Ndugu watatu walivyomuua balozi CCM, walimkata kiganja mbele ya mke, mtoto

Moshi. Mahakama ya Rufani, imebariki adhabu ya kifo iliyotolewa kwa ndugu watatu wa familia moja, akiwamo mwanamke, waliomuua Balozi wa Nyumba Kumi, Sebastiano Kimaro.

Wauaji walitekeleza mauaji hayo Aprili 28, 2019, saa 9 alasiri huko Kibosho Kirima, Wilaya ya Moshi huku mke na mwanaye wakishuhudia. Walimshambulia kwa mkuki, mishale na panga hadi kuondoa kiganja cha mkono wa kulia.

Katika hukumu hiyo imetolewa na jopo la majaji watatu— Dk Marry Levira, Zephrine Galeba na Mustafa Ismal Agosti 16, 2024, walioketi Moshi ambao wamebariki adhabu hiyo ya kifo kwa Ibrahim Abubakary, Salima Abubakari na Hadija Shio.

“Titus Kimaro (marehemu) alivuta pumzi ya mwisho siku hiyo. Aliuawa katika mwangaza na macho ya wanafamilia yake, baada ya kujeruhiwa vibaya na vitu vyenye ncha kali vilivyosababishwa na warufani (wauaji),” walisema majaji hao.

Tukio la mauaji lilivyokuwa

Aprili 28, 2010, marehemu aliyekuwa Balozi wa Nyumba Kumi (CCM) huko Kibosho Kirima, alikwenda kusuluhisha mgogoro wa ardhi uliojitokeza kati ya familia ya warufani na mtu mmoja aliyetajwa mahakamani kuwa ni Joseph.

Wakati akiendelea kusuluhisha mgogoro huo, warufani walishuku marehemu aliegemea upande wa mpinzani wao na hilo likawafanya wamshambulie kwa panga, mkuki na mshale.

Mashambulizi hayo yaliyoelekezwa sehemu mbalimbali za mwili wake, zilimsababishia majeraha mabaya ambapo wauaji hao walienda mbali na kufikia hatua ya kukata kiganja cha mkono wa kulia na kumsababishia umauti.

Mke, mtoto walivyoshuhudia

Wakati mauaji hayo yakifanyika, mke wa marehemu, Regina Titus aliyekuwa shahidi wa pili wa Jamhuri, alifika eneo la tukio baada ya kusikia kelele kutoka kwenye shamba jirani kwake, alikimbilia kuona nini kinatokea.

Alimuona mrufani wa kwanza, Ibrahim akimrushia mshale mumewe ambao ulimpata katika mguu na akaanguka chini, ikifuatiwa na mashambulizi ya panga kutoka kwa warufani Salima na Hadija.

Baadaye Ibrahim alimshambulia tena mumewe kwa mshale na safari hiyo ulimpata begani, huku mrufani wa tatu, Hadija alimshambulia lakini safari hiyo kwa mkuki na mrufani wa kwanza alirudi na kumshambulia kwa kumkata kiganja.

Wakati matukio yote hayo yakitokea, mtoto wa marehemu, Esther Titus aliyekuwa shahidi wa tatu na Francis Ferdinand aliyekuwa shahidi wa nne, nao walikuwa eneo la tukio wakishuhudia tukio hilo.

Taarifa za mauaji hayo ziliwafikia polisi na askari mwenye cheo cha sajini, Multo mwenye namba E.4932 aliyekuwa shahidi wa tano, alifika eneo la tukio na kukamata jambia, panga, upinde na mishale 19 na kuchukua mwili wa marehemu.

Mwili huo ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi uliofanywa na Dk Patrick Amsi aliyekuwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri ambaye alibaini sababu za kifo kuwa ni kutoka damu nyingi kulikosababishwa na majeraha mabaya.

Katika utetezi wao mahakamani, warufani walikanusha kosa la mauaji ya kukusudia na kueleza kuwa familia yao iliingia katika mgogoro wa kidini na jirani yao, mgogoro uliosababisha nyumba yao kuchomwa moto.

Walishangaa namna walivyohusishwa na tukio hilo ambalo walikuwa hawalifahamu na walipoulizwa kuhusu ushahidi wa mashahidi wa tatu na nne ambao walishuhudia tukio hilo, walisema mashahidi hao hawakuwepo eneo la tukio.

Baada ya kukamilika kwa usikilizwaji wa ushahidi, Jaji Safina Simfukwe aliwatia hatiani washtakiwa wote watatu kwa kosa la mauaji ya kukusudia na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa, kwani ndio adhabu wanayoistahili.

Walikata rufaa Mahakama ya Rufani wakipinga adhabu ya kifo wakiegemea sababu tisa za rufaa, ikiwamo kuwa jaji alikosea aliposema mnyororo wa utunzaji vielelezo ulizingatiwa.

Warufani hao walitetewa na jopo la mawakili sita— Mashaka Ngole, David Shillatu, Dominicus Nkwera, Desderius Hekwe, Hamis Mayombo na Lilian Mushemba, huku upande wa Jamhuri wakitetewa na mawakili wa Serikali Rose Sule na Isack Mangunu.

