Mwenza wako unamuomba ruhusa au unampa taarifa?

Dar es Salaam. “Niliwahi kufungiwa nje na mume wangu, akitaka nirudi nilikotoka, ilikuwa ngumu kumshawishi, nilikuwa kwenye msiba tena wa ndugu yake, yaani shemeji yangu, kisa tu niliondoka nyumbani bila kumuaga,” anaanza kusimulia Penina John.

Mama huyo wa mtoto mmoja wa miaka 12 na mumewe, Nelson Jumanne anasema siku hiyo alimpigia simu mumewe hakupokea, akalazimika kutoka kwenda msibani bila mumewe kuwa na taarifa.

“Ilikuwa msiba wa mama wa shemeji yangu ambaye ni rafiki wa mume wangu, ilitokea siku kama nne baada ya mazishi, nikaenda kuwatembelea kuwajulia hali, sikumuaga mume wangu, niliporudi nyumbani saa 2 usiku nilifukuzwa,” anasema.

Anasema, ilimlazimu kurudi kwa yule shemeji yake, ambaye alimpeleka nyumbani akiwa sambamba na mkewe, ndipo wakaleta amani kwenye familia ile.

Hata hivyo, Penina anasema pamoja na maswaibu yaliyomkuta, mumewe si mtu wa kuaga na wakati mwingine anaweza asionekane nyumbani hata siku tatu, asijue yuko wapi na akirudi hataki kuulizwa.

Penina ni miongoni mwa wanawake wengi wanaokutana na masaibu hayo, japo wengine wanatofautiana baadhi wakiamini hakuna haja ya kumuaga mumewe anapotaka kutoka kwenda kwenye mambo yake binafsi, achilia mbali ya kijamii.

Sarah Haule, yeye haamini kwenye kuaga na kuomba ruhusa kwa mumewe, anasema anapotaka kutoka hujiondokea tu na imeshazoeleka hivyo kwa mume wake.

Tabia ya Sarah inaakisi maisha ya wanandoa, Paul na Naima (siyo majina yao halisi) ambao walikuwa hawana utaratibu wa kuagana mmoja anapotoka.
Akisimulia kisa cha wanandoa hao, ndugu wa Naima anasema ilitokea siku moja dada yao katika toka yake akapata ajali eneo la Tazara na kupoteza maisha.

“Mumewe aliporudi nyumbani hakumkuta, alijua ni kawaida yake na hakuhangaika kumtafuta, siku ya tatu ndipo anakuja kufahamu mkewe alipata ajali na amefariki,” anasimulia kwa uchungu.

Mwanasaikolojia, Christian Bwaya anasema kuna uzuri na ubaya wake.

“Binadamu huwa tunapenda uhuru, japo unapoingia kwenye uhusiano kuna gharama na gharama kubwa ni kupoteza kiwango fulani cha uhuru.
“Kila mmoja anawajibika kwa mwenzake, mtu anapokuwa hawajibiki kwa mwingine hapo huwezi kusema kuna uhusiano,” anasema Bwaya.

Anasema, mbali na kupoteza sehemu ya uhuru wako, unapoingia kwenye uhusiano baadhi ya vitu ulivyokuwa ukifanya ukiwa singo vitaondoka, ikiwamo la kumuaga au kuomba ruhusa kwa mwenzako unapokuwa na safari zako.
“Hii ni kushirikishana taarifa, ili kujua uhusiano wenu una afya ni namna mnavyoshirikishana taarifa na hili la kuaga linaingia kwenye muktadha kwamba hakuna siri kati yenu na mwingine ana haki ya kujua uko wapi, unafanya nini na kina nani? 

Hata hivyo, anasema ndoa inahitaji kujenga katika mazingira ya kuaminiana, hivyo unapoaga unamtengenezea mazingira mwenzako ya kukuamini na usipofanya hivyo unampa mashaka.

“Ingawa upande mwingine unapotaka kujua sana mwenzako yuko wapi, anafanya nini? hili nalo huwa na ukakasi.”

Anasema kuna nyakati mtu huwa anahitaji nafasi, hivyo unapotaka kujua kila kitu cha mwenzako inaondoa ladha fulani.

“Pamoja na kwamba ni muhimu kuaga, lakini kwa upande mwingine ukimuamini mwenzako huwezi kumfuatilia sana, ni vizuri kuaga lakini haipendezi kufuatiliana fuatiliana,” anasema.

Wapo ambao hawajali, hawataki kujua wake zao wako wapi, wanafanya nini, watarudi muda gani kama ilivyo kwa Gaspar Mathayo, ambaye kwenye ndoa yake na mkewe, Christina iliyodumu kwa miaka 11 ndiyo maisha yao.

