Dar es Salaam. Kukithiri kwa vitendo vya mawakili ‘vishoka’ kumekiibua Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutangaza mkakati wa kuwashughulikia kwa kuunda kamati ya kitaifa inayolenga kuimarisha ubora wa huduma za uwakili nchini.
Mbali na kamati ya kitaifa, kila mkoa utakuwa na kamati yake kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.
Kamati hizo za kushughulikia mawakili vishoka ngazi ya mikoa nchi nzima zitashirikiana kikamilifu na Jeshi la Polisi na watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Hayo yamesemwa na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi wakati akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Agosti 18, 2024 lililotaka kujua hatua wanazochukua kuwakabili mawakili vishoka.
Msingi wa Mwananchi kumtafuta Mwabukusi ni tukio lililotokea Agosti 14, 2024 ambapo mawakili vijana wa Kanda ya Bagamoyo, inayoibeba (Kinondoni, Ubungo na Bagamoyo) kwa kushirikiana na TLS kumkamata mtu anayedaiwa kutoa huduma za uwakili kinyume cha sheria.
Mtu huyo anayedaiwa kuitwa John Malamoko (38), Mkazi wa Segerea, jijini Dar es Salaam, ambaye jina alilokuwa analitumia kama wakili ni Adam Mbaga alikamatwa wakati akimuhudumia mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Mawakili Vijana ya Taifa (AYL-Excom), Wakili Aristarko Msongela, amedai mtuhumiwa huyo amekuwa akitumia jina la Adam kwenye mihuri ya kughushi.
Msongela ameeleza mtu huyo amekuwa akitoa huduma za kughushi kwa zaidi ya watu 3,000, wakiwemo wanafunzi waliokuwa wakihitaji mikopo.
“Kisheria, watu wote ambao wamegongewa muhuri wa kuhakiki vyeti vyao na Adam wamepata mikopo na kazi isivyo halali, kwani aliyewapatia huduma hiyo hatambuliki kisheria,” amesema Msongela.
Kwa mujibu wa Msongela kumiliki muhuri wa sheria kuna vigezo kikiwamo cha lazima kupitia Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), ufaulu na kuomba kuwa wakili hivyo amedai Adam ni kishoka.
“Hata kama mtu amesoma sheria au shahada bila kupita Law School na jina la muhusika halipo katika orodha bado mtu huyo ni kishoka,” amesema Msongela.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Foka Dinya amesema Agosti 14, 2024 walimkamata Malamoko.
“Huyu kijana ni mfanyabiashara lakini alikuwa anatoa huduma ya uwakili au kujifanya wakili bila kuwa na utambulisho wa kisheria, alikamatwa katika steshenari moja inayofahamika kwa jina la Njiapanda,” amesema Dinya.
Amesema taarifa zilizagaa mtandaoni ndipo mmoja ya mawakili ambaye akimtaja kwa jina moja la Sadick alitilia shaka na aliamua kufuatilia kwa karibu na baadaye kutoa taarifa katika kituo cha Polisi lilichopo UDSM na kumkamata.
Katika upekuzi waliofanya mtuhumiwa alikutwa na mihuri miwili aliyoitengeneza ambayo alikuwa akitolea huduma kwa kutapeli watu, kwani hakuwa na sifa ya kuwa wakili na amefanya jambo hilo kinyume cha sheria.
“Hadi sasa bado yupo kituo cha polisi na upelelezi unaendelea pindi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani,” amesema.
Akizungumzia mikakati ya TLS kukomesha mawakili vishoka, Mwabukusi amesema kamati hizo zitashirikiana na Jeshi la Polisi katika kukamata na kuwachukulia hatua mawakili hao vishoka ambao wamekuwa chanzo cha mikataba mibovu na kutozingatia haki za kisheria, hususan katika uuzaji wa ardhi na mali nyinginezo.
Mwabukusi amesema mawakili hao vishoka wamekuwa wakitumia njia za udanganyifu, ikiwemo kughushi nyaraka na kuuza mashamba ya watu kinyume cha sheria, hali inayosababisha hasara kubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tumefuatilia kwa undani zaidi kwa sababu wanavyotoza pesa na kujiratibu hawafuati misingi ya kisheria,” amesema Mwabukusi.
Katika jitihada za kudhibiti vitendo hivi, TLS imeanzisha kamati za mikoa zitakazofuatilia kwa karibu vitendo vya mawakili vishoka na hadi sasa wameshakamata watu sita.
Mwabukusi ameongeza kuwa huduma zote za uwakili zinapaswa kuthibitishwa kwa muhuri rasmi na risiti za kielektroniki (EFD), ili kuhakikisha wakili anayetoa huduma anatambulika kisheria.
Kwa upande wa wananchi, Mwabukusi amewasihi kuepuka huduma za mawakili wasiokuwa na ofisi rasmi, badala yake kutafuta huduma katika ofisi zinazotambulika na TLS.
“Wananchi waache kupenda vitu vya bei rahisi kwa kukimbilia Sh2,000 ambayo baadaye itamletea hasara ya mamilioni,” amesema.
Alichokisema Profesa Anangisye
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye ametoa tahadhari endapo itagundulika wanafunzi wamepata mikopo kwa kutumia nyaraka za kughushi, itakuwa ni hasara kubwa kwa chuo na kwa Taifa.
“Leo hii bodi ya mikopo ikisimamisha mikopo yake kwa wanafunzi ambao wamekutana na hiyo changamoto, watashindwa kusoma na kitakachotokea ni hasara si tu kwa chuo bali kwa Tanzania nzima,” amesema Profesa Anangisye.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi kufuata utaratibu unaoeleweka ili kuepuka matatizo kama hayo.
Vilevile, ametoa wito kwa TLS kuongeza umakini na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuzuia madhara yanayowakumba wanafunzi na wazazi.
Yusta Gabnus, mfanyakazi wa steshenari alipokamatiwa mtuhumiwa, alikiri kufanya kazi na Adam kwa muda mrefu bila kujua kama alikuwa tapeli.
“Nimefanya naye kazi muda mrefu na wala sikujua kama ni tapeli hadi alipokamatwa. Hapa aliacha namba zake za simu na watu wakiwa na shida tunawapa namba wanawasiliana naye, kisha anakuja hapa na kuwasaidia,” amesema Yusta.
Yusta ameeleza Adam alikuwa maarufu kwa bei nafuu, akitoza Sh15,000 kwa kugonga mihuri kwenye vyeti vitano, tofauti na wengine wanaotoza kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000 kwa cheti kimoja.
Meneja Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Veneranda Malima amesema ukifanyika uchunguzi na ikibainika taarifa zilizotolewa na mnufaika ni za kughushi anasimamishiwa mkopo.
“Kutokana na vigezo vilivyoandikwa kwenye mkataba wake na ikabainika ameghushi nyaraka zake mkataba wake utasitishwa,” amesema Veneranda.