KMC yaikamua Simba Sh100 Milioni

WALIOSEMA hakuna mkate mgumu mbele ya chai wala hakukosea, kwani baada ya mikwara mingi ya kudai kumzuia kiungo mshambuliaji Awesu Awesu kutoenda kokote, KMC imemuachia nyota huyo, lakini ikivuna Sh100 milioni kutoka Simba iliyombeba.

Awali, KMC iliigomea Simba iliyomsajili Awesu na kumpeleka kambini Ismailia, Misri kabla kukimbilia Kamati ya Sheria na Hadhi la Wachezaji ya TFF kushtaki kuwa amechukuliwa kinyemela kwani klabu hizo hazikukaa chini na kufanya makubaliano.

Awesu alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na KMC na alitimkia Msimbazi baada ya kuvunja mkataba na kuilipa timu hiyo Sh50 milioni ambazo zilirudishwa kwani kipengele hicho kinalenga timu ikishuka na kukiwa na makubaliano ya pande mbili, kitu ambacho hakikufanyika.

Kamati hiyo iliridhia madai ya KMC, iliyotoa msimamo wa kumrudisha Awesu kikosini na kuweka dau la klabu inayomtaka ilipe Sh200 milioni, japo mwenyewe aligoma na kuendelea kusalia Simba na dakika za mwisho kabla ya kufungwa usajili juzi, mabosi wea Simba walirudi tena kwa Wana Kino.

Taarifa zinasema Simba walienda na Sh70 milioni zilizogomewa na mabosi wa KMC na kuongeza hadi 80 milioni ambazo pia ziligomewa.

“Baada ya kuona tumekomaa wakafika bei ya Sh90 milioni ambazo hata hivyo tulizikataa kwani msimamo wetu ulikuwa ni Sh200 milioni na kama ingeshindwa kabisa basi angalau Sh150 milioni,” chanzo kutoka ndani ya kKMC kililiambia Mwanaspoti na kuongeza:

“Hata hivyo, walisema pesa ya mwisho kutoa itakuwa Sh100 milioni nasi tuliona sio mbaya kwani lengo ni kuona mchezaji anaenda kucheza anapopataka, lakini klabu inanufaika na mauzo, hivyo tukakubali hizo 100 na kuwaachia.”

Inaelezwa Simba iliamua kurudi KMC na kulipa fedha hizo kutokana na kocha Fadlu Davids kumhitaji mchezaji huyo, hivyo isingekuwa rahisi kumuacha arudi klabu aliyokuwa akiichezea ambayo alishaigomea kurudi.

Simba itashuka kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge kuvaana na Tabora United ikiwa ni mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.

Related Posts