MAISHA yako yanaweza au kuna mtu anafananishwa nayo iwe unajua au pasipo kujua.
Uko ule ule wa mwonekano kuanzia sura na wa matendo, tabia na mengine kama ilivyo kwa nyota wa soka, hapa namzungumzia Maxi Mpia Nzengeli na Ng’olo Kante.
Kwa mambo yao uwanjani na nje ya uwanja, unaweza ukaona kuna baadhi wanafanana na yanavutia ukiwatazama wote.
Maxi kwa tabia za ndani na nje ya uwanja kwa karibu zinafanana na kiungo wa timu ya taifa ya Ufaransa na klabu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia, Kante.
Nzengeli (24) winga wa kushoto wa Yanga na Kante (33) kiungo mkabaji ni wachezaji wanaoipenda kazi yao na pengine wanajivunia kutokana na kukubalika sana na mashabiki wa timu wanazozichezea.
Jina Nzengeli maana yake ni malaika kwa lugha ya Kilingala, huku la Ng’olo mwenyewe anasema linatokana na Mfalme wa zamani wa Mali ambaye alianzia maisha chini kabla ya kuwa mtawala mwenye nguvu wa taifa hilo la Magharibi mwa Afrika.
Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya tabia zao nje na ndani ya uwanja na kwa hakika zinawavutia mashabiki nwengi na wadau wa soka ulimwenguni hasa kwa Kante huku kwa Maxi kwenye soka la Afrika na hasa Tanzania jina lake linaimbwa sana.
Maxi na Kante kwa mwonekano ni wafupi na nyota wa Kicongo ana urefu wa futi 5 na inchi 7, huku Mfaransa Kante akiwa na urefu wa futi 5 na inchi 6.
Ukiwaona uwanjani na vimo vyao, unaweza ukadhani ni wakorofi, lakini nyota hawa, ni wapole na wana aibu na hata wakisababisha faulo au wakichezewa rafu, hutawaona wakizozana na wachezaji wa timu pinzani, zaidi watasikiliza hukumu ya mwamuzi na wao wataendelea na mchezo.
Kutokana na aibu aliyonayo Kante mwaka 2018 wakati ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa lake la Ufaransa, alikwepa kupigwa picha na wachezaji wenzake na alijificha nyuma ya staa mwenzake Paul Pogba.
Hata wakati wenzake wakishangilia ubingwa wa dunia mwaka huo, hakuwa sehemu ya waliolibeba kombe hilo hadi alipopelekewa ili na yeye alibebe, huku mastaa wa Ufaransa wakiimba jina lake.
Nzengeli pia hivyo hivyo ingawa kwenye picha za pamoja utampata lakini si mtu wa kushadadia mambo na hujiweka pembeni kuangalia wenzake.
Mfano ni wakati timu ya Yanga inaingia kukagua Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kucheza fainali za Ngao ya Jamii ambalo miamba hiyo ilibeba taji hilo, alikuwa mbele akiwa peke yake, huku akiwa amevalia spika za masikioni ‘airphone’ na kuna muda alikuwa anatazama nyuma kama kujishitukia, kujiona yupo mbali na wenzake.
Baadhi ya mashabiki walioshuhudiwa na Mwanaspoti, wakimsema Nzengeli hana mambo mengi ila wanafurahisha na nguvu anayoitumia uwanjani na msimu wake wa kwanza Yanga alifunga mabao 11.
Kuhusu upole wa Maxi, Nkane anasema “Napenda kumchokoza mara kwa mara ndiyo maana amenizoea na anaweza akaniomba nimfundishe Kiswahili, ana huruma na upendo kwa wengine.”
Nkane aliwahi kumfanyia mahojiano, akimuuliza anapenda kutoa pasi ama kufunga? Alijibu “Napenda sana kutoa asisti.”
Hii sio uwanjani pekee, bali hata kwenye mambo nje ya uwanja hasa mazoezini.
Maxi anatajwa ni mmoja wa wachezaji wa Yanga anayewahi zaidi kwenye uwanja wa mazoezi.
Pia kwenye ibada ni mtu anayezingatia muda na hakosi kuwahi kanisani na marafiki zake wa karibu wanasema; “Anapopata mapumziko na anajua ana ratiba ya kwenda kanisani, anajiandaa mapema na anapenda kuwahi pia ukiwa na ahadi naye ni vizuri ukazingatia muda ili mwende sawa.”
Kama ilivyo kwa Kante ambaye mazoezini ni mtu wa kuwahi na hana mambo mengi ya kumfanya achelewe. Pia kwenye mambo nje ya uwanja hujali muda na hata akiwa na ratiba za kukutana na mtu hilo ni muhimu.
Nidhamu nyingine ya kipekee kwa Maxi ni kuchomekea awapo kwenye mechi au mazoezini na hilo limekuwa likiwavutia sana mashabiki na hata klabu yake kutenga siku maalumu ya nyota huyo ‘Maxi Day’ na mashabiki waliingia uwanjani wakiwa wamechomekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Merreikh ya Sudan.
Kuna video ilikuwa inamuonyesha Nzengeli akiabudu moja ya makanisa jijini Dar es Salaam. Hii inaonyesha ni mtu anayependa ibada na kama wanavyosema rafiki zake, anapenda kuwahi kanisani.
