutoka kwa Awesu Awesu, aliwatoka mabeki wa Tabora United, hivyo kipa akawa ametoka kuuwahi mpira, jambo lililofanya winga huyo kupiga chenga ambapo hakuwa na umaliziaji mzuri.

Awesu aliingia dakika ya 35 kuchukua nafasi ya Joshua Mutale ambaye alionekana kuugulia maumivu ya paja, hivyo akatolea nje, ingawa ni kama kasi ilipungua kwa upande wa Simba.

Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza Simba ilionekana kuanzisha vizuri mashambulizi yake kuanzia nyuma lakini ilionekana kutokuwepo kwa  muunganiko mzuri na eneo la mwisho la ushambuliaji.

Pasi nyingi ambazo zilikuwa zikipigwa katika eneo hilo, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Joshua Mutala walishindwa kuwa na maamuzi sahihi kiasi cha mabeki wa Tabora kuwadhibiti.

Simba walionekana kutumia zaidi maeneo ya pembeni huku kati ikionekana kuwa na ugumu kutokana na uwepo wa Pemba Kevin na Andy Bikoko waliokuwa wakiunda pacha ya ukuta wa chama hilo.

Angalau alipoingia Awesu, uwezo wa kupiga pasi katikati na kuwafungua Tabora katika eneo la kati kulionekana kuna kitu kimeongezeka huku Ahoua ambaye alikuwa akicheza nyuma ya Mukwala akihamia pembeni hata hivyo hakuonekana kuwa na madhara.

Zaidi Ahoua alikuwa akiibia ndani  na kuongeza idadi ya viungo ambao walikuwa ni Debora Fernandes na Mzamiru Yassin na kumwachia Mohammed Hussein jukumu la kuongeza nguvu ya mashambulizi kushoto.

Kuingia kwa Valentino Mashaka na Kibu Denis kipindi cha pili ni kama kiliongeza nguvu safu ya mashambulizi ya Simba, waliokuwa wamepisha ni  Mukwala na Ahoua ambao walionekana kukosa utulivu katika kipindi cha kwanza.

DAKIKA ya 68  Simba, ilipata bao la pili lililofungwa kwa kichwa na  Mashaka ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Mukwala,baada ya kupokea krosi ya Tshabalala.

DAKIKA 90 Awesu aliifungia Simba bao la tatu, ambapo ilipigwa klosi na Kibu beki wa Tabora akaokoa mpira ukakutana na Awesu.

Msimu uliopita Tabora United ilipigwa ndani, nje ya Simba jumla ya mabao sita.

Wafungaji wa mabao Pa Omar Jobe, Sadio Kanoute, Che Malone Fondoh na Fredy Koublan, mechi ilipigwa Februari 6, 2024  (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Wafungaji wa mabao ya Simba yametoka kwa Sadio Kanoute dakika ya 19 na Edwin Balua dakika ya 77, Mei 6, 2024 ( Azam Complex, Chamazi).

Kocha wa Simba, Davids Fadlu, alifanya mabadiliko mengine alimtoa Kapombe/Kijili,Mzamiru/Okejepha ni kama alilenga kuongeza kasi ya ushambuliaji.

SIMBA: Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdularazack Hamza, Che Malone,Mzamiru Yassin, Edwin Balua, Debora Fernandes,Steven Mukwala,Jean Charles Ahoua na Joshua Mutale.

TABORA: Haroun Mandanda, Shafih Maulid, Salum Chuku, Pemba Kevin, Andy Bikoko, Muganga Nelson, Daniel William, Ally Yusuph, Ismar Mhesa, Yusuph Jamal na Kiberege January.

Related Posts