Dodoma. “Jiandikishe piga kura Novemba 27, 2024.” Ni kauli muhimu kwa kila Mtanzania mwenye sifa ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaowaweka madarakani viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji.
Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo zilizotangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, kama hamna mgombea mwenye sifa, uchaguzi utatangazwa upya, pia mgombea uenyekiti anaweza kujitoa.
Pia, kanuni hizo zimetaja watu ambao hawana sifa za kuteuliwa kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo, ikiwamo wanaoweza kuwa wajumbe wa kamati ya rufani.
Kanuni zinaelekeza kwenye uchaguzi huo kutakuwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi na msimamizi wa kituo atakayeteuliwa kusimamia uchaguzi.
Hata hivyo, kanuni zimewataja ambao kwa nyadhifa zao hawatokuwa na sifa za kuteuliwa kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.
Watu ambao kanuni zimewaondoa kuteuliwa kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ni kiongozi wa chama cha siasa, hakimu au jaji, kiongozi wa dini, askari au ofisa yeyote wa chombo cha ulinzi na usalama.
Wengine wasiofaa kuteuliwa kwa mujibu wa kanuni ni katibu tawala wa wilaya, katibu tawala wa mkoa, mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa.
Kanuni zinaelekeza mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mtaa anaweza kujitoa katika nafasi hiyo kwa kujaza fomu na kuiwasilisha yeye mwenyewe kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi ndani ya siku nne baada ya tarehe ya uteuzi.
Pia, kanuni zinaelekeza endapo, baada ya uteuzi kufanyika, mgombea aliyeteuliwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa mtaa atajitoa, msimamizi msaidizi wa uchaguzi atatengua uteuzi wa mgombea huyo na wagombea waliobaki wataendelea na hatua ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa kanuni, endapo baada ya uteuzi kufanyika, mgombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya mtaa atajitoa, msimamizi msaidizi wa uchaguzi atatengua uteuzi wa mgombea huyo na wagombea waliobaki wataendelea na hatua ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa kanuni endapo, baada ya uteuzi kufanyika, mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mtaa atafariki, msimamizi msaidizi wa uchaguzi ataahirisha uchaguzi wa nafasi hiyo na chama cha siasa kilichotoa mgombea aliyefariki dunia kinaweza kuwasilisha jina la mwombaji mwingine ndani ya siku 40 tangu kuahirishwa kwa uchaguzi ili hatua za uteuzi wa mwombaji huyo zifanyike.
Pia, endapo, baada ya uteuzi kufanyika, mgombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya mtaa atafariki dunia, msimamizi msaidizi wa uchaguzi ataahirisha uchaguzi wa nafasi hiyo na chama cha siasa kilichotoa mgombea aliyefariki dunia kinaweza kuwasilisha jina la mwombaji mwingine ndani ya siku 40 tangu kuahirishwa kwa uchaguzi ili hatua ya uteuzi wa mwombaji huyo zifanyike.
Kuhusu ukomo madarakani, kanuni zinaelekeza mwenyeviti wa mtaa na mjumbe wa kamati ya mtaa watakoma kushika nafasi hizo siku saba kabla ya siku ya kuchukua fomu za kugombea uongozi chini ya kanuni hizi.
Kanuni zinaelekeza kuwa endapo baada ya saa 10 kamili jioni ya siku ya uteuzi kutakuwa hakuna mwombaji aliyejitokeza au kama waombaji wote waliojitokeza hawana sifa zinazostahili, msimamizi msaidizi wa uchaguzi atavitaarifu vyama vya siasa na wakazi wa mtaa kuhusu kukosekana kwa waombaji au kutokuwepo kwa waombaji wenye sifa.
Pia, kwa kuzingatia masharti ya kanuni ndogo ya (3), msimamizi msaidizi wa uchaguzi atavitaarifu vyama vya siasa na wakazi wa mtaa husika kuhusu kurudiwa kwa mchakato wa uchaguzi baada ya siku 40 kuanzia tarehe ya uteuzi.
Kanuni zinaelekeza kuwa endapo siku ya uteuzi kutakuwa na mwombaji mmoja aliyejitokeza katika nafasi ya uenyekiti wa mtaa, msimamizi msaidizi wa uchaguzi atamteua mwombaji huyo kuwa mgombea pekee kwa nafasi aliyoomba.
Pia, endapo idadi ya waombaji wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya mtaa, waliojitokeza na kuteuliwa itakuwa sawa na idadi ya wajumbe wanaohitajika kwa mujibu wa kanuni ya sita, msimamizi msaidizi wa uchaguzi atawateua waombaji hao kuwa wagombea pekee kwa nafasi waliyoomba.
Kwa mujibu wa kanuni endapo idadi ya waombaji wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya mtaa waliojitokeza na
kuteuliwa itakuwa chini ya idadi ya wajumbe wanaohitajika kwa mujibu wa kanuni ya sita, msimamizi msaidizi wa uchaguzi atawateua waombaji hao kuwa ni wagombea pekee wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya mtaa.
Kanuni zinaelekeza mtu yeyote aliyeomba kuteuliwa kuwa mgombea au mgombea ambaye hakuridhika na uamuzi uliotolewa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi au anapinga uteuzi wa mgombea yeyote, anaweza kuwasilisha pingamizi.
Pingamizi hilo atamuomba msimamizi msaidizi wa uchaguzi kupitia upya uamuzi uliofanyika ili amteue kuwa mgombea au atengue uteuzi anaoupinga na msimamizi msaidizi wa uchaguzi, baada ya kupitia pingamizi husika, anaweza kukubali au kulikataa pingamizi hilo.
Kwa mujibu wa kanuni mwombaji au mgombea ambaye hataridhika na uamuzi wa msimamizi msaidizi wa uchaguzi atakuwa na haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufani iliyoanzishwa chini ya Kanuni ya 24 katika muda usiozidi siku nne kuanzia tarehe ya uamuzi wa msimamizi msaidizi wa uchaguzi.
Kanuni zinaelekeza kwamba kutakuwa na Kamati ya Rufani katika kila wilaya ambayo wajumbe wake ni katibu tawala wa wilaya ambaye atakuwa mwenyekiti.
Wajumbe wengine ni watumishi wanne wa umma kutoka taasisi za umma zilizopo katika wilaya husika na mtumishi mmoja wa umma ambaye atakuwa katibu na hatakuwa na haki ya kupiga kura.
Pia, kanuni zinaelekeza uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Rufani watateuliwa na katibu tawala wa mkoa siku saba kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa katika kanuni ya 25.
Wasiofaa kuwa wajumbe wa kamati
Kanuni zinataja wasiofaa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Rufani kwamba ni endapo anahusika na uteuzi wa wagombea, ni msimamizi wa uchaguzi, msimamizi
msaidizi wa uchaguzi au msimamizi wa kituo.
Wengine wasiofaa kuteuliwa kwenye Kamati ya Rufani ni endapo ni mtumishi wa halmashauri au kiongozi wa chama cha siasa katika ngazi yoyote.