Kante pia amekuwa akiabudu na mara kadhaa hupenda kwenda Makka, Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Umrah na waislamu hukutana kwenye msikiti mkubwa wa Makka.
Pia maisha ya kawaida, anapenda kufanya ibada.
Winga wa Yanga, Denis Nkane anashuhudia tabia za Nzengeli wanapokuwa kambini ama wakati mwingine akimtembelea nyumbani kwake “Mara nyingi kambini ukimkuta chumbani kwake, anakuwa anasikiliza nyimbo za dini, kifupi hana mambo mengi.”
Kutokana na imani aliyonayo Maxi, inaelezwa inamfanya awe na nidhamu ya juu kwa kila jambo, ili kuepusha migongano isiyo na sababu, kama kuwahi mazoezi, kula na kulala.
Nyota hawa si watu wanaopenda kujionyesha maisha yao kama mastaa wengi ambao wanachofanya lazima dunia ijue, iwe ni starehe au jambo lolote nje ya uwanja.
Unaweza ukadhani nyota hawa wawili wanacheza bure, lakini ukweli wanalipwa pesa nyingi lakini maisha wanayoishi ni ya kawaida.
Kante hamiliki magari ya kifahari na kuna wakati huchekwa na marafiki zake kwa aina ya gari analomiliki lakini huwa hajali na ndiyo maisha yake.
Maxi pia anamiliki gari la kawaida analolitumia hapa nchini, Crown Athletic na kwenye mitandao mara nyingi huposti picha za akiwa mazoezini au kwenye mechi.
Ni kawaida kwa mastaa kuona mabadiliko katika miili yao, kama kuvaa herini, kuchora tatoo,kubadili rangi za miili yao, ila ni tofauti kwa Kante na Nzengeli ambao wananyoa kawaida na hakuna kilichobadilika kwao.
Kuna wakati mwingine kwa Kante upendo wa mashabiki unamfanya aonyeshe tu tabasamu, huku akiwa na aibu kubwa ya kushindwa kuendana na vaibu lao, pia siyo mchezaji anayependa kujichanganya na wenzake, muda mwingi anajitenga.
NDANI YA UWANJA NI HATARI
Nzengeli akiwa uwanjani, ana kasi wakati mwingine anaibia majukumu ya wengine wanapojisahau, ndivyo ilivyo kwa Kante ambaye anakuwa msaada mkubwa kwa mabeki na ana kasi.
Nzengeli ndiye aliyeivusha Yanga kutinga fainali, baada ya kuifunga Simba bao 1-0, ukiachana na hilo,kiwango alichokionyesha Afrika Kusini, Yanga ikinyakua taji la Toyota Cup, timu nyingi zilivutiwa na kiwango chake, ila ikawa ngumu kwa viongozi kumuachia.
Kante ana CV kubwa kuliko Nzengeli, kutokana na timu alizochezea na mafanikio aliyopata pia kiumri ni mkubwa.
Kwenye timu ya taifa anatajwa ni mmoja wa nyota wa kutegemewa kwani mchango wake ni mkubwa kwenye kubeba mataji na anapendwa na nyota wenzake hadi kumtungia nyimbo za kumsifia.
Maxi katika Ligi Kuu ya msimu uliopita alicheza dakika dakika 2090, mabao 11, asisti 2, mechi alizocheza 23.
Kante alizisaidia timu alizopita kama Leicester City, Chelsea, Al Ittihad aliko sasa na kwa jumla timu alizocheza amefunga mabao 21, mechi alizocheza ikiwa ni 370.
Msimu uliopita, ulikuwa msimu wa kwanza kwa Maxi kucheza Yanga, aliisaidia kuchukua taji la Ligi Kuu, FA, Toyota Cup baada ya kualikwa Afrika Kusini na Ngao ya Jamii ya ufunguzi wa Ligi msimu 2024/25.
Hata Kante akiwa na Leicester City na Chelsea alizisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na mataji mengine, makubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2020/21.
Kiungo wa zamani wa Azam na Simba, Joseph Kimwaga anakiri anaona mfanano wa baadhi ya tabia kwa mastaa hao, licha ya kucheza levo tofauti za ligi.
“Inatokea kwa wachezaji mbalimbali, kuna watu ambao walikuwa wakiniona wananifananisha na Sadio Mane, hivyo naona ni jambo la kawaida.”
Staa wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi anasema “Nikiwaangalia kimo ni kama wanaelekeana, wapole, hawana mambo mengi ila uwanjani wote wanajua, ingawa Kante kafanya makubwa zaidi kulingana na aina ya ligi anayocheza.”
2013–2015:Caen
2015–2016:Leicester City
2023–Al-Ittihad ya Saudi Alabia
2016:Bingwa Ligi Kuu England
2016: Ufaransa fainali Euro 2016
2017:Bingwa Ligi Kuu England
2017:Mchezaji Bora wa kulipwa
2017:Mchezaji bora wa Ligi Kuu
2017:Mshiriki tuzo ya Ballon d’Or
2018:Bingwa Kombe la Dunia