MPANGO wa muda mrefu wa kuupeleka mchezo wa kriketi katika shule za msingi na sekondari nchi nzima ndiyo siri ya ushindi wa timu ya vijana wa chini ya miaka 19 katika michezo ya kufuzu Kombe la Kunia iliyomalizika jijini hivi karibuni.
Tofauti na miaka ya nyuma, kriketi hivi sasa inachezwa na vijana wa shuleni karibu nchi nzima na wengi wao ndiyo waliounda timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 19 ambayo sasa imeipanda daraja kutoka divisheni ya pili na kuwa ya kwanza, kwa mujibu wa msemaji na meneja mawasiliano wa chama cha kriketi nchini, TCA, Ateef Salim.
“Kuna vijana wengi hodari katika shule nyingi nchini kwa sasa, na kwa mujibu wa ligi ya shule inayoendelea, mafanikio makubwa yameonekana kwa shule za mikoa ya Arusha, Morogoro, Tanga, Mwanza, Dodoma na Arusha,” alidokeza msemaji huyo wa TCA.
Kwa mujibu wa Salim, TCA ilizindua mpango unaoitwa Chanzo Kriketi (Grassroots Cricket Project) kiasi cha miongo miwili iliyopita ambao wachezaji nyota wa timu ya taifa walitawanywa katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kazi ya kufundisha kriketi shuleni.
Miongoni mwa wachezaji ambao hivi sasa wamekuwa ni waalimu wazuri wa Chanzo Kriketi ni pamoja na Benson Mwita, Hamis Kassim na Khalil Rehmetulla wakati wengine kama Riziki Kiseto wameweza kuzalisha wachezaji kama Kassim Kiseto ambaye alituzwa kama mtengeneza mikimbio bora wa mashindano yaliyomalizka hivi karibuni ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
“Kriketi imeshamiri vijijini na utakaposoma matokeo ya michezo ya Ligi ya Kriketi ya Shule utakuta majina mengi ya shule zinazofanya vizuri katika mchezo huu. Chama cha kriketi chini, TCA na kile cha dunia, ICC, vinapaswa kupongezwa kwa mafanikio haya,” alisema Salim.
Kwa mujibu wa Salim, wakati michezo ya kufuzu ikiendelea jijini Dar es Salaam, ligi ya shule nayo ilikuwa ikitimua nyasi katika viwanja mbalimbali nchini.
Mkoani Tanga, timu ya Mwenge iliifunga Usagara kwa wiketi 6 katika mchezo wa mizunguko 20.
Usagara ndiyo walioshinda kura ya kuanza na kuamua kuanza kwa kubeti, na uamuzi wao uliwafikisha kwenye mikimbio 63 baada ya wapigaji (batsmen) wote 10 kutolewa.
Vijana wa Mwenge walijipanga na kufaulu kuzipiku alama za Usagara kwa kutengeneza mikimbio 64 huku wakiangusha wiketi 4 tu na hivyo kushinda kwa wiketi 6.
Mkoani Morogoro, timu ya Shule ya Ngiloli iliifunga Lolela pia kwa wiketi 6 katika mchezo wa kusisimua.
Lolela ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 65 baada ya wapigaji wao wote 10 kutolewa.
Vijana wa Ngiloli waliweza kuzifikia alama hizo bila taabu kwa kupiga mikimbio 55 huku wakiangusha wiketi 4 na hivyo kupata ushindi wa wiketi 6.
Katika mchezo mwingine uliofanyika mkoani Morogoro, timu ya Mazimbu iliifunga Mtawala kwa wiketi 7.
Mtawala walioanza kubeti, walifanikiwa kutengeneza mikimbio 38 baada ya kupoteza wiketi 9 na hivyo kuwapa kazi rahisi vijana wa Mazimbu ya kutengeneza mikimbio 41 baada ya kupoteza wiketi 3.