Lissu asisitiza msimamo wa kumjibu Msigwa

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu amesisitiza msimamo wake wa kutaka kujibiwa kwa hoja za aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa ambaye sasa amejiunga na CCM.

Sambamba na hilo, amesisitiza pia msimamo wake wa kuondoka ndani ya Chadema iwapo kitakwenda kinyume na sababu zilizomfanya ajiunge nacho akisema, “Chadema sio mama yangu.”

Kwa mara ya kwanza, Lissu alionyesha msimamo wa kutaka kujibiwa kwa tuhuma zinazoibuliwa na Mchungaji Msigwa dhidi ya Chadema tangu Juni mwaka huu alipowasili  nchini akitokea Ubelgiji.

“Kwa kuzingatia tuhuma zenyewe, zinatakiwa zijibiwe. Kama mali zisizohamishika majengo na chochote kitakuwa na nyaraka, lakini kama mali zinazohamishika kama fedha hizo vile vile zina nyaraka,” alisema Lissu alipozungumza na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Miongoni mwa tuhuma zinazoibuliwa na Msigwa dhidi ya Chadema tangu alipohamia CCM, Juni 30 mwaka huu, ni ufisadi anaodai upo ndani ya chama hicho.

Moja ya matendo aliyoyarejea kama ya kifisadi ni fedha zaidi ya Sh2 bilioni walizochangishwa waliokuwa wabunge wa chama hicho mwaka 2015, ambazo amedai hadi sasa haijulikani zilipokwenda.

Lissu ameyasema hayo jana usiku alipohojiwa katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Kituo cha Luninga cha Star TV.

Amesema kuna umuhimu wa mamlaka sahihi ndani ya Chadema kuzijibu hoja za Mchungaji Msigwa kuhusu ubadhilifu wa fedha ndani ya chama hicho.

Lissu amesema hawezi kuzijibu tuhuma hizo kwa sababu hana mamlaka kwa kuwa nyaraka zote za chama hicho, huwa chini ya ofisi ya Katibu Mkuu (John Mnyika) ambaye ndiye anayepaswa kumjibu.

“Hoja za Msigwa sio ngumu kwa sababu rekodi za fedha zipo hizi fedha zinazosemwa zimeenda wapi kutakuwa na akaunti za chama ukimuuliza Katibu Mkuu wa chama au mtu wa fedha wa chama ana majibu,” amesema.

Suala la uamuzi wa kumjibu Mchungaji Msigwa, amesema wamekuwa wakilizungumza hata katika vikao vya ndani vya chama hicho.

Majibu hayo ya Lissu, yalitokana na swali aliloulizwa ni nini kinaifanya Chadema ikae kimya dhidi ya tuhuma zinazoibuliwa na Mchungaji Msigwa.

Katika hatua nyingine  Lissu amezungumzia kuhamia CCM kwa Mchungaji Msigwa akisema ni pigo kwa chama hicho, kwa kuwa alifanya kazi vema akiwa ndani ya Chadema, anafahamu utendaji wake na zaidi walikuwa marafiki.

“Ni rahisi sana kumtukana kwa sababu amekwenda huko (CCM) lakini mimi niliyefanya naye kazi kwa ukaribu zaidi tumepoteza,” ameeleza.

Hata hivyo, amesema pamoja na urafiki wao hakumshirikisha juu ya uamuzi wake wa kuhamia CCM na anadhani wangegombana iwapo angemwambia.

Ameeleza tangu Msigwa alipoihama Chadema hawakuwahi kuwasiliana akisisitiza, haoni watakachozungumza.

“Mimi na Msigwa ni marafiki sana tangu mwaka 2006 na kwa sababu tulikuwa kwenye mapambano. Amejiunga na kambi ya adui kawaida yangu huwa… sasa tutazungumza nini,” amesema.

Kauli ya ‘Chadema sio mama yangu’

Katika mahojiano hayo, Lissu amesema kauli ya Chadema sio mama yake lilitokana na swali aliloulizwa katika moja ya mijadala kwamba wapinzani wakinyang’anywa madaraka wanakwenda upande wa pili.

Katika swali hilo, amesema aliulizwa atoe hakikisho kwamba hataondoka ndani ya chama hicho hata iweje, ndipo alipojibu kwamba Chadema si mama yake, kikikiuka misingi iliyomfanya ajiunge nacho atakiacha.

“Katika wote waliopo Chadema nani Chadema ni mama yake, ni chama cha siasa. Tunajiunga na chama cha siasa kwa sababu fulani,” amesema.

Hata hivyo, amewajibu wanaomkaribisha kujiunga na CCM baada ya kauli yake hiyo, akisema kwa kuwa ana akili timamu: “No thank you.”

