Siku moja baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipiga mkwara Tabora United kuwa itaichukulia hatua ya kinidhamu kwa kuendelea kufanya kazi na Yusuph Kitumbo aliyefungiwa maisha kujihusishwa na soka, uongozi wa timu hiyo umeibuka na kumruka ukidai haumtambui kama kiongozi wa klabu hiyo.
TFF jana ilitoa onyo la mwisho kwa Tabora United ambayo jana ilikuwa uwanjani kupepetana na Simba katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu, kwa mdai imekuwa ikishirikiana naye licha ya kutambua amefungiwa maisha kujihusisha na soka tangu Mei mwaka jana.
Taarifa ya TFF iliyosainiwa na Ofisa Habari, Cliford Ndimbo ilieleza Tabora ilishaandikiwa barua kuitaka iachane na Kitumbo, lakini imekuwa ikikaidi na shirikisho lilikuwa likijipanga kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya uongozi wa klabu hiyo iliyokuwa ikifahamika kama Kitayosce.
Hata hivyo, mapema jana Tabora ilitoa taarifa kwa umma ikimruka Kitumba, ikisema sio sehemu ya uongozi na wala haishirikiani naye kutokana na kutambua aliadhibiwa tangu mwaka jana.
Taarifa ya Tabora iliyosainiwa na Ofisa Habari, Christina Mwagala inasema inatambua taratibu, sheria na kanuni zote zinazotolewa na mamlaka ya soka nchini na kwamba haumtambui Kitumbo na umma uelewe kwamba hawashirikiani naye.
Kabla ya kifungo hicho, Kitumbo ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (Tarefa) na alikutwa na hatia sambamba na Ulimboka Mwakingwe aliyekuwa kocha wa Fountain Gate iliyovaana na Kitayosce katika mechi ya Championship waliyiodaiwa kupanga matokeo.
Kabla ya adhabu ya mwaka jana, Kitumbo aliwahi kuadhibiwa kwa tuhuma kama hizo mwaka 2016 wakati TFF ilipozishusha daraja, Polisi Tabora, Kanembwa JKT, Oljoro JKT na Geita Gold na kuiopandisha Mbao FC, japo adhabu hiyo ilikuja kufutwa baadae.