“Huwa sitaki kumuuliza chochote nikiamini anatambua wajibu wake kama mke, nampa uhuru na mimi huwa sipendi aniulize ulize niko wapi, au nikitaka kwenda kwenye safari zangu huwa naondoka tu,” anasema.
Kwa Said Juma ni tofauti kidogo, anasema yeye kama kichwa cha familia haruhusu mkewe ajiondokee nyumbani bila kuaga.

“Atakapofanya hivyo, lazima nitambadilikia, lakini nitampa nafasi ya kumsikiliza, nikiona alikuwa na hoja ya kufanya hivyo yatakwisha, la sivyo sitamuelewa,” anasema.

Anasema yeye kama baba na kichwa cha familia, lazima ajue watu wake na si mke tu, familia yote anayoihudumia, kila anayetoka yuko wapi na anafanya nini na atarudi muda gani.

“Huwezi mke wa mtu kujiondokea tu, hapo utakuwa wewe ndiyo umenioa au unamaanisha nini? Kwa upande wangu, mke wangu lazima aniombe ruhusa na nitaangalia safari yake ina mashiko? Nina uwezo wa kumkatalia kuondoka,” anasema.

Anasema hata yeye anapotaka kutoka huwa anaaga kwa mkewe, japo wapo wanaume hawapendi kufanya hivyo na hawataki wasumbuliwe na mke kutaka kujua wako wapi na nani na wanafanya nini?

Viongozi wa dini watoa mwongozo

Akizungumzia umuhimu wa kuagana kwa wenza, mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro anasema mke kumuaga mumewe ni ishara ya utii.

“Biblia imetaka wake watii waume zao, japo vitabu vya dini havijaelekeza kwamba ni wajibu wa mke kumuaga mumewe kila anapotaka kutoka, lakini kwa muktadha wa kutakiwa kutii, hiyo ni moja ya utii,” anasema.

Mchungaji Sendoro, ambaye pia ni mtaalamu wa ushauri na saikolojia anasema kuaga ni suala la utamaduni na mazingira na dini haijaelekeza hilo.

“Japo dini inataka watu waishi kwa kuheshimiana na kuthaminiana, hivyo kutoa taarifa mmojawapo anapohitaji kutoka si kwa mke tu, hata kwa mume au suala la kuomba radhi unapochelewa kurudi ni sehemu ya kuheshimiana.”
Anasema mke kuomba ruhusa kwa mumewe ni suala la kistaarabu, kwa falsafa ya kuwa mtiifu kwa mumewe, pia kuonyesha ustaarabu, hekima na busara.

“Wale wanaohisi kwa kupenda hufanya hivi, na kila mmoja ataona wajibu, siyo kwa mke tu, hata mume pia, kwani mkiingia kwenye ndoa ninyi ni mwili mmoja na mnapaswa kufanya yale yanayowapasa kama wanandoa,” anasema.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waisalamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema kwa mwongozo wa dini yao, mke anatakiwa kuomba ruhusa pale anapotaka kutoka kwenda kwenye safari zake.

“Ataomba ruhusa kwa kuwa mume ndiye kiongozi wa familia na kama asipofanya hivyo, basi huyo mwanamke hawajibiki katika kufanya yanayompasa kufanya kwenye ndoa yake na ana jukumu la kujirekebisha,” anasema.

Sheikh Mataka, ambaye pia ni Katibu mkuu wa Taasisi ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania na mwenyekiti mwenza wa kamati ya taifa ya dini mbalimbali, anasema mume anayo ruhusa kumzuia mkewe kutoka.

“Siyo tu kumzuia mkewe, hata kumzuia mtu kwenda nyumbani kwake ambaye ana shaka naye, ingawa kwa mke pia anaweza kutoa ombi hilo na kusema fulani simtaki hapa nyumbani na mume mwenye akili atalizingatia,” anasema.

Anasema ndoa na familia inajengwa kwa maelewano na siyo mabavu, kwani unapozungumzia maisha ya ndoa unazungumza maisha ya watu walioacha watu wao na kwenda kutengeneza familia mpya.

“Wanatakiwa kupendana wakiishi pamoja na kuwa mfano wa kutengeneza kizazi chao katika maisha ya upendo, kila mmoja ana haki ya kumpa mwenzake ulinzi na kufichiana aibu zao.

“Mke kuomba ruhusa kwa mumewe na vivyo hivyo mume kumuaga mkewe ni kitendo cha busara na kitendo hiki hakionyeshi uwepo wa kudharauliana, hivyo watapeana taarifa zinazowahusu sababu kila mmoja anawajibika kwa mwenzake.

Related Posts