Katika hoja zao, mawakili hao walisema wazee washauri wa mahakama hawakupewa muhtasari wa kesi kwa mujibu wa sheria, kabla ya kutoa maoni yao na kusema waliegemea ushahidi wa shahidi wa pili uliondolewa na jaji.

Hata hivyo, wakili Mangunu akijibu hoja hiyo alisema hakuona tatizo kwa namna jaji alivyowasomea wazee hao muhtasari wa ushahidi wa kesi hiyo, lakini majaji wa rufaa katika uamuzi wao walisema hitimisho la jaji lilizingatia viwango.

Mawakili hao waliibua pia hoja kuwa ushahidi wa upande wa Jamhuri uligubikwa na mkanganyiko na kutolea mfano ushahidi wa shahidi wa tatu na wa nne ambao walieleza mashahidi hao walipishana ushahidi wao katika jambo moja.

Katika uamuzi wao kuhusu hoja hiyo, majaji walisema wamepata tabu na kujitahidi kutafuta maana ya hoja ya mawakili hao na kwamba mkanganyiko huo ulikuwa mdogo na haukugusa mzizi wa kesi, hivyo hoja hiyo nayo wakaitupa.

Kuhusu hoja ya kupokelewa kwa kielelezo P2 hakikuzingatia mnyororo wa utunzaji (chain of custody) kwamba Inspekta Kapusi hakuelewa alitunza wapo kielelezo hicho baada ya kukichukua kutoka katika eneo la tukio.

Majaji walisema waliipa uzito hoja hiyo, lakini wakasema hoja hiyo haipaswi kuwachukulia muda mrefu kuiamua, kwani kumbukumbu za mahakama zinaonyesha warufani hawakujua Jamhuri itaegemea kielelezio hicho.

“Hii maana yake kuwasilishwa kortini na baadaye kupokelewa kama kielelezo hakikuzingatia sheria, hivyo kilistahili kukataliwa. Tunaona hoja ya sita ya rufaa ina mashiko na tunaikubali,” walisema majaji hao.

Kuhusu hoja kuwa ushahidi wa utetezi haukuzingatiwa wakati jaji alipotoa hukumu yake, majaji walisema katika hoja hiyo kunaibuka masuala mawili, moja ni kuwa ushahidi wao haukuzingatiwa na pili, kama haukuzingatia, madhara ni nini.

Hata hivyo, majaji hao walisema rekodi zinaonyesha ushahidi wa utetezi ulifanyiwa kazi wakati jaji anatoa hukumu yake, ikiwamo utetezi wa kwamba hawakuwepo eneo la tukio (alibi), hivyo majaji wakaona hoja hiyo haina mashiko na kuitupa.

Hoja nyingine ya rufaa ni kuwa walitiwa hatiani wakati upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shtaka dhidi yao bila kuacha mashaka.

Majaji walisema ni msimamo wa kisheria kuwa yule anayetoa tuhuma dhidi ya mwingine ni lazima athibitishe tuhuma hizo na hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya ushahidi na kwamba katika kesi za jinai, jukumu hilo ni la upande wa mashtaka.

Kwa mujibu wa majaji hao, kuhusu nani alisababisha kifo cha marehemu, ushahidi wa mashahidi wa tatu na wa nne walitoa ushahidi namna alivyokufa mikononi mwa warufani.

“Ushahidi huo ulitoka kwa watu walioona tukio likitokea na kwamba ingawa walipingwa na warufani, upingaji wao ulikuwa wa jumla na hata walipojaribu kuingiza ushahidi wa alibi (hawakuwepo eneo la tukio) hawakuzingatia sheria,” walisema.

Majaji hao walisema ushahidi uliopo katika kumbukumbu za mahakama unaonyesha ushahidi wa Jamhuri uliegemea ushahidi wa shahidi wa tatu na wa nne ambao ni watu waliokuwepo eneo la tukio na waliona kila kitu kilichotendeka.

“Kuna mashahidi walioona kwa macho ambao ni ushahidi bora sana,” walisema majaji na kueleza kuwa mawakili wa utetezi walijaribu kutoboa mashimo kwenye ushahidi wa shahidi wa tano kwa kushindwa kuchukua tamko la kifo la marehemu.

“Kwa heshima kubwa hii haina dosari kubwa, hasa katika katika mazingira ambayo kulikuwepo watu waliotoa ushahidi kuhusiana na nini kilichotokea na ushiriki wa kila mrufani,” walisema majaji hao katika huku na kuongeza:-

“Tamko la kifo (dying declaration) lisingekuja na kitu tofauti au ushahidi bora zaidi wa nini kilisababisha kifo cha marehemu. Tunaikataa hoja hii.”

Katika hitimisho lao, majaji hao walisema kwa ushahidi uliokusanywa, ni warufani ndio walimuua marehemu na walikuwa na dhamira ovu ya kufanya hivyo na kusema kesi dhidi ya warufani ilithibitishwa bila kuacha mashaka.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts