WADAU wa mchezo wa ngumi mkoani Mbeya wamesema mchezo huo unashindwa kupiga hatua kubwa kutokana na mabondia wa mikoani kutopewa nafasi kama ilivyo Dar es Salaam na hivyo kuwafanya wakali wengi wa mikoani kukimbilia jijini humo.
Baadhi ya mabondia ambao awali walikuwa wakitamba kwa kutoa vichapo mkoani Mbeya kama Tony Rashid na Alfonce Mwambalange ‘Mchumiatumbo’ hivi sasa wote wanawasha moto Dar es Salaam, huku Meshack Mwankemwa, Joseph Sinkara na Donald Mwakisu ndio wanaotesa kwa sasa hapa Mbeya.
Promota wa ngumi za kulipwa nchini, Edgar Mwansasu alisema Tanzania inao mabondia wengi na wenye vipaji, lakini jicho la karibu liko Dar es Salaam jambo linaloondoa ushindani kitaifa kwani wengi wanaowika wanakimbilia Dar.
Alisema mbali na Dar es Salaam kupewa kipaumbele, pia mwamko wa mikoani bado ni mdogo kwa wadau na mashabiki kutosapoti mchezo huo tofauti na ilivyo kwa michezo mingine ikiwamo soka.
“Nyanda za Juu Kusini vipo vipaji na mabondia wanafanya vizuri, lakini hawapewi nafasi kama ilivyo kwa Dar es Salaam, pia sapoti ni ndogo,” alisema Mwansasu.
Mwansasu alisema kwa muda aliodumu katika kazi hiyo anajivunia kuibua na kuwapandisha mabondia wanne, Joseph Sinkara, Meshack Mwankemwa, Maisha Samson na Joseph Maigwisa.
Promota mwingine, Gadina Mwakasyuka alisema kutetereka kwa mchezo huo mkoani Mbeya ni kutokana na kukosa uongozi ambao unaweza kuandaa mapambano ya kuwainua mabondia.
Alisema baada ya kuonekana mkoa huo umepoa, kwa sasa anakusanya nguvu kuanzisha mapambano kabla ya mwaka huu kumalizika ili kuwapa fursa mabondia mkoani humo.
“Kwanza hatuna uongozi, jambo linalowanyima fursa vijana, hakuna programu zozote za mchezo huo, sisi wadau ndio tunaamua kuandaa mapambano,” alisema Mwakasyuka.