Katika maelezo yake, Lissu amesema hana uhakika kama hatua ya kukamatwa kwa viongozi na wafuasi wa Chadema waliokuwa wanakwenda na waliokuwepo Mbeya kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani ilitokana na amri ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi

Msingi wa majibu yake hayo ni swali aliloulizwa iwapo anaona kukamatwa kwa viongozi na wafuasi wa Chadema Agosti 11, mwaka huu ni agizo la Dk Nchimbi.

Swali hilo, limerejea tukio la Agosti 11, mwaka huu lililohusisha kukamatwa kwa viongozi na wafuasi wa chama hicho 520, baada ya kukaidi amri ya Jeshi la Polisi ya kusitisha shughuli ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Jeshi hilo lilikizuia chama hicho kufanya shughuli hiyo kwa kile lilichodai liliona dalili ya kuvunjika kwa amani na vurugu ndani yake, likirejea maneno yaliyotamkwa na Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana la chama hicho, Twaha Mwaipaya.

Mapema baada ya tangazo la kufanyika kwa shughuli hiyo lililotolewa na Katibu Mwenezi wa Bavicha Taifa, Twaha Mwaipaya Msajili wa Vyama vya Siasa aliandika barua ya kuisihi Chadema isitishe maadhimisho hayo.

”Siku ya Agosti 12, waje washuhudie vijana wote nchi nzima tunakutana Mbeya, siku hiyo ni siku ya kwenda kuweka hatama ya Tanzania…tupo serious sana na jambo hili.

“Vijana wa CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, tunakwenda kuacha uteja wa Serikali na kuweka maazimio makubwa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025,” alisema Mwaipaya katika kipande cha video ya kuwahamasisha vijana kushiriki shughuli hiyo.

Katikati ya tukio hilo, Dk Nchimbi aliingilia kati na kumwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni awaachie viongozi hao na kusisitiza vema yafanyike mazungumzo badala ya hatua iliyochukuliwa.

Haukupita siku, viongozi na wanachama wa Chadema waliachiwa huru.

Akifafanua hilo katika majibu yake, Lissu amesisitiza hana ushahidi wala uhakika kama waliachiwa kwa amri ya mtendaji mkuu huyo wa CCM.

Hilo linatokana na kile alichoeleza, wito wa kuachiwa haukutolewa na Dk Nchimbi pekee ni wadau na watu wengi walifanya hivyo.

“Kitu tofauti ni kwama CCM haina historia ya kutetea mpinzani yeyote anayeonewa au kuumizwa na Serikali ya CCM, kwa hiyo kama kuna tofauti ni hiyo,” amesema.

Hata hivyo, amesema ameichukulia kauli ya CCM kama uthibitisho kuwa walikamatwa kwa kuonewa kwa kuwa si mara zote chama hicho kinawatetea wapinzani.

Lakini, amesema ni vigumu kuitenganisha CCM na hatua ya kukamatwa kwao, kwa kuwa vyombo vya dola vipo chini ya Serikali ambayo ni ya chama hicho tawala.

Alipoulizwa kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, Lissu amesema ni mbaya kwa sababu limedhibitiwa kioperesheni, kiutawala na utendaji kwa ujumla.

Kudhibitiwa huko, amesema ndilo kunakofanya shughuli zake ziingiliwe na watawala na mzizi wa yote ni Katiba iliyotoa mwanya kwa kila kiongozi kuwa na amri juu ya jeshi hilo.

Kwa sababu hiyo, ameeleza matatizo yaliyopo ndani ya jeshi hilo ni mfumo uliosababishwa na kasoro za kisheria na kunahitajika mabadiliko ya Katiba iondoe mamlaka ya yeyote kuliamuru.

“Mamlaka ya Amiri Jeshi Mkuu iishie kwenye kuwateua maofisa wakuu na kutangaza vita pekee.

“Kama Rais anaweza akamuamuru polisi akamate mpinzani maana yake jeshi hilo halina uhuru wa kioperesheni,” amesema.

Katika mahojiano hayo, Lissu ameonyesha matatizo yanayoikabili Tanzania yanatokana na mfumo ambao msingi wake ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Msingi huo, ameeleza ni Katiba tangu mwaka 1962 ilipoasisiwa na Mwalimu Nyerere baada ya uhuru, hivyo haiwezekani kumtenganisha mwasisi huyo wa Taifa na changamoto ya mfumo wa kiutawala uliyopo.

Kwa mujibu wa Lissu, hata wakati wa Mwalimu Nyerere watu wengi walioonekana kumpinga waliwekwa kizuizini.

Lissu ametumia mahojiano hayo kupigia msumari nia yake ya kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, aliyonayo sasa.

