WAKATI pambano la Namungo na Fountain Gate likiahirishwa jana Jumamosi kwa sababu za ishu za usajili, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, Mnyama Simba itashuka uwanjani kuanza msako wa taji la 23 la Ligi Kuu Bara kwa kuikaribisha Tabora United inayocheza msimu wa pili sasa.
Mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 10:15 jioni, itakutanisha makocha wapya kabisa katika ligi hiyo, Simba ikiwa na Fadlu Davids kutoka Afrika Kusini na Nyuki wa Tabora wakiwa na Francis Kimanzi kutoka Kenya.
Kabla ya mchezo huo wa Dar, saa 8:00 mchana wageni wa ligi, KenGold watakuwa wenyeji wa Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika mchezo mwingine unaosubiriwa kwa hamu kuona wageni wataanza na mguu gani mbele ya matajiri wa Singida.
Kwa pambano hilo la Dar, makocha wa timu hizo kila mmoja ataanza kuonja joto la Ligi Kuu, kwani wote ni mara yao ya kwanza kufundisha hapa Tanzania baada ya timu zao kuwanasa katika dirisha lililomalizika hivi karibuni la usajili, lakini macho yapo kwa Fadlu mwenye kibarua cha kuirudisha Simba heshima Bara.
Msimu uliopita, Simba ilimaliza ligi hiyo ikiwa nafasi ya tatu, ikitoka kapa kwa msimu wa tatu mfululizo bila kubeba ubingwa wa Bara wala michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya awalui kutwaa Ngao yua Jamii iliyoipoteza msimu huu mbele ya Yanga.
Hivyo, kocha huyo ana kibarua cha kutaka kuonyesha mashabiki wa klabu hiyo, kwamba yeye nui mtu sahihi baada ya kuajiriwa hivi karibuni na kwenda pre season kambini jijini Ismailia, Misri, lakini akianza na timu iliyonusurika kushuka daraja kupitia play-off.
Timu hizo zimekutana mara mbili ambazo zote zilikuwa ni katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita ambapo Simba ilivuna pointi sita katika mechi hizo.
Mchezo wa kwanza, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 ikiwa ugenini na zilipokutana mara ya pili, Tabora United ilipoteza kwa mabao 2-0.
Simba imekuwa na historia nzuri ya ushindi katika mechi za mwanzo za msimu ambapo imekuwa ikipata matokeo mazuri mara kwa mara na kuthibitisha hilo, imepata ushindi katika mechi nane kati ya 10 za mwanzo kwenye misimu 10 iliyopita, ikifunga mabao 26 sawa na wastani wa mabao 2.6 kwa mechi na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.
Tabora ambayo huu ni msimu wake wa pili kushiriki Ligi Kuu, mechi moja iliyocheza nyuma ya kwanza kwenye msimu haikuacha kumbukumbu nzuri kwao kwani walipoteza kwa mabao 4-0 mbele ya Azam FC na hivyo leo ni fursa kwao kuondoa nuksi kwa kupata ushindi dhidi ya Simba.
Hata hivyo, Tabora imefanya marekebisho makubwa ya kikosi chake msimu huu kulinganisha na uliopita ambapo hivi sasa inao nyota kadhaa ambao kama Simba isipowachunga wanaweza kuamua matokeo ya mchezo kwa upande wao.
Timu hiyo kutoka mkoani Tabora imekuwa na nuksi na mechi za ugenini katika Ligi Kuu kwani tangu ilipopanda daraja, haijawahi kupata ushindi katika mechi zote za ligi ilizocheza ugenini.
Msimu uliopita katika mechi 15 za Ligi ilizocheza ugenini, ilitoka sare tano na kupoteza michezo 10 huku ikifunga mabao saba na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26.
Simba nyumbani imekuwa haina unyonge na hilo linajidhihirisha kwa matokeo ya mechi 15 za Ligi Kuu msimu uliopita ilizocheza ikiwa nyumbani ambapo imepata ushindi mara 11, imetoka sare mbili na kupoteza michezo miwili na imefunga mabao 30 huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12.
Matumaini makubwa kwa Simba leo hapana shaka yapo kwa mshambuliaji wake mpya Leonal Ateba ambaye timu hiyo ilimsajili siku ya mwisho ya kufungwa kwa usajili wa dirisha kubwa, Agosti 15 akitokea USM Alger ya Algeria.
Tabora inaonekana itaelekeza matumaini makubwa kwa washambuliaji mwenye uzoefu mkubwa na Ligi hiyo Heritier Makambo na Yacouba Songne waliowahi kuitumikia Yanga misimu kadhaa iliyopita, pia ikiwa na majembe mengine kama Morice Chukwu, Faria Ondongo, Ismail Mhesa, Abdallah Seseme na Offen Chikola.
Kocha wa Simba akizungumzia mchezo huo alisema wamejiandaa kuanza vyema msimu, kwani pointi tatu za mwanzo ni muhimu kwa timu inayotaka mafanikio.
“Tunahitaji kuwa na mafanikio msimu uu, kila mechi ya Ligi tuna lengo la kubeba pointi tatu na naamini mechi ya kesho (leo) itakuwa hivyo kutokana na maandalizi mazuri tuliyofanya na wachezaji,” alisema Fadlu huku kocha Kamanzi akisema anaiheshimu Simba, lakini hawaiogopi na watapambana kwa dakika zote 90.
Fadlu atawategemea nyotya wapya aliotua nao kikosini kama Augustine Okejepha, Debora Mavambo, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, mbali na Ateba na wakali wengine ambao watakuwa na kazi ya kuipa Simba pointi hizo ili kuanza vyema msimu.
Mchezo huo wa Simba na Tabora United utatanguliwa na ule wa KenGold dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuanzia saa 10:00 jioni. Ni mechi ya ukaribisho kwa KenGold ambayo ndio inashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tofauti na Singida Black Stars ambayo huu ni msimu wake wa tatu.
Hata hivyo, katika misimu miwili ambayo timu hiyo ilishiriki, ilikuwa ikijulikana kama Ihefu hivyo huu ni msimu wa kwanza ikicheza Ligi Kuu kwa kutumia jina la Singida BS.
Ni mechi inayotarajiwa kuwa na msisimko kutokana Singida inayonolewa na kocha Patrick Aussems mwenye uzoefu wa ligi hiyo, huku ikiundwa na mastaa wa ndani na nje ya nchi wenye majina makubwa, tofauti na KenGold.