Mwanza. Wakazi wa Kata ya Mabatini jijini hapa, wakishirikiana na Polisi Kata, wameanzisha mpango wa kuwaepusha vijana na vitendo vya kihalifu kwa kuwapatia elimu na mafunzo ya ujasiriamali.
Mpango huu pia unawalenga wajane, wastaafu, wanawake na wazee kwa lengo la kuwawezesha kupata vyanzo vya mapato.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumapili, Agosti 18, 2024, Mtaa wa Mabatini, Polisi Kata, Shabani Kashakala amesema mpango huo ulianzishwa baada ya kubaini kuwa kundi kubwa la vijana katika kata hiyo hawana ajira na baadhi yao wanajihusisha na uhalifu.
Kashakala amesisitiza kuwa vijana wanaoendelea kufanya uhalifu watachukuliwa hatua za kisheria, lakini wale wenye nia ya kujirekebisha watapewa mafunzo ya ujasiriamali ili kuwawezesha kujiajiri na kujipatia kipato halali.
“Baada ya kukaa na kufuatilia tumegundua vijana wa Mabatini wanahitaji kupata elimu ya ujasiriamali, wapo ambao ni wezi na wahalifu, hawa watakamatwa na kupelekwa kwenye haki yao, lakini ambao ni wema lazima wapate elimu ya ujasiriamali,” amesema Kashakala.
Mwalimu wa Ujasiriamali kutoka Emichem Enterprises, Daniel Mnyozi amesema Polisi pekee hawawezi kumaliza vitendo vya uhalifu katika jamii, lakini kupitia mafunzo ya ujasiriamali, vijana wataweza kujiajiri na hivyo kuepuka uhalifu.
Wananchi walioshiriki mkutano huo wamepongeza mpango huo, huku wakiomba vijana wanaojiingiza kwenye uhalifu wachukuliwe hatua kali.
Juma Ngereja, Katibu wa Baraza la Ushauri la Wilaya ya Nyamagana, amesema kuwa hatua hii itasaidia kupunguza uhalifu katika mtaa wao.
David Juma, kijana mkazi wa Mabatini, ameiomba serikali kuwawezesha kiuchumi vijana watakaopatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kuchangia maendeleo ya jamii.
Naye Balozi wa Shina Namba 06, Pilly Kamalamo amewahimiza mabalozi wenzake kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwakusanya vijana katika maeneo yao na kuwaunganisha na mafunzo hayo.
Kwa sasa, vijana na wananchi wa Mabatini wamepatiwa fursa ya kupata mafunzo ya ujasiriamali bure kupitia Emichem Enterprises, ambapo watajifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali kama sabuni na batiki.