Katika kulithibitisha hilo, amesema alishamwandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika ya nia yake hiyo kama miongozo ya chama hicho inavyotaka.

“Mwanachama anayetaka kugombea kwa mujibu wa kanuni kwa kutegemea nafasi anayotaka, anatakiwa kumwandikia Katibu wake wa ngazi husika barua ya kusudio la kutaka kugombea,” amesema.

Pamoja naye, nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho ilishatiliwa nia hadharani na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje Agosti 5, mwaka huu alipozungumza na wanachama wa chama hicho jijini Mwanza.

Alipoulizwa Lissu kuhusu nia ya Wenje, amejibu kama hajafuata mwongozo wa Chadema wa kuandika nia yake kwa Katibu wa ngazi husika bado si mtia nia.

Ingawa, amesema chama hicho hakifungi milango ya mtu yeyote kugombea iwapo ataanza kwa kutangaza hadharani, kisha akaandika barua kwa mujibu wa kanuni.

Lissu amesema amefanya hivyo hata katika nia yake ya kugombea urais mwakani, huku aliahidi kumuunga mkono yeyote atakayepitishwa na chama hicho kuwania nafasi hiyo, iwapo hatapendekezwa yeye.

“Sikuzaliwa nije kuwa mgombea urais wa Chadema nilijiunga na Chadema hata miaka 20 haifiki na nimefanya hivyo nikidhani ndicho chama chenye msingi ya ukweli wa mabadiliko ya kijamii na kila kitu. Nimekuwa tayari na niko tayari kutumikia nafasi yoyote ile,” ameeleza.

Lakini, amesema atakaposhinda urais moja ya vitu atakavyofanya ni kujiuzulu wadhifa wake ndani ya Chadema ili kutenganisha dola na chama, tofauti na ilivyo sasa kwa CCM.

Sambamba na kujiuzulu kwake, amesema atabadili na Katiba ili kuweka msingi mzuri ili jambo hilo lisitokee atakapoingia mtawala yeyote.

“Kumekuwa na kama mapacha wanaofanana ukitenganisha dola na CCM, chama hicho kinakufa. Kama tukiiondoa CCM kitu ambacho tumekisema mara zote ni Katiba mpya,” amesema.

Katika mabadiliko hayo ya Katiba, amesema hawatapata kitu kipya zaidi ya kwenda na mapendekezo ya Tume ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba kwa kuwa iliweka wazi kuwa kiongozi wa nchi hapaswi kuwa kiongozi wa chama.

Katika hali isiyojulikana na wengi, Lissu amesema katika maisha yake amewahi kuwa mwanachama wa CCM.

Ingawa uanachama wake huo, amesema haukutokana na mapenzi yake na chama hicho, bali ilikuwa kazima kutokana na mazingira ya wakati huo.

“Kwa watu wasiojua sisi wa umri fulani kuna kipindi tulikuwa wanachama wa CCM. Mtu yeyote aliyeenda JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) nyuma ya mwaka 1993 alikuwa mwana CCM ilikuwa ni lazima,” amesema.

Kipindi hicho, amesema ukimaliza mafunzo ya JKT pamoja na cheti cha jeshi hilo, ulikabidhiwa kadi ya CCM.

Hata mwaka 1991 alipokwenda kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu, amesema pamoja na cheti cha jeshi alitakiwa pia kuonyesha kadi ya CCM.

Amesema utaratibu huo, uliondolewa mwaka 1993.

Mwaka 2017, mwanasiasa huyo alishambuliwa kwa risasi jijini Dodoma, karibu na viwanja vya Bunge.

Licha ya tukio hilo lililomsababishia ulemavu wa kudumu, amesema itabaki kuwa aibu ya nchi, Serikali na jeshi la polisi kwa kutochunguzwa tukio hilo.

Amesema upo utaratibu wa kisheria unaotoa mwanya wa shahidi kuhojiwa hata anapokuwa nje ya nchi yake, lakini katika tukio lake haikufanyika hivyo.

Ameeleza alipokuwa Kenya kwa matibabu, Jeshi la Polisi liliwahi kumtafuta nduguye kumweleza nia yao ya kwenda kumuhoji, lakini hadi sasa hawakuwahi kufanya hivyo.

Ameliambatanisha hilo na hatua ya kutolipwa fedha za matibabu alizotumia, ingawa kiinua mgongo chake alilipwa miaka mitatu baada ya ubunge wake.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipokwenda Ubelgiji kwa ajili ya shughuli za kikazi pamoja na mambo mengine walizungumzia juu ya kulipwa kwake gharama za matibabu.

