Hati za kimila mwarobaini migogoro ya ardhi Kigoma

Kigoma. Hati miliki za kimila 500 zimetolewa kwa wananchi wa vijiji vya Kigalye na Mwamgongo, vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, hatua  iliyotajwa itapunguza migogoro ya ardhi hasa ya ngazi za familia.

Wakizungumza leo Jumapili Agosti 18, 2024 katika Kijiji cha Mwamgongo baada ya kupokea hati hizo zilizotolewa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Jane Goodall kupitia mradi wake wa “Tumaini kupitia vitendo”, wananchi wamesema wao kumiliki hati hizo ni fursa kwa sababu watatumia katika maeneo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamgongo, Hamimu Masoud amesema kumekuwa na migogoro ya ardhi katika eneo lake iliyokuwa ikihusisha mashamba, mipaka ya viwanja, mashamba na makazi.

Amesema hali hiyo ilikuwa ikisababisha shida kwa wananchi wake kutatua migogoro ya mara kwa mara kwa sababu walikuwa hawajapimiwa maeneo yao na kupata hati miliki.

“Pamoja na watu wengi wamepata hati kwenye kijiji changu, lakini niwaombe wasichoke kutoa hati hizo kwa wananchi waliokosa,  kwani ukiwa na hati ni moja ya fursa kwa familia au mtu mmoja mmoja,” amesema Masoud.

Mkazi wa Mwamgongo, Daudi Kisimbi amesema yeye na mke wake wamepokea hati hiyo ambayo itawasaidia kwanza kuwa na uhalali wa umiliki wa eneo na hata wakihitaji kukopa fedha kwenye taasisi za kibenki itakuwa rahisi.

Kwa upande wake, Mariam Swedi amesema, “Mimi ni mjane, hati hii niliyopata inaama kubwa kwangu kwa sababu hata nikifa, watoto wangu hawatapokonywa maeneo yao na nyumba.”

Naibu Mkurugenzi, Mradi wa ‘Tumaini kupitia Vitendo’, Kasukula Nyamaka alisema mradi huo unatekelezwa ndani ya vijiji 104 katika halmashauri nne za mikoa ya Kigoma na Katavi.

Amesema lengo la taasis hiyo kufadhili upimaji wa vipande vya ardhi na utoaji wa hati miliki za kimila, ni kuongeza ushirikishwaji wa wanawake na vijana kwenye suala la umiliki na usimamizi wa rasilimali ardhi  pamoja na kuongeza chachu ya uhifadhi wa maliasili nyingine kama misitu na wanyamapori, hususani sokwemtu katika vijiji vyao.

Kwa upande wake, Kamishna Ardhi Msaidizi wa Uwekezaji na Mapato kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, Merichiory Msafiri amesema kila mwananchi aone umuhimu wa kuwa na hati yake kwenye maeneo yao, kwani mbali na kuwa inapunguza migogoro, pia itasaidia kupata fursa za kimaendeleo.

Related Posts