Siku nyingine ya Simba kujiuliza

Makocha Fadlu Davids wa Simba na Francis Kimanzi wa Tabora United leo kila mmoja ataanza kuonja joto la Ligi Kuu Tanzania Bara wakati timu zao zitakapokutana kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Wawili hao wote hii ni mara yao ya kwanza kufundisha ndani ya ardhi ya Tanzania baada ya timu zao kuwanasa katika dirisha lililomalizika hivi karibuni la usajili.

Timu hizo zimekutana mara mbili ambazo zote zilikuwa ni katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita ambapo Simba ilivuna pointi sita katika mechi hizo.

Mchezo wa kwanza, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 ikiwa ugenini na zilipokutana mara ya pili, Tabora United ilipoteza kwa mabao 2-0.

Simba imekuwa na historia nzuri ya ushindi katika mechi za mwanzo za msimu ambapo imekuwa ikipata matokeo mazuri mara kwa mara na kuthibitisha hilo, imepata ushindi katika mechi nane kati ya 10 za mwanzo kwenye misimu 10 iliyopita, ikifunga mabao 26 sawa na wastani wa mabao 2.6 kwa mechi na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.

Tabora United ambayo huu ni msimu wake wa pili kushiriki Ligi Kuu, mechi moja iliyocheza nyuma ya kwanza kwenye msimu haikuacha kumbukumbu nzuri kwao kwani walipoteza kwa mabao  4-0 mbele ya Azam FC na hivyo leo ni fursa kwao kuondoa nuksi kwa kupata ushindi dhidi ya Simba.

Hata hivyo, Tabora United imefanya marekebisho makubwa ya kikosi chake msimu huu kulinganisha na uliopita ambapo hivi sasa inao nyota kadhaa ambao kama Simba isipowachunga wanaweza kuamua matokeo ya mchezo kwa upande wao.

Timu hiyo kutoka mkoani Tabora imekuwa na nuksi na mechi za ugenini kwenye Ligi Kuu kwani tangu ilipopanda daraja, haijawahi kupata ushindi katika mechi zote za ligi ilizocheza ugenini.

Msimu uliopita katika mechi 15 za Ligi ilizocheza ugenini, ilitoka sare tano na kupoteza michezo 10 huku ikifunga mabao saba na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26.

Simba nyumbani imekuwa haina unyonge na hilo linajidhihirisha kwa matokeo ya mechi 15 za Ligi Kuu msimu uliopita ilizocheza ikiwa nyumbani ambapo imepata ushindi mara 11, imetoka sare mbili na kupoteza michezo miwili na imefunga mabao 30 huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12.

Matumaini makubwa kwa Simba leo hapana shaka yapo kwa mshambuliaji wake mpya Leonel Ateba ambaye timu hiyo ilimsajili siku ya mwisho ya kufungwa kwa usajili wa dirisha kubwa, Agosti 15 akitokea USM Alger ya Algeria.

Tabora United inaonekana itaelekeza matumaini makubwa kwa mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa na ligi kuu ya Tanzania, Heritier Makambo ambaye aliwahi kuitumikia Yanga miaka ya nyuma kwa nyakati mbili tofauti.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema wanahitajika kuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi kwa kushinda leo.

“Tunahitaji kuwa na mafanikio msimu huu. Kwenye kila mechi ya ligi tuna malengo ya kupata pointi tatu na naamini mechi ya kesho (leo) itakuwa hivyo kutokana na maandalizi tuliyoyafanya na wachezaji wangu,” alisema Davids.

Kocha wa Tabora United, Francis Kimanzi alisema kuwa wanaipa heshima Simba lakini wamejipanga kuwadhibiti.

“Ni mechi nzuri ya kutupa changamoto kwa ajili ya mechio zitakazofuata. Mpango wetu kimbinu utabadilika na nadhani mtaona. Kila mechi tunakuwa na staili ya kucheza,” alisema Kimanzi.

Mchezo huo wa Simba na Tabora United utatanguliwa na ule wa Kengold dhidi ya Singida Black Stars ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuanzia saa 10:00 jioni.

Ni mechi ya ukaribisho kwa Kengold ambayo ndio inashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tofauti na Singida Black Stars ambayo huu ni msimu wake wa tatu.

Hata hivyo, katika misimu miwili ambayo timu hiyo ilishiriki, ilikuwa ikijulikana kama Ihefu SC hivyo huu ni msimu wa kwanza ikicheza Ligi Kuu kwa kutumia jina la Singida Black Stars.

Related Posts