Tuanze mjadala huu na kisa cha unyenyekevu na uelevu. Siku moja, nchini Marekani, mwandishi mmoja alimsifia Nelson Mandela akimhoji.
Alimwambia kuwa alikuwa mtakatifu. Mandela alimkatiza hata kabla ya kumaliza na kusema “mie si mtakatifu, vinginevyo unamwongelea mtakatifu mwenye dhambi anayehangaishwa na dhambi zake.”
Hakuna mwanandoa mtakatifu wala shetani, bali binadamu mwenye kila udhaifu. Hatumaanishi kuwa binadamu hana ubora.
Mke au mmeo ni kiumbe dhaifu aliyeumbwa mwisho, kama tutaamini katika ngano za dini za kigeni. Huko hatuendi, japo bado zinatuendesha hadi kuathiri mahusiano na ndoa zetu. Hivyo, hazikwepeki, vinginevyo tujikomboe nazo.
Kama kichwa cha habari kinavyosema, huoi au kuolewa na malaika japo wapo waja shetani. Tumetumia neno malaika sababu, tumeambiwa, kuaminishwa na kuamini ni viumbe wasiokosea kwa mujibu wa Ukristo na Uislamu. Katika kutafiti, tumegundua kuwa watakatifu ni watu wa kawaida waliopewa utakativu na Kanisa Katoliki kwa sababu lijuazo iwe kweli au vinginevyo. Huko pia hatuendi, japo bado kuna athari zake katika maisha kwa wale waziaminio.
Waingereza husema kuwa mwanamke anayetafuta mume kumuoa anatafuta Mr Right. Mwanamume hutafuta Miss Right kumaanisha anayefaa lakini siyo mtakatifu. Nawe, kama yeyote, unatafuta anayekufaa lakini si mtakatifu. Utampata wapi? Kwani u mtakatifu? Unatafuta au kutafutwa na mtu kama wewe.
Je, inakuwaje watu huwapata Mr and Miss Right wakaishia kuwa kinyume? Hili swali linaweza kujibika baada ya kuandika vitabu hata kumi au zaidi.
Turejee kwa Mandela. Siku moja alikuwa na mazungumzo na kibinti cha miaka mitano kilichotaka kujua umri wake. Mandela alijibu kuwa alikuwa amezaliwa miaka mingi iliyopita. Kibinti kiliuliza ‘miaka mitano iliyopita?
Mandela alijibu ‘miaka mingi kuliko hiyo.” Kilimuuliza. Ni kwa nini ulifungwa? Mandela akajibu “sikufungwa kwa vile nilitaka. Kuna watu walinifunga.”
Kibinti kiliuliza tena “nani?” Mandela alijibu “watu ambao hawakunipenda.” Kibinti kiliuliza “ulikaa kule kwa muda gani? Mandela alijibu “siwezi kukumbuka ila ulikuwa ni muda mrefu kweli.” Kilisema “wewe ni mzee mpumbavu, si ni kweli?”
Je, tunajifunza nini? Kwanza, tunaowatafuta au kuwapata kama wenzi wetu si watakatifu. Tunaweza kuwaona hawatufai au wapumbavu, hata sisi wenyewe wapumbavu lakini ndiyo binadamu.
Sisi tuna msemo kuwa unaweza kumuogopa na kumuepuka mjusi ukajikuta unamkumbatia chatu na mamba katika ndoa.
Pili, wale ambao hawajaingia kwenye ndoa, wanaweza kutuona kama wazembe hata wapumbavu kwa kuchagua tuliowachagua au kuishi tulivyoishi wasijue zamu yao itafika.
Tatu, kabla ya kumhukumu mwenzako jihukumu. Kabla ya kulaumu jichunguze, kutaka kilicho bora hakikisha u bora.
Muhimu, usisahau kuwa wote ni wanadamu viumbe dhaifu kuliko hata wadudu na wanyama. Kondoo, mbuzi, ng’ombe, na wanyama wote huwa hawaogi wala kupiga mswaki kama sisi. Wakioga, hawatumii sabuni wala kujifukiza utuli. Je, sisi twaweza kukaa wiki bila kufanya hivyo tusinuke? Tia akilini.
Wapo wanaowatafuta wenzi wakamilifu nao si wakamilifu? Wanaowatafuta matajiri na wasomi bila wao kuwa navyo. Watafuatao bikra ilhali wao si bikra, watafutao Mr au Miss Right. Je, wewe vipi?
Kama unamsaka mtakatifu umuoe au akuoe, umenoa. Japo binadamu si malaika, vilevile si shetani, japo wapo mashetani.
Hivyo, unapochagua, usitafute mtakatifu ila waepuke mashetani. Je, mashetani ni wapi? Ni wengi tu. Mfano, wenzi wanaokuja kwa lengo la kumega familia au kukutenga na familia yako au wanafamilia yako, wanaotaka kukutenga na mwenzi wako, wote ni mashetani.
Wambea wanaozusha mambo ni mashetani. Mfano, mwenzi asiyejiamini wala kutunza siri ya ndoa ni, mshirikina, mzinzi, na muongo ni shetani. Aliyeolewa kuchuna buzi na kuchuma kwa ajili ya familia na ndugu zake ni shetani. Anayejiona bora kuliko wewe ni shetani. Orodha ni ndefu sana.
Tumalizie. Unapotafuta mwenzi, hakikisha unajiakisi mwenyewe ili upate unayefanana naye. Kama u mwovu usitegemee kumpata mwema, ingawa wema wanaweza kuangukia kwenye mikono ya mitego ya waovu.
Wewe si mkamilifu. Hivyo, umtafute mwenzi mwanadamu ila si malaika wala mtakatifu, kwani, hutampata kwa vile hayuko. Epuka kuchagua kupita kiasi, usijeambulia koroma kama mchagua nazi au kuishia na manonihiyo kama achambaye sana.