Matokeo ya mtihani, mwanafunzi akishitaki chuo, AG kortini

Morogoro. Aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mwikwabe Mungine, ameruka kiunzi cha kwanza katika kesi ya madai ya fidia ya Sh600 milioni, dhidi ya chuo hicho, baada ya Mahakama Kuu kulitupa pingamizi la awali alilowekewa.

Mwingine amefungua kesi ya madai namba 3827 ya 2024 dhidi ya chuo hicho kama mdaiwa wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mdaiwa wa pili, kwa kile alichodai ni kwa kukiuka wajibu wao wa kisheria na uzembe.

Hata hivyo, wajibu maombi hao, licha ya kuwasilisha majibu yao ya utetezi kwa maandishi, waliwasilisha pia pingamizi la awali wakitaka Mahakama iifute kesi hiyo, wakidai ni mbaya kisheria kwa kufunguliwa kwenye jukwaa lisilo sahihi.

Lakini katika uamuzi wake mdogo alioutoa Agosti 15,2024 baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji  Latifa Mansoor wa Mahakama Kuu kanda ya Morogoro, alilitupilia mbali pingamizi hilo, akisema kesi hiyo imefunguliwa jukwaa sahihi.

Kutokana na uamuzi huo, sasa Mahakama itaendelea kusikiliza kesi ya msingi ambayo Mungine anajiwakilisha mwenyewe kortini, huku Mzumbe na AG wakitetewa na mawakili wa Serikali, Emma Ambonisye na Nzumbe Machunda.

Katika kesi hiyo ya madai, Mwikwabe Samo Mungine anadai kuwa yeye alikuwa mwanafunzi wa chuo hicho kikuu na kati ya Februari 21,2022 na Julai 2022, aliomba kuahirisha kufanya mtihani kwa mwaka wa masomo 2021/2022.

Hata hivyo anadai Septemba 18 2022, alilipia ada na kufanya mitihani lakini katikati ya Oktoba 2022, Chuo Kikuu Mzumbe kilitoa matokeo lakini hawakuwa wamepakia (upload) matokeo yake kwa mwaka wa masomo wa 2021/2022.

Kwamba mdaiwa wa kwanza ambaye ni Chuo Kikuu Mzumbe, alieleza tu kuwa mdai  “amefaulu mitihani yote”, na baada ya kuona kosa hilo, alimjulisha mdaiwa wa kwanza ili aweze kulirekebisha, lakini hata hivyo hakurekebisha kosa hilo.

Mwanafunzi huyo wa zamani wa Mzumbe aliendelea kudai maneno kuwa “amefaulu mitihani yote”, hayakuonyesha  daraja, hadhi, alama za UE (mitihani ya chuo) , GPA ya kila mwaka, daraja la jumla na GPA ya muhula huo wa masomo.

Licha ya mdaiwa kushindwa kurekebisha kosa hilo, mwanafunzi huyo alipewa namba ya malipo (control number) kwa ajili ya kulipia mwaka mpya wa masomo wa 2022/2023 na alilipia na kusajiliwa kwa ajili ya masomo ya mwaka wa tatu.

Julai 13,2023 kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, mwanafunzi huyo alimaliza mwaka wa tatu wakati kosa lile alilomjulisha mdaiwa likiwa halijarekebishwa.

Kulingana na hati hiyo, Mungine anadai kuwa licha ya jitihada zake za kutaka kosa hilo lirekebishwe, wadaiwa hawakurekebisha hadi pale alipotoa notisi ya siku 90 ya kusudio la kuwashitaki wadaiwa ambao ni Chuo Kikuu Mzumbe na AG.

Baada ya kuwapa notisi hiyo, chuo kilifanya masahihisho kuhusiana na matokeo ambayo hayakupakiwa kwa mwaka 2021/2022 na kuondoa maneno “amefaulu mitihani yote” na kuandika kuwa “carry over marks”, kuwa alama zilihamishwa.

Lakini Oktoba 20,2023, mwanafunzi huyo akapokea barua kutoka chuo kikuu Mzumbe ikimjulisha kuwa amefutiwa usajili (De-registered) wa masomo.

Hivyo mdai katika shauri hilo anasema mjibu maombi wa kwanza alishindwa kutimiza wajibu wake wa kuchapisha matokeo yake kwa mwaka wa masomo 2021/2022 na kwamba huo ulikuwa ni uzembe ambao umemletea athari.

Katika maombi yake, anaiomba mahakama iwaamuru wadaiwa kumlipa fidia ya jumla kwa uvunjaji wa wajibu wa kisheria, kumlipa fidia maalumu ya Sh600 milioni kwa kosa hilo na madhara aliyoyapata na pia waamriwe kulipa gharama za kesi.

