Mirerani. Madini ya Tanzanite yenye thamani ya Sh18.6 bilioni yamesafirishwa kwenda kuuzwa nje ya nchi, tangu kuanzishwa kwa soko la madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Nchagwa Chacha Marwa ametoa taarifa hiyo leo Jumapili, Agosti 18, 2024 wakati akisoma taarifa ya utendaji kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliyefanya ziara wilayani Simanjiro. Marwa amesema Serikali imepata mrabaha na ada ya ukaguzi ya Sh1 bilioni kutokana na madini hayo yaliyosafirishwa nje ya nchi.
Amesema vibali 700 vimetolewa tangu kuanzishwa kwa soko hilo mwaka 2024 kwa ajili ya kusafirisha madini yenye thamani ya Sh38.4 bilioni nje ya nchi.
Hata hivyo, Marwa amebainisha kuwa uzalishaji katika eneo hilo ni hafifu kutokana na changamoto za miundombinu, ikiwemo umeme, barabara, maji na mawasiliano, hali inayosababisha wachimbaji kutumia gharama kubwa kuzalisha madini.
Marwa amesema baadhi ya changamoto ni migogoro ya mara kwa mara inayotokana na mitobozano chini ya ardhi katika njia za uchimbaji na migogoro ya umiliki wa leseni, ambayo husababisha wachimbaji wengi kusitisha shughuli za uchimbaji.
Naye Waziri wa Madini, Mavunde amesema mchakato wa kuongeza thamani na biashara ya madini hayo utaendelea kufanyika Mirerani. Amesisitiza kuwa suala hilo lipo kikanuni na hakuna atakayeweza kubadilisha uamuzi huo baada ya Rais na waziri mkuu kutoa maelekezo.
“Serikali inajenga jengo kubwa la ghorofa, na Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia Sh800 milioni zaidi ili kufanikisha ujenzi huo kwa asilimia 99, hivyo biashara ya madini ya Tanzanite haitaondolewa Mirerani,” amesema Waziri Mavunde.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Nchini (Femata), John Bina amesema madini ya Tanzanite yanapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa kwani yanapatikana Mirerani pekee duniani.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala amempongeza Waziri Mavunde kwa kujitolea siku nzima kutembelea machimbo ya madini na kuzungumza na wadau bila kuchoka. Ameongeza kuwa Serikali ipo mbioni kufanikisha upatikanaji wa maji, zahanati na ukarabati wa barabara kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite.