Ni Mbowe au Lissu 2025 urais Chadema

Dar es Salaam. Joto la uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limeanza kufukuta, huku likiibuka swali la nani kati ya Freeman Mbowe na Tundu Lissu atapitishwa kuipeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi hiyo.

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, ameshaonyesha kusudio la kuwania wadhifa huo na tayari ameshamwandikia barua Katibu Mkuu, John Mnyika kuonyesha nia yake.

Sio siri tena, nia yake hiyo ameiweka wazi hata katika mahojiano mbalimbali aliyoyafanya katika vyombo vya habari, akisema amemwandikia Mnyika barua ya nia ya kugombea urais 2025 na nia ya kuwania nafasi aliyonayo sasa ndani ya chama hicho.

Mnyika amelithibitishia Mwananchi kwamba tayari barua ya Lissu imemfikia na itafuata taratibu za chama. Katika barua ya Lissu, ameonesha nia pia ya kutetea nafasi yake ya umakamu mwenyekiti kwenye uchaguzi ujao.

Wakati mambo yakiwa hadharani kwa upande wa Lissu, taarifa ambazo Mwananchi linazo kutoka ndani ya chama hicho, Mbowe ambaye ndiye Mwenyekiti wa Chadema, anatajwa kuwania tena urais mwakani.

Licha ya kukaa kimya na hata alipoulizwa na Mwananchi mara kadhaa hakujibu lakini duru za siasa zinaeleza naye ni miongoni mwa wanaoweza kukata tiketi ya kuomba ridhaa ya Chadema kuwania kiti cha urais.

Mwananchi linazo taarifa za ndani kuwa Mbowe atajitosa kuwania nafasi hiyo na tayari Lissu mara kadhaa amekuwa akisema ikitokea nafasi anayokusudia kuiwania, Mbowe ataitaka basi atamwachia.

“Kaka hilo la urais halina ubishi mpaka sasa ni Mbowe na umakamu bara ataendelea Lissu, hata kama kutakuwa na mtu hataki hatutakubali sijui Lissu asigombee urais, asigombee umakamu, hilo halipo,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, huku  akiomba asitajwe jina. Aliongeza:

“Ukiwaweka kwenye mizania na siasa za sasa za Rais Samia (Suluhu Hassan) Mbowe ni mtu sahihi, Lissu sawa ila si wakati huu. Lissu atarudi jimboni akasaidie bungeni wakati Mbowe akiwa anakwenda Ikulu.”

Chanzo hicho kilidokeza zaidi kwa kusema: “Hatutakuwa na mgombea mwingine zaidi ya hawa, Mbowe au Lissu. Hatutakuwa na mgombea sijui ametoka CCM au wapi. Mwaka huu tumejipanga wenyewe na kama itatokea Mbowe akasema hataki, Lissu ataendelea lakini Mbowe akijitosa tu imekwisha.”

Mjumbe mwingine wa kamati alisema: Jambo  linalowatofautisha wawili hao ni rasilimali fedha. Mwamba (Mbowe) ana fedha bwana, haitakuwa jambo gumu. Fikiria operesheni za kurusha chopa na magari anatoa fedha zake mwenyewe.”

Halitakuwa jambo jipya kwa yeyote kati yao kuwania urais, kwa nyakati tofauti walishawahi kushiriki kinyang’anyiro hicho, Mbowe katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na Lissu aligombea mwaka 2015.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Mbowe alipata kura 668,756 akishika nafasi ya tatu dhidi ya kura 9,123,952 za mshindi wa kiti hicho aliyekuwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete. Nafasi ya pili ilishikwa na Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyepata kura 1,327,125.

Wakati wa Lissu nao mambo yalikuwa hivyo hivyo, aliukosa urais kwa kupata kura 1,933,271 akishika nafasi ya pili dhidi ya mgombea wa CCM, John Magufuli aliyetetea wadhifa huo kwa kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.

Hata hivyo, wagombea wote hawana historia ya kushiriki au kufanya siasa nje ya Chadema, wote walisikika wakiwa upinzani na umaarufu wao wa kisiasa umetokana na chama hicho.

Katika historia ya Chadema, haikuwahi kurudia kumsimamisha mgombea aliyeshiriki kinyang’anyiro hicho, jambo linaloibua swali Je, mwakani kitamrejesha aliyewahi kushindwa nafasi hiyo?