Amesema Mkuu huyo wa nchi alimtaka kumwandikia barua na vielelezo vyote na kumwelekeza namna atakavyoifikisha ili alipwe

Ameeleza hadi sasa ameshaandika barua na kuzituma mara mbili bila mafanikio na hata alipowahi kufuatwa na mtoto wa Rais Samia, alimkabidhi nakala ya mwisho Novemba mwaka jana.

“Aliponifuata akisema anataka kunisaidia, nikamwambia wewe unataka kunisaidia mimi. Namna ya kunisaidia mimi kamwambie mama yako anipe hela zangu kwa sababu nadai fedha zangu,” amesema Lissu.

Pamoja na kijana huyo kukubali na kukabidhiwa barua hadi sasa Lissu amesema hajapokea malipo hayo.

Pesa chafu ndani ya Chadema

Mwanasiasa huyo, amesema mambo yaliyofanyika katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho yanaashiria kulikuwa na fedha chafu ndani yake.

Hilo linatokana na kile alichofafanua, nyakati zote chama hicho kinahangaika na fedha za kufanya mikutano yake, ilishangaza kuona katika uchaguzi kunakuwa na matangazo na mikutano ya gharama kiasi kile.

“Kuna kila sababu ya kuamini kwamba kuna fedha chafu. Hivi nchi hii na kila mtu anajua kuna rushwa sana kwenye nyanja mbalimbali za maisha yetu ya umma na kwenye siasa zetu. Ni jambo geni kiasi gani,” amehoji.

Amesema jambo geni ni kuwepo mazingira yanayozuia kueleza ukweli juu ya kuwepo kwa fedha chafu katika mamlaka na taasisi mbalimbali.

Hata hivyo, Lissu hakuweka wazi ni nani alipokea fedha hizo chafu, ingawa alidai anadhani zimetoka CCM.

Msimamo wa Lissu, amesema ni kuwekwa hadharani kiasi na matumizi ya fedha zilizochangwa wakati wa Operesheni ya Join the Chain iliyoendeshwa na chama hicho.

Kwa sababu fedha hizo zilikusanywa kwa njia ya mitandao na benki, amesema bila shaka nyaraka zipo ni sahihi watu kuhoji zilivyotumika na sahihi kuambiwa ukweli.

“Ni jambo jema hesabu hizo ziwekwe wazi kwa sababu kinyume na hivyo kunakuwa na hisia tofauti,” ameeleza.

Hata hivyo, amesisitiza hawezi kuwa na majibu sahihi atakapokuwa kuhusu fedha hizo kwa sababu hakuwa muhusika katika ukusanyaji wala kuzitunza.

“Ni suala ambalo tumelijadili mara nyingi ndani ya chama na kwamba watu wa fedha na Katibu Mkuu ni watu sahihi kulijibu,” amesema.

Kuhusu michango ya kununua gari mpya baada ya la awali kuwa na matundu ya risasi, amesema katika hesabu za mwisho ilifika zaidi ya Sh100 milioni.

Tangu hapo, amesema hakupiga tena hesabu na anahitaji utulivu ili afanye hivyo.

Ameeleza bado hajajua gharama halisi na aina ya  gari atakalonunua na atafanya hivyo muda utakapofika.

Amesema michango hiyo haikuanzishwa naye na walioanzisha ndiyo watakaosema mwisho wake.

“Walioanzisha walisema wanataka kupata fedha ya kununua gari jipya ili lililopo liwekwe makumbusho. Sikuwahi kuangalia gari jipya linagharimu kiasi gani na utafika wakati nitaangalia,” amesema.

Amesema mabadiliko ya sheria yaliyobadilisha jina la tume ya uchaguzi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), hayana tija yoyote katika kuleta uchaguzi huru na wa haki.

Kwa sababu, amesema jina la tume limebadilika lakini utendaji na  mwenendo ni ule ule na hata viongozi wake ni wale wale.

“Ili kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, kwanza ni kufanya mabadiliko ya Katiba kwenye mambo yote yanayohusu tume na mamlaka yake kwenye masuala ya uchaguzi,” amesema.

Mabadiliko hayo, amesema yahusishe namna ya kuwateua makamishna, kuwapata watendaji, mamlaka na shughuli za tume, uwajibikaji wake na masuala ya fedha za kuendeshea shughuli za tume.

Katika mahojiano hayo, Lissu ameweka wazi msimamo wa chama hicho kuendelea kushiriki chaguzi mbalimbali licha ya kudai kuwapo kwa mazingira magumu.

Amesema awali waliahidi kususia chaguzi zote zitakazofanyika bila ya uwepo wa Katiba mpya, lakini kwa sasa wameona ni vema washiriki kuonyesha upinzani.

“Silaha ya kususia ni muhimu lakini inapaswa kutumika mara chache zaidi. Iwe silaha ya mwisho kabisa,” amesema.

Related Posts