MAGWIJI WA TIBA RADIOLOJIA DUNIANI WAKUTANA MUHIMBILI KUJADILI MBINU ZA KUONGEZA WIGO WA HUDUMA HIYO NCHINI

Magwiji wa tiba radiolojia duniani ambao hutumia vifaa kama vile CT-Scan, MRI, Xray, Angiography system, Utrasound n.k kufanya uchunguzi na kutibu magonjwa mbalimbali kupitia matundu madogo, mapema wiki hii wamekutana Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutathmini hali ya utoaji huduma hiyo nchini na kujadili mbinu za kuongeza wigo wa huduma hiyo kuanzia ngazi ya hospitali zote za rufaa za kanda, kwani kwa sasa inatolewa tu kupitia hospitali ya taifa, maalum na hospitali chache za kanda.

Tiba radiolojia ni aina ya taaluma ya matibabu ambapo daktari bingwa mbobezi wa tiba radiolojia hutumia teknolojia ya picha (CT, Xray, Ultrasound) kumuongoza kufanya uchunguzi au tiba kupitia matundu madogo mwilini bila kufanya upasuaji mkubwa ili kuzibua mishiba ya damu iliyoziba au kusinyaa, kupunguza ukubwa wa uvimbe au vivimbe, kutibu kuvuja kwa damu (kunakosababishwa na kupasuka kwa mishipa midogo ya kwenye tumbo na utumbo), kuingiza dawa ya kutibu uvimbe wa saratani moja kwa moja kupitia mishipa ya damu inayolisha uvimbe, kuchepusha damu kwenye ini lililonyafuka na matibabu mengine mengi.

Mratibu wa Tiba Radiolojia na Tiba Mtandao kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Grace Bash amesema lengo la Serikali ni kupunguza gharama za huduma hizo kutokana na uwekezaji ilioufanya kupitia vifaa tiba na kwa kutambua umuhimu huo, wizara ina kitengo maalum kinachoratibu upatikanaji wa huduma hizo nchini ambacho kwa sasa kipo katika hatua kadhaa za utengenezaji miongozo ya huduma hiyo.

Amesema, katika jitihada za kuongeza idadi ya wataalamu wa tiba radiolojia nchini, Serikali kupitia Mpango wa Ufadhili wa Dkt. Samia wa Huduma za Kibobezi kwa mwaka wa masomo 2024/2025 imetangaza kufadhili wataalamu waliochaguliwa katika vyuo vilivyopo ndani au nje ya nchi kwa ajili ya ubobezi wa tiba radiolojia.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema kuanzia Julai 2023 hadi Juni 2024, wagonjwa zaidi ya 2,700 wamepata huduma mbalimbali, ikiwemo kuziba mishipa inayolisha vivimbe vya kwenye kizazi kwa kutumia dawa ili kuufanya uvimbe huo kusinyaa na kuyeyuka badala ya upasuaji, kuziba mishipa ya damu iliyolika kutokana na vidonda sugu vya tumbo ambavyo humfanya mgonjwa kutapika damu, kuzibua mishipa ya damu ya miguu iliyoziba kwa wagonjwa wenye kisukari na kuwaepusha kukatwa miguu na huduma nyingine nyingi.

Ameongeza kuwa tiba radiolojia imeleta mageuzi makubwa kwa wagonjwa mbalimbali wakiwemo wa saratani kwani kupitia njia kifaa cha maalum hupelekwa moja kwa moja kupitia mishipa ya damu hadi kwenye uvimbe mahususi na kufanya matibabu hivyo kuongeza ufanisi wa hali ya juu wa tiba ukilinganisha na kuchoma sindano ambapo dawa kwanza lazima isambae mwili mzima ndipo ifike kwenye tatizo husika.







Related Posts