Wajibu maombi hao katika majibu yao ya pamoja ya maandishi, walikanusha madai yote hayo huku wakitaka mdai ayathibitishe, lakini wakaenda mbali na kuwasilisha pingamizi hilo la awali wakitaka Mahakama iitupe kesi hiyo.

Katika usikilizwaji wa pingamizi, mawakili wa Serikali waliowatetea wadaiwa, walidai kosa kama lipo, basi lilifanywa na seneti na uamuzi wa kumuondoa kwenye masomo ulifanywa na seneti kulingana na kifungu 23 cha chata ya chuo ya 2007.

Waliendelea kueleza kuwa kuidhinishwa na kutolewa kwa matokeo ya mtihani na kwa namna gani na lini matokeo yanatakiwa kutolewa ni kikoa cha pekee (exclusive domain) ya chuo hicho chini ya kanuni ya 28 ya kanuni za mitihani.

Mawakili hao walisema kama anataka kupinga uamuzi wa kiutawala uliofikiwa na seneti ya chuo, ni lazima afuate njia au utaratibu sahihi, badala ya kupinga uamuzi huo kupitia Mahakama.

Walieleza kuwa chuo kikuu cha Mzumbe kama taasisi ya umma, maamuzi yake hayawezi kupingwa kupitia kesi ya kawaida na kwamba kama kuna madai yanayotokana kwa chuo kukiuka wajibu, basi yafanywe kwa njia ya marejeo.

Hata hivyo, Mungine alipinga vikali hoja hizo akisema pingamizi haliwezi kukubalika kwa kushughulikiwa kama hoja za kisheria kwa kuwa uamuzi wake unahitaji uchunguzi wa sheria, kanuni na kufanyiwa tathmini kwa ushahidi.

Alisema ni sahihi kwake kuwashitaki wadaiwa kwa madai ya kashfa kwa kushindwa kuwajibika ambao wamepewa na sheria ambayo umemuumiza mdai.

Mungine aliendelea kueleza kuwa uzembe kama madai (tort) ni ukiukwaji wa wajibu wa kisheria wa kujali (take care) ambao unaharibu mdai na kunukuu vifungu 50(1), (2) na (8) vya sheria ya vyuo vikuu ya mwaka 2005.

Kwa mujibu wa Mungine, vifungu hivyo viko wazi kuwa mdaiwa wa kwanza ana wajibu wa kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri na kukiuka wajibu huo kutasababisha chuo kikuu kukabiliwa na matokeo ya makosa yake yenyewe.

Kuhusu kama Mahakama hiyo ni jukwaa sahihi ama la, Mungine alieleza mahakama inayo mamlaka chini ya kesi za madai, kupima kama wadaiwa walikuwa wamekosea na walifanya uzembe katika kutekeleza wajibu wao.

Alisema kesi hiyo sio mbaya wala haiko katika jukwaa lisilo sahihi, kwa kuwa kile kinachoombwa kinatokana na makosa ya wajibu na nafuu inayotokana na makosa hayo ni fidia kutokana na makosa yaliyotendwa na chombo cha umma.

Uamuzi wa Jaji ulivyokuwa

Katika uamuzi wake huo mdogo alioutoa Agosti 15,2024, Jaji Latifa Mansoor, alisema hakuna ubishi kuwa Chuo Kikuu Mzumbe ni chuo kikuu cha umma kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria ikiwamo chata yake ya mwaka 2007.

Jaji alisema chuo kikuu Mzumbe kinajiendesha chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kwamba haibishaniwi kuwa chuo hicho katika kutekeleza wajibu wake, kinatoa elimu na mafunzo, kufanya tafiti na kutoa huduma kwa umma.

“Nakubaliana na wasilisho la mdai kuwa ili kupima kama chuo kikuu Mzumbe kilikiuka wajibu wake wa msingi huo wajibu wenyewe ni lazima uthibitishwe kabla ya ili itoe mwanya sasa wa kupima fidia”alisema Jaji Latifa katika uamuzi wake.

Jaji akasema mamlaka ya usikilizwaji kesi za madai haujakasimiwa kwa chata ya chuo au sheria ya chuo kikuu na kama kuna ukiukwaji wa wajibu wa chuo ambao umesababisha wanafunzi kuumia na kustahili fidia, wajibu huo ni wa Mahakama.

“Kwa mtazamo wangu, mahakama kuu katika kesi za madai ndio jukwaa sahihi la kushughulikia madai ya fidia yanayotokana na makosa dhidi ya chombo cha umma kama vile kukiuka wajibu wa taasisi ya umma na hapa ni chuo kikuu,” alisema.

Jaji alisisitiza mamlaka ya kusikiliza madai ya fidia kutokana na uharibifu, ardhi au miamala ya kibiashara kati ya Serikali, taasisi zake na watu binafsi, yapo kwa mahakama hata yanapotokana na kutofanywa kwa wajibu wa kisheria.

Related Posts