Akihojiwa katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Kituo  cha Star TV usiku wa juzi Jumamosi, Lissu alisema alishamwandikia Mnyika barua ya nia yake ya kuwania urais mwaka 2025 na kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti bara katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

“Mwanachama anayetaka kugombea kwa mujibu wa kanuni kwa kutegemea nafasi anayotaka, anatakiwa kumwandikia Katibu wake wa ngazi husika barua ya kusudio la kutaka kugombea,” alisema.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa iwapo chama chake hakitampitisha yeye, atamuunga mkono mgombea yeyote atakayependekezwa na chama hicho kuwania nafasi hiyo.

“Sikuzaliwa nije kuwa mgombea urais wa Chadema nilijiunga na Chadema hata miaka 20 haifiki na nimefanya hivyo nikidhani ndicho chama chenye msingi wa ukweli wa mabadiliko ya kijamii na kila kitu. Nimekuwa tayari na niko tayari kutumikia nafasi yoyote ile,” alieleza.

Lakini, alisema atakaposhinda urais moja ya vitu atakavyofanya ni kujiuzulu wadhifa wake ndani ya Chadema ili kutenganisha dola na chama, tofauti na ilivyo sasa kwa CCM.

Sambamba na kujiuzulu kwake, alisema atabadili  Katiba ili kuweka msingi mzuri ili jambo hilo lisitokee atakapoingia mtawala yeyote.

Alipotafutwa kuzungumzia uamuzi wa kugombea au la, Mbowe simu yake iliita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya WhatsApp hakujibu.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alikiri kupokea barua za Lissu akitia nia katika nafasi hizo.

Kinachofuata baada ya hatua hiyo, alisema ni kupeleka kusudio hilo la Lissu mbele ya Kamati Kuu ya chama hicho kwa ajili ya uamuzi wa kupitishwa au vinginevyo.

“Muongozo wa utiaji nia katika kanuni za chama chetu (Chadema), mamlaka ya Katibu Mkuu yanaishia kwenye kupokea barua lakini si kutangaza majina. Hivyo nitapeleka Kamati Kuu kwakuwa ndiyo yenye mamlaka ya kuamua,” alieleza.

Alipoulizwa iwapo kuna barua za watia nia wengine mbali na Lissu, Mnyika alifafanua ni kinyume na kanuni za chama hicho kuliweka hadharani hilo.

“Nimekujibu kuhusu Lissu kwa sababu umeniambia mwenyewe ameweka wazi, sasa siwezi kuweka wazi kama nimepokea nia ya mwingine yeyote au la na siwezi hata kutaja ni kinyume na matakwa ya kanuni,” alisisitiza.

Wakati Lissu akiandika barua, Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa Viktoria, Ezekiel Wenje naye amekwisha kutangaza hadharani kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti-bara akieleza amejitathimini na kujiona anatosha kumsaidia Mbowe baada ya uchaguzi huo kufanyika.

Takwimu za Google Trends katika kipindi cha miezi mitatu yaani siku 90 zilizopita, zinaonyesha Lissu amefutiliwa zaidi ukilinganisha na Mbowe katika mikoa mitano ya Tanzania bara.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, katika Mkoa wa Morogoro Lissu alifuatiliwa kwa asilimia 66, dhidi ya asilimia 34 alizofuatiliwa Mbowe, vivyo hivyo katika Mkoa wa Arusha.

Katika Mkoa wa Pwani Lissu aliongoza kufuatiliwa kwa asilimia 60 dhidi ya asilimia 40 za Mbowe, huku mkoani Dodoma Lissu akiongoza kwa asilimia 70 dhidi ya 30 za Mbowe.

Ni Mkoa wa Kilimanjaro pekee ndiko ambako Mbowe ameongoza kufuatiliwa kwa asilimia 54, akimzidi Lissu aliyefuatiliwa kwa asilimia 46.

Ingawa Mbowe ana haiba ya kiuongozi, lakini Lissu anawavutia wapiga kura zaidi, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe.

Kwa mujibu wa Dk Kabobe, wawili hao wanatofautiana haiba ya kiuongozi na mvuto kwa wapiga kura,akisema  kila mmoja ana turufu yake kwa wanachama na wafuasi wa Chadema.

