Mbeya. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB) imejitosa kufuatilia sakala la Jeshi la Polisi kuzuia maadhimisho ya siku vijana yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).
Maadhimisho hayo yalikuwa yafanyika Agosti 12, 2024 katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.
Hata hivyo, maadhimisho hayo hayakufanyika baada ya kuzuiliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi huku zaidi ya viongozi na wanachama wa Chadema 520, pamoja na waandishi wa habari walitiwa nguvuni.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Makamu wake Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu.
Pia, viongozi wa Bavicha wakiongozwa na Mwenyekiti wake, John Pambalu, Makamu wake-bara, Moza Ally na katibu mwenzi wa baraza hilo, Twaha Mwaipaya.
Mbali na kukamatwa, baadhi yao walidai kupata kipigo kutoka kwa askari polisi. Lissu, Mnyika na Sugu wamewahi kuwaeleza waandishi wa habari jinsi walivyokamatwa usiku wa Agosti 11, 2024 kisha kupata mateso wakati wakisafirishwa kupelekwa vituoni Njombe na Iringa.
Chadema limekwisha kuweka wazi kwamba litawafunguliwa mashtaki kwa majina yao, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kutokana na kuchangia kadhia zilizowapata.
Leo Jumapili, Agosti 18, 2024, Mwananchi limemtafuta Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Methew Mwaimu kujua kipi wanakifanya kutokana na tukio hilo ambalo liliwaibua wadau mbalimbali za haki za binadamu ndani na nje, mabalozi kuliliaani.
Jaji Mwaimu katika maelezo yake amesema wanaendelea kufanyia kazi suala hilo na tume itatoa taarifa muda si mrefu.
“Kuna kazi itafanyika, taarifa kamili ya Tume itatoka muda si mrefu,” amesema Jaji Mwaimu huku akifafanua kuna kazi inayoendelea.
Wakati huohuo, Chadema Mkoa wa Mbeya kimelaani tukio hilo wakidai kukamatwa kwa viongozi wao ni kuwadhalilisha.
Mwenyekiti wa chama hicho Mbeya, Masaga Kaloli akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, amedai katika tukio la Agosti 11 na 12 Jeshi la Polisi lilitumia vibaya madaraka kwa kuwapiga na kuwajeruhi wafuasi wa chama bila kujali nafasi za viongozi.
“Lakini tunamshukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kwa busara aliyotumia kumuomba katibu Mkuu wa Chadema kupanda gari kwa busara tofauti na baadhi ya askari polisi waliokuwa wakiwashurutisha viongozi wa Chadema kwa kuwapiga na kuwadhalilisha,” amesema.
“Hata kama tukimpongeza RPC (Kuzaga) akashushwa cheo ni sawa, lakini pia katibu Mkuu wa CCM, Dk Emanuel Nchimbi kwa kauli yake ya kuwataka viongozi wa Chadema watolewe ndani, tofauti na wengine walionyamaza hadi sasa,” amesema Kaloli.
Kaloli amesema pamoja na njama hizo kuwazuia wananchi kupata haki zao za kuwasikiliza viongozi wao, lakini hawarudi nyuma na mwaka huu wamejipanga kushiriki vyema uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025.
“Zipo mali hadi sasa hazijarejeshwa kwa wafuasi wetu, lakini ofisi za kanda yetu ziliharibiwa kwa milango mitatu, hivyo tunaendelea kufanya tathimini kujua gharama yake na Polisi wajitathimini,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa huo, Elisha Chonya amesema kutokana na kuzuiwa maadhimisho yao, wamependekeza Septemba 14 siku ya Demokrasia duniani au Siku ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 14 waadhimishe siku hizo jijini Mbeya, ili kukata kiu yao.
Amesema nguvu waliyotumia Polisi kushika na kuwapiga Chadema, haikuakisi kile kinachoelezwa kuhusu maridhiano.
“Yeyote atakayehusika kuhujumu uchaguzi ujao tutashughulika naye, vijana tunayo nafasi ya kuhakikisha Taifa letu linakuwa salama, tutafute uhuru wa nchi na maendeleo ya kweli,” amesema Chonya.