“Hawa  wawili wana siasa za tofauti mbele ya wapiga kura. Haiba  ya Lissu ni ya kimageuzi wakati Mbowe anawaza zaidi maridhiano. Mikikimikiki ya Lissu inaonekana kushawishi wapiga kura wengi zaidi ya Mbowe,” alieleza.

Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo, Lissu pia anabebwa na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja na kuifafanua kwa umma, ikaeleweka, tofauti na Mbowe.

Katika mazingira ya sasa, Dk Kabobe alisema Chadema inahitaji mgombea mwenye uwezo wa kujenga hoja na kuonyesha mbinu za kutatua changamoto za watu.

Kadhalika, alisema chama hicho kinahitaji mgombea mwenye uwezo wa kufafanua hoja zilizoibuliwa na zinazoibuliwa na wapinzani wao kwenye majukwaa ya kisiasa, akisisitiza:“Maoni yangu binafsi naona mtu sahihi zaidi kwenye haya ni Lissu.”

Aliongeza: “Kama Chadema wangeamua kuchagua mgombea leo nadhani turufu yao ingeenda kwa Lissu na kumwacha Mbowe abaki kama baba na mlezi wa viongozi wa sasa na wa baadaye ndani ya chama. Pengine tunaweza kuona tofauti kadiri muda unavyosogea,” alieleza mwanazuoni huyo.

Wakati Dk Kabobe akiwa na mtazamo huo, mhadhiri mwingine wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Mohamed Bakari alisema kuna mizania sawa ya nguvu za kisiasa kwa Lissu na Mbowe.

Kwa uwezo, historia, harakati na ushawishi wawili hao, alisema ni kama wanalingana, kunahitajika utafiti kubaini nani zaidi na sio kwa jicho la kawaida.

“Kwa hali ilivyo wote wana nguvu ya siasa. Ni vigumu kuonyesha nani zaidi bila utafiti, lakini nyakati zinabadilika tusubiri siku zijazo pengine ataonekana yupi zaidi,” alisema mwanazuoni huyo.

Katika hatua nyingine, kikao cha kamati kuu ya Chadema chini ya uenyekiti wa Mbowe kilichokutana kwa siku tatu, Agosti 8-10, 2024, pamoja na mambo mengi kilijadili uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Uchaguzi huo ambao tayari umemalizika kwa kanda nne za Magharibi, Ziwa Viktoria, Serengeti na Nyasa kati ya kanda 10.

Mwananchi limedokezwa na mmoja wa wajumbe wa kikao hicho kwamba uchaguzi wa ndani awali ulipangwa kufanyika Septemba 2024, lakini kutokana na uchaguzi ngazi ya kanda na mikoa haujamalizika ni vigumu kufanyika.

“Ni vigumu kwenda kwenye uchaguzi ngazi ya Taifa wakati ngazi za mikoa na kanda hatujamaliza, tumefanya kanda nne tu umeona shughuli yake, sasa twende kanda zote 10 halafu uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba.”

“Hiki ndicho kimetufanya tusogeze mbele hadi Desemba na kwa kuwa katiba yetu inaturuhusu kusogeza miezi sita mbele. Ili twende kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa tukiwa wamoja,” alidokeza mjumbe huyo..

Hilo linathibitishwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano wa Chadema, John Mrema alipiulizwa na Mwananchi ambapo alisema ni kweli wamesogeza uchaguzi huo mbele hadi Desemba.

“Tunataka kwenda kwenye uchaguzi tukiwa wamoja. Lengo ni kushinda mitaa, vitongoji na vijiji vingi. Wakati tunajiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi ngazi ya mikoa na kanda unaendelea,” alisema.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kikao hicho cha kamati kuu kilikuwa cha moto kwa baadhi ya ajenda ikiwemo ya baadhi ya viongozi na wajumbe kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari mara kwa mara.

“Ilikuwa kamati kuu ya moto kwelikweli, (anamtaja jina) alishughulikiwa kwelikweli, wanasema haiwezekani kiongozi anashinda Club House, X-Sapce na vyombo vya habari.

“Huko viongozi wanaongea mambo ambayo yanakigharimu chama kwa hiyo ilikuwa kufundana kwelikweli. Mfano (anatajwa jina) aliambiwa anapaswa kubadilika na kuishi kiuongozi kwani si kila jambo la kuzungumza na kama anazungumza anazungumza nini, na nani na wakati gani,” kilisema chanzo chetu.

Lissu ‘aibana’ Chadema

Juzi Jumamosi, Lissu alisisitiza msimamo wake wa kutaka kujibiwa kwa hoja za aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa ambaye sasa amejiunga na CCM.

Sambamba na hilo, alisisitiza pia msimamo wake wa kuondoka ndani ya Chadema iwapo kitakwenda kinyume na sababu zilizomfanya ajiunge nacho akisema, “Chadema sio mama yangu.”

Kwa mara ya kwanza, Lissu alionyesha msimamo wa kutaka kujibiwa kwa tuhuma zinazoibuliwa na Mchungaji Msigwa dhidi ya Chadema tangu Juni 2024 alipowasili nchini akitokea Ubelgiji.

“Kwa kuzingatia tuhuma zenyewe, zinatakiwa zijibiwe. Kama mali zisizohamishika majengo na chochote kitakuwa na nyaraka, lakini kama mali zinazohamishika kama fedha hizo vile vile zina nyaraka,” alisema Lissu alipozungumza na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Miongoni mwa tuhuma zinazoibuliwa na Msigwa dhidi ya Chadema tangu alipohamia CCM, Juni 30 mwaka huu, ni ufisadi anaodai upo ndani ya chama .

Moja ya matendo aliyoyarejea kama ya kifisadi ni fedha zaidi ya Sh2 bilioni walizochangishwa waliokuwa wabunge wa chama hicho mwaka 2015, ambazo alidai hadi sasa haijulikani zilipokwenda.

Lissu alisema kuna umuhimu wa mamlaka sahihi ndani ya Chadema kuzijibu hoja za Mchungaji Msigwa kuhusu ubadhirifu wa fedha.

Lissu alisema hawezi kuzijibu tuhuma hizo kwa sababu hana mamlaka kwa kuwa nyaraka zote za chama hicho, huwa chini ya ofisi ya Katibu Mkuu  ambaye ndiye anayepaswa kumjibu.

“Hoja za Msigwa sio ngumu kwa sababu rekodi za fedha zipo hizi fedha zinazosemwa zimeenda wapi kutakuwa na akaunti za chama ukimuuliza Katibu Mkuu wa chama au mtu wa fedha wa chama ana majibu,” alisema.

Suala la uamuzi wa kumjibu Mchungaji Msigwa, alisema wamekuwa wakilizungumza hata katika vikao vya ndani vya chama hicho.

Majibu hayo ya Lissu, yalitokana na swali aliloulizwa ni nini kinaifanya Chadema ikae kimya dhidi ya tuhuma zinazoibuliwa na Mchungaji Msigwa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano wa Chadema, John Mrema akijibu madai hayo alisema: “Kwa miaka mitano mfululizo chama kimepata hati safi ya ukaguzi kutoka Kwa CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) na Msigwa anajua alikuwa mjumbe wa vikao vya Kamati Kuu ambayo taarifa za fedha huwasilishwa.”

“Pili, kwamba ajibiwe kwa nyaraka, haiwezekani mtu akaenda kusema uongo huko hadharani, hana ushahidi kisha chama ndio kimsaidie ushahidi! Aweke ushahidi hadharani kwani tunajua anafanya porojo za kisiasa,” alisema Mrema na kuongeza:

“Tatu, mali zote za chama zipo salama chini ya bodi ya wadhamini ambayo ndio msimamizi mkuu wa mali zote za chama zinazohamishika na zisizohamishika. Aidha rejista ya mali hukaguliwa na CAG kila mwaka.”

Katika mahojiano hayo, Lissu aliweka wazi msimamo wa chama hicho kuendelea kushiriki chaguzi mbalimbali licha ya kudai kuwapo kwa mazingira magumu.

Alisema awali waliahidi kususia chaguzi zote zitakazofanyika bila ya uwepo wa Katiba mpya, lakini kwa sasa wameona ni vema washiriki kuonyesha upinzani.  

“Silaha ya kususia ni muhimu lakini inapaswa kutumika mara chache zaidi. Iwe silaha ya mwisho kabisa,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia uamuzi wake, Mbowe simu yake iliita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya WhatsApp hakujibu.

Baadaye alipopigiwa tena simu, iliita kisha ikakatikwa kwa kusema, “Simu unayoipigia inatumika.”

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917

Related Posts